Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Gubu la wakongwe Al Ahly na anguko la klabu yao

Al Ahly Pic Gubu la wakongwe Al Ahly na anguko la klabu yao

Wed, 3 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Maisha baada ya kuondoka kwa Kocha Pitso Mosimane, hayajawa mazuri kwa klabu ya Al Ahly ya Misri.

Usiku ambao Tanzania ulitawaliwa na Mandonga, kwa Misri ulitawaliwa na habari kubwa ya Al Ahly kutoshiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Hii ni baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Arab Contractors, katika mchezo wake wa 26 wa ligi, huku ikibaki na michezo minne lakini alama nane nyuma ya vinara Zamalek, na alama nne nyuma ya timu inayoshika nafasi ya pili, Pyramids.

Sare dhidi ya Arab Contractors ni mwendelezo wa matokeo mabaya tangu kuondoka kwa kocha wake raia wa Afrika Kusini, Pitso Mosimane, Juni mwaka huu.

Katika michezo tisa tangu kuondoka kwa Pitso, michezo minne imetoka bila alama tatu ikifungwa au kutoka sare.

Kwenye msimamo wa ligi, Al Ahly iko nafasi ya tatu, ikiwa mchezo mmoja nyuma ya Pyramids lakini hata ikishinda haiwezi kuifikia.

Hii ina maana Al Ahly ili ifuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni lazima iiombee Pyramids ipoteze angalau mchezo mmoja katika saba iliyobaki na yenyewe ishinde yote.

Kwenye mpira chochote kinawezekana lakini kwa mwenendo klabu hizi mbili kwa sasa hilo ni aghalabu kutokea.

MAGWIJI NA GUBU

Al Ahly ilikuwa na maisha mazuri uwanjani wakati wa utawala wa Pitso Mosimane .

Lakini haikuwa na maisha mazuri nje ya uwanja kutokana na ukosoaji wa magwiji wa klabu hiyo iliyojaa siasa kupita kawaida.

Ilikuwa ishinde au isishinde, lazima ataibuka mkongwe mmoja aliyewahi kucheza kwa mafanikio na mwenye wafuasi wengi miongoni mwa mashabiki, na kukosoa kitu kuhusu Pitso.

Atasema maneno mengi kisha atahitimisha kwa kusema, “Pitso hatoshi kuifundisha Al Ahly.”

Wakati Pitso alipokwenda Al Ahly aliikuta ikiwa kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akashinda mechi hizo hadi ubingwa wa Afrika. Wakongwe wakaibuka na kusema aliikuta timu iko nusu fainali, hivyo makocha waliotangulia walifanya kazi kubwa ambayo yeye alimalizia tu.

Timu ikaenda klabu bingwa ya dunia na kushika nafasi ya tatu, jambo ambalo haikuwahi kulifanya hapo kabla.

Lakini wakongwe wakakosoa kwa kitendo cha Al Ahly kupaki basi kwenye nusu fainali dhidi ya Bayern Munich. Yaani walitaka Al Ahly iwapelekee moto Bayern Munich, mwanzo mwisho.

Msimu mpya ukaanza na Pitso akaiongoza Al Ahly kushinda ubingwa wa Afrika, lakini akapoteza ubingwa wa Ligi Kuu kwa wapinzani wao wakuu, Zamalek.

Akaiongoza Al Ahly kushinda taji la Super Cup la CAF na rais wa klabu ambaye ni mkongwe mkubwa zaidi kuliko hao wenye gubu akamuunga mkono Pitso na kumuahidi ushirikiano mkubwa huku akisema klabu haimdai chochote Pitso, bali yeye ndiye anaidai.

Lakini wakongwe wenye gubu wakaibuka tena kumkosoa Pitso kwamba anapotezaje ubingwa wa Ligi Kuu.

Msimu huu unaoendelea ulikuwa wa tatu kwa Pitso na aliifikisha timu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakapoteza dhidi ya wenyeji Wydad Casablanca na hapo gubu la wakongwe likazidi.

Wakamuandama na kuweka ushawishi hadi kwenye bodi ya klabu kiasi cha kuitisha mkutano wa dharura wa kumjadili Pitso.

Baada ya mkutano wakakubaliana kwamba aendelee kama kocha mkuu kwa sababu wamegundua anawafaa zaidi kuliko anavyolaumiwa.

Lakini yeye mwenyewe akaona inatosha. Ni vigumu sana kuliendesha gari ambalo kila abiria anakukosoa.

Ukipiga honi anaibuka mmoja anasema umepiga honi kubwa sana. Mwingine anasema hakukuwa na haja ya kupiga honi.

Ukibana breki anaibuka abiria mwingine anasema umewashtua kwa breki yako, mwingine anasema usingebana breki bali ungekwepa.

Sasa maisha bila Pitso ndiyo yamekuwa magumu zaidi kwa Al Ahly na wale wakongwe wenye gubu kama la mawifi kwa mke wa kaka yao wako kimya.

Kutoka fainali tatu mfululizo za Ligi ya Mabingwa hadi kutofuzu kabisa...unadhani itakuwaje?

Baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Zamalek kwenye fainali ya Kombe la FA, mashabiki wa Al Ahly walipaza sauti kumlilia Pitso.

Wapo waliojilaumu kwa kutompigania vya kutosha wakati wa gubu la wakongwe na wengine wakiwataka wakongwe wapaze sauti kwa kocha wa sasa kama walivyofanya kwa Pitso.

Mwisho wa yote, wakongwe wa Al Ahly wamesababisha anguko la klabu yao kwa kujua au kutojua...kwa kutumika au kutotumika.

Bila shaka hili litakuwa somo kubwa kwao kwa makocha wanaofuata. Kocha anapaswa kuungwa mkono na kila mmoja klabuni kwa maslahi mapana ya klabu.

Kukosoana kupo, hasa pale mambo yanapokuwa hayaendi vizuri.

Lakini siyo kila siku tunakosoana, mambo yanapoenda sawa au mrama.

Haijulikani tatizo ni matokeo au nafasi. Wakongwe walivuja jasho kuisimamisha klabu wakati wa uchezaji wao, lakini sasa wanavuja jasho kuiangusha klabu yao.

Hatari sana!

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz