Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MUBIRU: Kocha wa mataji anayezitaka Simba, Yanga

Mubiru Pic MUBIRU: Kocha wa mataji anayezitaka Simba, Yanga

Fri, 18 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Pamoja na kutozungumzwa sana, lakini Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mubiru Abdallah ni miongoni mwa makocha wenye uwezo na ubora katika kufundisha soka kwa mbinu zenye manufaa.

Kocha huyo raia wa Uganda alijiunga na Mbeya City mwanzoni mwa msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya huku akiwa amepitia klabu mbalimbali za nyumbani kwao.

Miongoni mwa timu alizofundisha na kuzipa mafanikio ni Police FC na Vippers lakini akizinoa pia Timu za Taifa ‘The Cranes’ na zile za vijana (U17 na 23) huku akizisaidia kufuzu michuano mbalimbali.

Miongoni mwa mafanikio anayojivunia ni kuivusha The Cranes kufuzu kwa Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) 2020, Cocafa kwa timu ya Wanawake.

Pia, aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Uganda KCCA na Kombe la Mapinduzi mwaka 2014 na taji la Michuano ya Eapco Police FC akieleza kuwa alistaafu kifahari na hadi sasa anajivunia makubwa kwenye kazi ya ukocha.

Lakini pia anaeleza katika zama zake akisakata kabumbu amefanya makubwa ikiwa ni kutwaa mataji mbalimbali ya Ligi Kuu Uganda akiwa na timu za SC Villa na Police FC.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti nyumbani kwake Mitaa ya Isyesye jijini Mbeya, kocha huyo ameeleza mengi ikiwamo ndoto zake za kuzinoa Simba na Yanga.

AZITAMANI SIMBA, YANGA

Kocha huyo anasema licha ya kuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi Tanzania, lakini ni wazi hakuna asiyependa kufanya kazi na Simba na Yanga na hata yeye yuko tayari kuungana na miamba hiyo.

Anasema wakati akicheza soka miaka hiyo, licha ya kukutana na timu hizo katika mashindano mbalimbali ikiwamo Kombe la Mapinduzi, lakini hakuwahi kupata ofa kutoka kwa timu yoyote.

Hata hivyo, anabainisha kuwa kwa kipindi hicho, hakufahamu kama ingewezekana mchezaji kutoka Uganda kucheza Tanzania japokuwa baadaye alielewa baada ya Simba kumpa kazi, Jackson Mayanja.

“Simba na Yanga hakuna asiyezijua hapa Afrika na kwa sasa wachezaji au makocha wanapenda kufanya kazi na timu hizo na hata mimi ikija ofa tunafanya kazi pamoja,” anasema kocha huyo.

UGANDA NA TANZANIA

Kocha huyo asiye na maneno mengi, anasema mataifa yote yana soka safi na la ushindani, isipokuwa utofauti ni kuwa Uganda kuna vipaji vingi, huku Tanzania ikichagizwa na mapenzi kwa mashabiki.

Anasema kama haitoshi, viongozi, wadau na mashabiki wa soka Tanzania wanaheshimu sana makocha tofauti na Uganda jambo ambalo linawafanya makocha wengi kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kama soka la ushindani mataifa yote yanafanana, japokuwa Tanzania kuna mapenzi kwa mashabiki, lakini heshima kwa wachezaji na makocha, Uganda hawako hivyo,” anasema kocha huyo.

Hata hivyo kocha huyo anaweka wazi kuwa haoni sababu ya kuondoka mapema Tanzania labda itokee Mungu kuamua, lakini vinginevyo hatarajii kufanya hivyo.

ISHU YA MKATABA

Kocha huyo anaanza kwa kushangaa kilichomtokea baada ya kucheleweshewa mkataba na mabosi wake kwa zaidi ya mwezi mmoja bila kumalizana naye akibainisha kuwa aligundua changamoto yao.

Kutokana na uzoefu alionao kwenye soka aliona kuna ‘mentality’ ya baadhi ya viongozi kutoelewa ukubwa wa timu wakidhani Mbeya City ni klabu ndogo.

Anasema pamoja na yote hayo, aliamua kutokata tamaa bali kusubiri muda kuonesha uwezo wake katika kufundisha soka na kwamba hiki kinachoonekana ni mwanzo tu.

“Kwa hiyo nikahisi kuna ile dhana ya kwamba Mbeya City ni timu ndogo bila kujua chochote kikubwa huanzia chini hivyo nikaamua kunyamaza ili niwaoneshe kwa vitendo kazini,” anasema Abdallah.

AUTAKA UBINGWA

Ni wazi Mbeya City imekuwa na matokeo mazuri msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita chini ya Lule, ilipomaliza nafasi ya nane huku ikiweka rekodi ya kibabe ya kutofungwa na timu za Simba, Yanga na Azam huku ikichukua pointi nane kwa vigogo hao.

Hata hivyo, hadi msimu huu City imeonesha ushindani katika mechi tisa ilizocheza hadi sasa imekusanya pointi 15 na kukaa nafasi ya tano huku ikicheza kwa muunganiko, ari na morari.

Kocha huyo anasema baada ya kujiunga na timu hiyo alikaa na wachezaji akiwataka kujitambua lakini kuthamini kazi yao na kupambania timu kwanza ili kuipa thamani.

“Ni mapenzi ya Mungu nilikaa na wachezaji nikawaambia siri ya kufanikiwa kwa mchezaji ni kujituma na kuthamini kile anachokifanya, zaidi ni nidhamu na thamani kwa timu,” anasema.

Anaeleza kuwa hadi sasa anafurahia kiwango cha wachezaji, japokuwa bado hawajafikia pale anapotaka, akibainisha anahitaji kuona Mbeya City inatwaa ubingwa na lolote linawezekana.

“Kama tutashindwa ubingwa, basi tusikose nafasi nne za juu, timu yangu ni bora na wachezaji wana uwezo kupambania tunachotaka, kimsingi ni kujiamini na wadau kuisapoti,” anasema kocha huyo. Kuhusu rekodi ya msimu uliopita kutofungwa na Simba, Yanga au Azam

“Mimi siangalii yaliyopita au kujipanga na timu moja isipokuwa kila mechi kwetu tunataka pointi tatu,” anasema

LULE AMVUTA MBEYA CITY

Abdallah anakiri wazi kuwa hakuwa na ofa yoyote hapa Tanzania japokuwa wapo baadhi ya watu wake wa karibu walimuunganisha na Dodoma Jiji, lakini alikataa kutokana na nafasi waliyokuwapo.

Anasema ndugu na rafiki yake aliyekuwa akiinoa Mbeya City msimu uliopita, Mathias Lule (kwa sasa Singida Big Stars) ndiye alimshawishi kujiunga na timu hiyo akimpa uhalisia wa soka la Tanzania.

“Kwa hiyo baada ya kuitazama Dodoma Jiji nikaona ipo kwenye wakati wa kushuka daraja nikaachana nao, ndio Lule akaniambia nije Mbeya City ambayo ilikuwa nafasi nzuri.”

“Kabla ya hapo sikuwa na ofa yoyote kwa timu za hapa Tanzania kwahiyo nilisubiri msimu ukaisha nikaja kuungana na Mbeya City ambao niko nao hadi sasa,” anasema.

KUHUSU KOFIA

Mara kadhaa wadau na mashabiki wamekuwa na minong’ono pale wanapomuona kocha huyo kwenye mechi amevalia kofia wakihisi pengine ndio siri ya mafanikio.

Akielezea kilichopo kwenye kofia yake hiyo uwanjani, anafafanua kuwa hiyo ni Imani yake na asili kwani yeye ni mpenzi wa dini ya kiislamu na amekuwa akiivaa muda wowote na sehemu yoyote.

“Kwanza najivunia na uislamu wangu, lakini kuhamasisha na kushawishi waislamu wenzangu kuendelea kuipenda dini yao, kama kuna ambao wanadhani kuna ushirikina wanapotoka,” anasema.

NJE YA SOKA

Unaambiwa kocha huyo ni paparazi mzuri sana kwani baada ya kumaliza elimu ya ukocha na kujipatia cheti cha leseni A ya shirikisho la soka Afrika (CAF) aliingia darasani kusomea uandishi wa habari.

Kocha huyo anasema kwa sasa anayo stashahada (Diploma) ya Habari na mawasiliano na anaweza kufanya kazi popote kwa misingi yote ya habari na ni kazi ambayo anaikubali sana.

“Mimi ni mwandishi wa habari kitaaluma nje ya ukocha, nina diploma yangu na ni kazi ambayo naipenda na nikipata sehemu naweza kuingia kazini nikafanya wanavyotaka kulingana na misingi,” anasema.

CHAKULA, HALI YA HEWA

Kocha huyo anasema alipotua hapa nchini alikutana na hali ya hewa ya baridi ambayo ilimpa wakati mgumu, lakini kwa sasa anaona hali inabadilika na anazoea tofauti na mwanzo.

Kuhusu vyakula anasema yeye ni mpenzi sana wa ndizi, wali, ugali, viazi, mihogo, viazi na chipsi japokuwa tatizo ni mapishi hapa Tanzania tofauti na nyumbani tunavyoandaa.

“Hali ya hewa kwa sasa ni kawaida sawa na Uganda na vyakula nipendavyo vipo ishu ni mapishi na maandalizi yake, lakini kwa ujumla nafurahia maisha ya Tanzania na kuondoka si leo au kesho labda Mungu aamue,”anasema.

ALIANZAJE SOKA

Kiungo huyo mshambuliaji wa zamani, anasema yeye mpira ulikuwa kwenye damu kwani tangu akiwa elimu ya msingi hadi chuo alifanya makubwa na kila alipokwenda walikubali kipaji chake.

Anasema hata akiwa kijijini kwao, Chibhuli nchini Uganda alikuwa akiwapa raha mashabiki kwani kama siyo kufunga mabao, basi aliweza kusaidia kutengeneza mabao kwa wengine.

Miongoni mwa mashindano anayotaja kufanya kweli ni pamoja na yale ya mashule (Schools competition), Cocacola, mashindano ya makampuni na ile ya mabingwa wa shule (Schools Championship) na ile ya makabila nikicheza Mamba clan.

“Timu yangu ya kwanza kucheza kiushindani ilikuwa Uganda Cement Industry) kisha kujiunga na Village FC na baadaye Kagoma japokuwa nasahau ilikuwa mwaka gani,”anasema

“Mwaka 2000 niliamua kutundika daruga na kuanza kusomea ukocha na sasa nashukuru nimekuwa na timu kadhaa kwa mafanikio kama makombe na kuzijenga kiushindani,” anasema Abdalah.

Columnist: Mwanaspoti