Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Jina la Manyara Stars limeshaachwa?

Manyara Stars Jina la Manyara Stars limeshaachwa?

Thu, 29 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Timu za Taifa za Soka za Tanzania zimekuwa kwenye harakati mbalimbali ndani ya mwezi huu wa Septemba.

Serengeti Boys, Timu ya Taifa Chini ya Miaka 17, iko kambini Karatu ikijiandaa na Mashindano ya CECAFA yatakayofanyika Ethiopia.

Serengeti Girls, chini ya miaka 17 - wanawake, iko Southampton England kwenye kambi ikijiandaa na Kombe la Dunia litakalofanyika India.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, iko Libya ilicheza mechi za kirafiki. Akaunti rasmi ya Instagram ya Shirikisho la Soka hapa nchini, @tanfoot, iko ‘bize’ sana kutoa taarifa ya maendeleo ya timu hizi huku ikitumia majina yao ya utani ambayo yamezoeleka sana.

Lakini kuna timu nyingine ya taifa ambayo pia iko kwenye harakati ila jina lake halitumiki au halitajwi kabisa.

Timu hiyo ni ile ya chini ya miaka 23 ambayo pia ilikuwa kwenye harakati za kufuzu AFCON yao ya 2023. Jina lake ni MANYARA STARS, lakini kila inapotajwa, jina la Manyara Stars haliguswi...utasikia tu, ‘Timu ya Taifa Chini ya Miaka 23’, basi.

Siyo ofisa habari wa TFF, siyo akaunti rasmi za mitandao ya jamii za TFF wala siyo viongozi wa TFF wanaolitaja jina hilo.

Mtu unajiuliza, hivi TFF wamelifuta hilo jina? Maana nchi hii ngumu sana. Kila utawala ukiingia madarakani unakuja na mambo yake.

Jamali Malinzi alianzisha tuzo kwa ajili ya wachezaji bora chipukizi na zikapewa jina la Ismail, yule kijana wa Mbao FC aliyeanguka na kufariki akiwa uwanjani kule Kagera kwenye ligi ya vijana.

Lakini tangu Malinzi aondoke madarakani, jina la hiyo tuzo halijawahi kutajwa tena. Utasikia tu, tuzo ya mchezaji bora chipukizi.

Mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo kwa jina hilo alikuwa Shaaban Idd Chilunda. Wengine wote waliofuata hawakushinda tuzo hiyo kwa jina la Ismail.

Kwa hiyo inawezekana na jina la Manyara Stars limekutana na ajali hiyo hiyo.

Bahati mbaya zaidi hata vyombo vya habari, hakuna hata kimoja kinacholitaja jina la Manyara Stars, pale panapokuwa na ripoti inayoihusu hiyo timu.

Idara ya habari ya TFF kazi yake ni kuhakikisha taarifa za shirikisho hilo zinaripotiwa kwa usahihi wake ili kuepusha mikanganyiko.

Ina maana nao hawajui kama timu hii inaitwa Manyara Stars?

Timu hii ilianzishwa mwaka 1967 ili ishiriki harakati za kufuzu Olimpiki za mwaka 1968.

Na kwa miaka yote, timu hii ilikuwa ikishiriki harakati za kufuzu olimpiki tu.

Kwa hiyo, Tanzania ilikuwa na timu mbili tu za taifa; ile ya wakubwa yaani Taifa Stars, na hii ya chini ya miaka 23.

Timu za taifa zikaongezeka baada ya FIFA na CAF kuanzisha mashindano ya vijana katika umri tofauti.

Mwaka 1977 FIFA ilianzisha Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 20 na kutaka mabara yote yashiriki kupitia hatua za kufuzu kwenye bara husika.

Mwaka 1979 Shirikisho la soka Afrika, CAF, likaanzisha mashindano ya vijana chini ya miaka 20 ambayo pia yalitumika kama mchujo wa Kombe la Dunia.

Tanzania ilianza kushiriki mashindano haya mwaka 1981 kwa kuunda timu ya kwanza ya vijana chini ya miaka 20 mwaka 1980.

Timu hiyo ambayo iliitwa Vijana Stars, ilikuwa na nyota kama akina Zamoyoni Mogella, Jamhuri Kihwelo, Ahmed Amasha na wengine wengi na baada tu ya kuundwa ikaenda Norway kuweka kambi ya muda.

Mwaka 1985 FIFA ikaanzisha mashindano mengine ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 16.

Mwaka 1991 mashindano haya yakabadilishwa na kuwa chini ya miaka 17. Afrika ilianza kwa kushiriki mchujo tu wa Kombe la Dunia lakini mwaka 1995 CAF ikaanzisha mashindano yake ya vijana chini ya miaka 17.

Tanzania ilithibitisha kushiriki lakini ikashindwa kuunda timu na hatimaye kujitoa kabisa.

Tanzania iliendelea kushindwa kuunda timu hadi mwaka 2000 ndipo timu ya kwanza ya vijana chini ya miaka 17 ikaundwa.

Timu hii ilikuwa na akina Steven Mapunda Garrincha na Munyu Kassim.

Huyu Munyu Kassim alikuwa beki wa kushoto wa Tanzania Prisons ya Mbeya.

Mchezaji huyu baadaye alijitoa kwenye timu ya taifa baada ya kukerwa na maneno ya Steven Mapunda ambaye alikuwa anasema Munyu kazidi umri.

Ikashiriki kufuzu AFCON U17 ya 2001 na kuanza vizuri kwa ushindi mnono wa jumla wa mabao 6-2 dhidi ya Swaziland.

Lakini ikatolewa raundi iliyofuata na Burundi kwa jumla ya mabao 2-0.

Timu hii ilikuja kupata umaarufu baada ya kufuzu AFCON U17 ya 2005 lakini baadaye ikabainika kwamba kuna wachezaji walivuka umri, ikaondolewa kwenye mashindano.

Timu hiyo ikavunjwa na timu mpya ikaanza kuundwa ikiwa na wachezaji kama akina Erasto Nyoni.

Hadi hapo kukawa na timu nne za taifa; ya wakubwa, ya chini ya miaka 23, chini ya miaka 20 na chini ya miaka 17.

Timu ya wakubwa tayari ilikuwa na jina lake la Taifa Stars tangu mwaka 1973.

Lakini hizi zingine zilikuwa zinatumia tu majina ya umri wao.

Ndipo ikaja hoja ya kutoa majina kwa kila timu ili iwe rahisi kuzitofautisha lakini pia kupunguza urefu wa jina kwa mtamkaji.

Ikaja hoja ya kutumia majina ya hizi timu kutangaza utalii wa nchi yetu.

Chini ya miaka 23 ikaitwa MANYARA STARS.

Chini ya miaka 20 ikaitwa NGORONGORO HEROES.

Chini ya miaka 17 ikaitwa SERENGETI BOYS.

Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes, zimekuwa zikishiriki mashindano mara kwa mara kwa sababu mashindano yake yapo kila baada ya miaka miwili.

Lakini Manyara Stars huitwa kila baada ya miaka minne kwa sababu mashindano yake hufanyika kila baada ya kipindi hicho.

Kama ilivyoelezwa huko juu kwamba timu hii ilianza rasmi mwaka 1967 kwa ajili ya kufuzu Olimpiki.

Lakini mwaka 2011 CAF ikaanzisha mashindano ya AFCON U23 kama sehemu ya mchujo wa kufuzu Olimpiki ya 2012.

Ikiwa chini ya Kocha Jamhuri Kihwelo Julio, Manyara Stars ikaitoa Cameroon na kukaribia kufuzu fainali za AFCON U23 za 2011.

Lakini bahati ikakutana na Nigeria kwenye hatua ya mwisho ya mchujo na kutolewa.

Timu hii iliundwa na nahodha Shaaban Kado, walikuwepo akina Thomas Ulimwengu, Kigi Makasy na Mbwana Samatta.

Na huo ndiyo mwaka ambao Mbwana Samatta alicheza mechi mbili za timu ya taifa katika nchi mbili tofauti.

Alianzia Dar Es Salaam Tanzania akiitumikia Taifa Stars dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, na baada ya mechi akapanda ndege, yeye na Shaaban Kado, kwenda Cameroon kucheza siku iliyofuata akiwa na Manyara Stars.

Bahati mbaya TFF chini ya Rais Malinzi ilishindwa kuipeleka timu hii kushiriki mchujo wa AFCON U23 ya 2015 na Olimpiki ya 2016 London.

Kwa hiyo Manyara Stars ambayo ilitakiwa kuitwa tena mwaka 2014, haikuitwa kabisa.

Ikaja kuitwa mwaka 2018 kwa ajili ya AFCON U23 ya 2019 chini ya utawala wa Rais Wallace Karia.

Timu hii ilikuwa chini ya Kocha Bakary Shime na aliita wachezaji kama Kelvin Kongwe Sabato, Habib Kyombo na Salum Kihimbwa.

Ikatolewa na Burundi kwa sheria ya bao la ugenini.

Ilipoteza 2-0 ugenini na kuongoza 3-0 nyumbani kabla Burundi hawajapata bao la dakika za mwisho. Safari hiii timu iko chini ya Kocha Hemed Suleiman Morocco.

Lakini hakuna hata sehemu jina hili la Manyara Stars linatajwa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz