Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Badru anahukumiwa na kitu kimoja, kufanya kazi Azam

Mohamed Badru Mohamed Badru

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 17 ya Azam FC, Mohamed Badru, ameiongoza timu yake kushinda ubingwa wa ligi kuu kwa staili ya hali ya juu sana. Katika mechi 12 za msimu mzima, timu ya Badru imeshinda mechi 11 na kutoka sare mchezo mmoja tu.

Imefunga mabao 39 na kufungwa mabao 5 tu. Imevuna alama 34 kati ya 36 ambazo zingeweza kupatikana. Timu yake imetoa mfungaji bora imetoa kipa bora na imetoa mchezaji bora wa mashindano.

Lakini yeye amekosa tuzo ya kocha bora. Ajabu sana! Tuzo hiyo imeangukia kwa kocha wa vijana wa Simba SC, Nico Kiondo. Bila kumkosea heshima Kiondo, lakini hakuna namna yoyote ambayo TFF wanaweza kutoa utetezi kwa Kiondo kuwa kocha bora msimu huu, mbele ya Badru.

Timu yake imecheza mechi 12 na kushinda tano. Imetoa sare mechi sita na kufungwa moja na hiyo moja yenyewe ni dhidi ya timu ya Badru.

Timu ya Kiondo imezidiwa alama 13 na timu ya Badru, lakini bado TFF wanasema Kiondo ni bora kuliko Badru. Taarifa za chini zinasema eti vyeti vya ukocha vya Badru siyo sahihi kwa Tanzania.

Inakuwaje vyeti siyo sahihi na vikaleta matokeo ya namna hii? Hatujiulizi kwamba labda Sisi ndiyo hatuko sahihi kuvikataa vyeti vya namba hiyo? Na je tunatoa tuzo kwa cheti kwa kocha? Sawa, labda vyeti vya Kiondo ni bora kuliko vyeti vya Badru...lakini Kiondo mwenyewe kama kocha mbele ya Badru kama kocha?

Hiyo siyo sababu ya msingi kwa kuwa Badru ameshiriki mashindano tangu mwanzo na mamlaka hizi hizi za mpira wetu zimemuona. Kama hakuwa na sifa, wangechukua hatua kumtoa kwenye benchi ili wanaostahili waendelee kuliko kufanyauamuzi kama huu ambao unaunajisi mpira wetu.

GHARAMA ZA KUVAA AZAM FC

Badru anahukumiwa na kitu kimoja tu, kufanya kazi Azam FC. Katika mpira wa Tanzania, kufanya kazi Azam FC kuna gharama kubwa sana ya kulipa mbele ya mamlaka na hata umma wa mashabiki. Mkasa wa Badru ni muendelezo wa gharama za wanazolipa wanaovaa nembo ya Azam FC kwa miaka na mikaka. Wakati John Bocco yuko Azam FC, alikuwa bora sana lakini hakuwahi kushinda tuzo hata mara moja.

Ni hadi alipohamia Simba na ndipo alipoanza kushinda tuzo, lakini kiufundi ubora wake ulipungua kwa kulinganisha na ule alikokuwa nao akiwa Azam FC. John Bocco wa msimu wa 2011/12 ambaye alifunga mabao 18 katika ligi yenye mechi 22 msimu mzima, hakuwa wa kawaida hata kidogo.

Msimu wa 2020/21 hakukuwa na mchezaji hata mmoja wa Azam FC kwenye fainali za tuzo, ilhali Idd Suleiman Nado alistahili kabisa angalau kuingia fainali kama kiungo bora mbele ya Feisal Salum na Mukoko Tonombe. Prince Dube alistahili angalau kuingia fainali ya mchezaji bora wa msimu kwa kiwango chake, lakini hakuna aliyemfikiria.

Msimu uliopita wa 2021/22, tuzo ya mchezaji bora wa mwezi kwa mwezi wa mwisho wa msimu, yaani mwezi Juni ilipaswa kwenda kwa mchezaji wa Azam FC Idris Ilunga Mbombo. Ndani ya mwezi huo mwamba alicheza mechi zote nne za timu yake na kufunga mabao tisa akifunga kila mchezo ikiwemo hat trick katika mchezo wa mwisho. Unataka kiwango gani ndani ya mwezi ili mtu astahili kushinda?

Ofisa habari wa Azam FC, Zaka Zakazi alipewa onyo kali na Kamati ya Maadili ya TFF kwa kuwatuhumu Yanga kufanya ushirikina. Kimsingi kanuni za TFF zinakataza ushirikina na alichokifanya Zaka ni kukemea vitendo vya kishirikina ambavyo Yanga walivifanya dhidi ya Azam FC kwenye Kombe la Mapinduzi 2021.

Kamati inatoka na onyo kwa Zaka, badala ya kumuita na kumtaka athubitishe pasi na shaka kama sheria zinavyotaka. Lakini msimu uliopita, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally naye aliwashutumu Yanga kwa kufanya ushirikina dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Mkapa.

Kamati ikakaa kimya kama hakuna kilichotokea..kosa alifanye wa Azam FC akiwafanya mwingine siyo kosa. Tuzo ya kocha bora wa Machi 2019 ni moja ya gharama ambazo wavaa nembo ya Azam FC wamekuwa wakilipa kwenye mpira wa Tanzania.

Kocha wa Azam FC, Meja mstaafu Abdul Mingane aliiongoza Azam FC kushinda mechi zote tatu za mwezi huo kwa staili ya aina yake. Africa Lyon 1-3 Azam; Azam 6-1 JKT Tanzania na Azam 4-0 Singida United.

Timu yake ilifunga mabao 13 katika mechi hizo tatu ikiruhusu mawili. Lakini kocha bora akawa Patrick Aussems wa Simba ambaye licha ya kushinda pia mechi zake zote za mwezi huo, lakini matokeo yake hayakuwa makubwa kama ya Mingange. Aliishinda Stand United 0-2 Simba; Simba 2-0 Ruvu Shooting na Simba 3-0 Mbao FC.

Ni vigumu kwa Azam FC kutoboa mbele ya Yanga na Simba kwa usimamizi huu wa upendeleo wa mamlaka za mpira wetu.

Uamuzi ambao mamlaka zinaufanya dhidi ya Azam FC kwa miaka mingi unaikandamiza klabu hiyo, lakini hakuna anayejali kwa sababu hayupo wa kuipigia kelele mitaani.

Sakata la kufungiwa Haji Manara wa Yanga linapigiwa kelele hadi na viongozi wa dini achilia mbali wanasiasa. Sasa pata picha hapo Manara ana hatia, vipi angekuwa anaonewa?

Na hali hii pia hutokea pale Simba wanapokutana na mkono wa sheria. Sasa Azam FC inakosa hao viongozi wa dini wa kuipiga presha mamlaka. Hao wanasiasa wa kuishinikiza mamlaka. Anayevaa nembo ya Azam FC ataonewa, atanyanyaswa, lakini hakuna atakayepaza sauti.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz