Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Kasongo anafanya nini India?

Almasi Kasongo India Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo

Wed, 19 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya umri wa miaka 17 zinaendelea huko Goa, India, na Timu ya Taifa ya Tanzania, Serengeti Girls, inafanya vizuri.

Lakini katika viongozi kutoka Tanzania walioko huko ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo.

Mtu unaweza kujiuliza, Kasongo anahusikaje na Timu ya Taifa...anafanya nini India? Bodi ya Ligi ni chombo (huru?) kinachosimamia na kuendesha ligi yetu.

Chombo hiki kilichoanza kama kamati ya kusimamia ligi, kilikuwa na majukumu ya kusimamia Ligi Kuu pekee na baadaye kuongezewa Ligi Daraja la Kwanza na La Pili.

Bodi ya Ligi haiingiliani majukumu yake na timu za taifa, hivyo watendaji wake hawahusiki kwa lolote kwenye timu za taifa.

Sasa Kasongo kama mtendaji mkuu, anaendaje India katika msafara wa timu ya taifa?

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, naye yuko India (kituko) lakini anaweza kujificha kwenye kichaka cha umakamu wa Pili wa Rais wa TFF.

Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Walace Karia ambaye hata hivyo siyo lazima aende, anaweza akawa amemtuma kumwakilisha, japo nalo linaweza kuhojiwa pia kwa sababu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao naye yupo huko.

Lakini Kasongo anamwakilisha nani, kwanini?

Nafasi ya Kasongo ingeweza kuchukuliwa na hata kocha fulani mzawa ili akajifunze kiufundi. Au ingeweza kuchukuliwa na mchezaji mwingine wa ziada akajifunze kwa kuona mashindano.

Ronaldo de Lima alichukuliwa na Brazil kwenda Kombe la Dunia 1994, Marekani, akajifunze. Theo Walcott alichukuliwa na England kwenda Kombe la Dunia 2006 ili akajifunze.

Na sisi tungeweza kumchukua mchezaji mmoja chipukizi akajifunze, badala ya kumchukua Kasongo ambaye hahusiki na lolote. Bodi ya ya Ligi inapaswa kuwa chombo huru ambacho kitasimamia ligi kwa maslahi ya wadau wa ligi ambao ni klabu za soka.

Lakini kwa tabia hii ya viongozi wa Bodi ya Ligi kuhongwa safari za timu ya taifa, Bodi haiwezi kuwa huru kutoka TFF hata mara moja.

Ni lini Kasongo ataweza kuwa na jeuri kama ya Silas Mwakibinga, kubishana na TFF pale linapokuja suala lisilo na maslahi kwa klabu?

Haiji kutokea kwa sababu tayari anafungwa mdomo na hivi visafari vya India.

Watendaji wa Bodi ya Ligi wanajiona kama wameajiriwa na TFF badala ya klabu ambazo ndiyo wamiliki wa bodi.

Badala ya kukaa na kutafakari ni namna gani Bodi ya Ligi italeta fedha zaidi kwenye ligi zake, mtendaji mkuu yuko India anaangalia Kombe la Dunia.

Ligi Kuu ina udhamini dhaifu, Ligi Daraja la Kwanza na La Pili hazina udhamini, mtendaji mkuu anakula bata India, siyo shida zake.

Nasema Ligi Kuu ina udhamini dhaifu kwa sababu mdhamini wake mkuu ni NBC ambayo inatia fedha kiduchu kwa uwezo wao.

Inatakiwa kupambana kuongeza udhamini kwenye ligi, lakini mtendaji mkuu yuko India, anakula bata.

Badala ya kupambana kuongeza thamani za klabu ambazo ndiyo wadau wake, mtendaji mkuu yuko India akifurahia Kombe la Dunia.

Nadhani kuna haja ya kuchunguza kwa kina vitabu vya hesabu vya TFF na kuhoji Kasongo anahusikaje na Kombe la Dunia kiasi cha kumpeleka huko kwenye ‘picnic.’

TFF wenyewe wanatumia gharama hizi huku ligi zake, Ligi Daraja la Tatu na La Nne zina changamoto kubwa.

Idara yake ya habari haina kamera, watendaji wao kazi kuazima kamera kwa waandishi kila uchao, lakini fedha zinatumika kumpeleka Kasongo kwenye Kombe la Dunia.

Pamoja na mambo mengine, Karia anaiminya na kuiweka mfukoni Bodi ya Ligi.

Ni ajabu sana kwa sababu ni bodi hii ndiyo iliyomleta Karia kwenye soka la kitaifa.

Aliingia TFF kama mjumbe wa Mkutano Mkuu kuiwajilisha Coastal Union kwenye Uchaguzi Mkuu wa TFF wa 2005 uliomuingiza Leodegar Tenga madarakani.

Baada ya Mkutano Mkuu wa Bagamoyo 2007 uliokuja na maagizo ya Club Licensing, baadaye zikaja harakati na chombo huru cha kusimamia ligi, ndipo ilipoanza Kamati ya Ligi ambayo mwenyekiti wake akawa Karia.

Kwa hiyo yeye anaijua sana Bodi ya Ligi na ilitakiwa aisaidie ijitegemee huku TFF ikibaki kuwa mwanahisa wake.

Lakini hataki, ameichukua na kuiweka mfukoni kiasi kwamba watendaji wa bodi wanamuona Karia kama mmiliki.

Na kwa hizi bakshishi za kuwasafirisha watendaji wa bodi, ndiyo kabisa anawaziba mdomo...wataendelea kuwa watumwa wake maisha yote. Kasongo anafanya nini India?

Columnist: Mwanaspoti