Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA PWANI: Yanga SC, Azam FC wana deni kubwa kimataifa

Aggrey Morris Yanga SC, Azam FC wana deni kubwa kimataifa

Sat, 9 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba kwa sasa wanasubiri kuumana na Orlando Pirates katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huu, wakianzia nyumbani.

Simba imejikuta ikiangukia kwa wababe hao hao wa Afrika Kusini baada ya kushika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D la mashindano hayo ikiwa imekusanya jumla ya pointi 10, nyuma ya RS Berkane ya Morocco ambayo nayo ina idadi kama hiyo ya pointi ila zimetofautishwa kwa matokeo katika mechi mbili baina yao.

Katika hatua hiyo ya robo fainali, Simba itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 17 na Aprili 24, Orlando Pirates itakuwa mwenyeji katika mechi ya marudiano itakayochezwa katika Uwanja wa Orlando jijini Johannesburg.

Kwa mujibu wa droo iliyochezeshwa Jumanne wiki hii, mshindi wa mechi baina ya Simba na Orlando Pirates ataumana na timu itakayopata matokeo mazuri baina ya Al Ittihad Tripoli na Al Ahli Tripoli za Libya.

Kitendo cha Simba kutinga hatua ya robo fainali kimeihakikishia Tanzania Bara uwakilishi wa klabu nne katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao, ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.

Tanzania imepata fursa hiyo kwa mara nyingine nafasi baada ya kufikisha jumla ya pointi 30.5 na kuzipiku Zambia na Nigeria ambazo awali zilikuwa juu yake pamoja na Libya ambayo nayo imepanda baada ya timu zake mbili, Al Ahli Tripoli na Al Ittihad kufanya vyema katika hatua ya makundi.

Kwa mujibu wa Caf, nchi 12 zinazoongoza chati ya viwango vya ufanisi katika mashindano ya klabu Afrika, kila moja inapata fursa ya kuwakilishwa na klabu nne katika mashindano hayo ambapo mbili hushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba kwa kutinga robo fainali, Tanzania imepata alama pointi mbili ambazo zinazidisha kwa tano kisha zinajumlishwa na pointi 20.5 ambazo zimekusanywa na timu za Tanzania katika misimu minne iliyopita ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu zinafafanua kwamba timu itakayotwaa ubingwa wa ligi na ile itakayomaliza katika nafasi ya pili zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na ile itakayotwaa taji la Kombe la Shirikisho la Azam na itakayomaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Ukitazama msimamo wa ligi na muelekeo wake ulivyo, ni wazi kwamba Yanga, Simba na Azam zina nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi tatu za juu na hivyo kuwa katika uwezekano mkubwa wa kushiriki mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.

Baada ya kupata nafasi hizo nne, jukumu kubwa lililobakia ni klabu hizo kuhakikisha inazilinda ili tuendelee kunufaika kwa kuwakilishwa na idadi kama hiyo kwa misimu mingi ijayo.

Namna ya kuzilinda ni kufanya vizuri katika mashindano husika hasa kwa kuingia angalau hatua ya makundi na kuendelea kwani hilo litapelekea kuongezeka kwa pointi za Tanzania katika mfumo wa ukokotoaji wa alama kwa nchi husika kulingana na ufanisi wa klabu zake katika mashindano ya klabu.

Na hapa klabu ambazo zinapaswa kuhakikisha hilo litimie ni Yanga na Azam kwani ndizo ambazo bado hazijatoa mchango mkubwa katika kuisaidia nchi kupata uwakilishi wa timu nne.

Yanga ingawa imechangia, pointi zake ni ndogo kwa vile mara mbili tofauti ilizotinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika, ilishika nafasi ya mwisho jambo lililofanya ipate pointi chache.

Azam FC yenyewe ndio haijawahi hata kuingia hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika na imezidiwa hata na Namungo FC ambayo msimu uliopita iliweza kufika hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Ieleweke kwamba Yanga na Azam ni miongoni mwa timu tatu kubwa ambazo zina nguvu kubwa kiuchumi hivyo ni lazima zipewe kipaumbele na watu kujenga matumaini makubwa nazo tofauti na timu nyingine ya nne kwani klabu nyingi tofauti na hizo hazina misuli ya kifedha ya kumudu mashindano ya kimataifa.

Tumechoka kuona tambo za hapa nchini na sasa ni wakati wa klabu hizo kudhihirisha ubabe wao katika mashindano ya kimataifa kama ambavyo Simba imejitahidi kufanya.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz