Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Bocco alilia, tusubiri kumuona Sure Boy

Sure Boy Salum Abubakary ’Sure Boy’

Wed, 6 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Septemba 7, 2017 John Rafael Bocco alicheza mechi yake ya kwanza ya mashindano akiwa na klabu yake mpya, Simba SC. Mechi hiyo ilikuwa dhidi ya Azam FC dimbani Azam Complex - ulikuwa mchezo wa raundi ya pili katika msimu mpya wa 2017/18.

Wakati akigusa nyasi za uwanja kutoka vyumba vya kuvalia, John Bocco alitokwa na machozi kutokana na hisia kali zilizomjia kwa kukutana na Azam FC. Bocco aliondoka Azam FC baada ya msimu wa 2016/17 kama sehemu ya mipango ya mtendaji mkuu mpya wa klabu hiyo, Abdul Mohamed.

Akichukia nafasi ya Saad Kawemba kama mtendaji mkuu, Abdul Mohamed alikuja na wazo la kuisafisha Azam FC kwa kuwaondoa wachezaji wote wakongwe waliodumu na timu kwa muda mrefu akiamini ndiyo wanaoikwamisha.

Ndipo Bocco na wenzake watatu Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe safari ilipowakuta. Panga lilianza na hawa kwa sababu mikataba yao ilikuwa inaelekea kwisha mwishoni mwa msimu huo.

Baada ya hawa, walikuwa wanafuata kina Aggrey Morris na Salum Abubakary’Sure Boy’ ambao mikataba yao ilikuwa inaisha msimu wa mbele yake. Bahati mbaya sana ni kwamba wachezaji hawa hawakuambiwa ukweli kuhusu hatima yao, badala yake walidanganywa kwamba kampuni imeyumba kiuchumi hivyo imepunguza bajeti kwenye timu.

Wakapewa mikataba yenye maslahi yaliyopunguzwa sana imani ikiwa watakataa, hivyo kuachana na klabu. Na kweli, wengine wote walikataa kasoro John Bocco. Yeye alikubali kupokea chochote ambacho klabu itamuwekea mezani.

Utayari huu wa Bocco uliwachanganya sana wanafanya uamuzi wa klabu ikiwemo bodi ya wakurugenzi.

Katika wakurugenzi watatu wa klabu hiyo, mmoja alikuwa tayari Bocco asaini, mmoja akawa hataki na mwingine alikuwa anasubiri uamuzi wa mmoja katika wale wawili - yule aliyekataa, akaungana naye. Kazi ikawa kumueleza Bocco kwamba hatakiwi klabuni hivyo aondoke.

Waliopewa majukunu hayo ni watu ambao Bocco alicheza nao hapo klabuni na waliheshimiana sana. Wakashindwa kumueleza. Wakaanza kumzungusha hadi yeye mwenyewe alipobaini kwamba hatakiwi tena na kuchukua uamuzi mgumu.

Katika maisha yake klabuni hapo, Bocco hakuwahi kuwaza kwamba kuna siku angeondoka kwa sababu aliamini angestaafia hapo hapo na kugeukia ukocha. Hiyo ni ndoto ambayo alikuwa nayo yeye na Sure Boy.

Kwa hiyo kuondoka kwake kulimuuma sana na alipokutana na timu hiyo siku ya kwanza alishindwa kuzuia hisia zake, akalia kwa uchungu. Lakini sasa ameshazoea maisha ya Simba na anasonga mbele.

Miaka mingi baadaye, yule swahiba wake ambaye alikuwa na ndoto moja naye ya siku moja kuwa kocha wa Azam FC, naye ameondoka.

Aprili 6, 2022 atarudi kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Azam Complex, vipi naye atalia?

John Bocco na Salum Abubakary walisajiliwa na Azam FC mwaka mmoja, 2007. Abubakary alianza kusajiliwa na baadaye Bocco akafuata kwenye usajili uliofanyika nje ya dirisha.

Mkasa wake utakuja katika toleo jingine huko mbele. Wakaisaidia Azam FC kupanda ligi kuu na baadaye kuupa ubingwa wa ligi. Lakini baada ya hali ya hewa kuchafuka na Bocco kuondoka, Sure boy hakuwa na furaha.

Maisha yake yakawa magumu hasa baada ya kubaini kwamba kumbe mpango ulikuwa kuwaondoa, akiwemo yeye. Na ndiyo maana mara kadhaa alijaribu kuomba kuondoka klabuni hapo hadi alipofanikiwa msimu huu. Je, atalia? Tusubiri tuone Aprili 6, 2022.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz