Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA PWANI: Klabu zisaidie muendelezo wa vijana Stars

Stars Taifa FT Kikosi cha Stars

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa muda kupisha mechi za timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Katika kipindi hiki cha kalenda ya mechi za kimataifa, timu ya taifa, Taifa Stars itacheza mechi tatu za kirafiki kwa malengo ya kujipima ngumu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na zile za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).

Pia mechi hizo tatu ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mechi hizo tatu ni dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, mchezo ambao ulichezwa juzi Jumatano, kisha mwingine utakuwa kesho dhidi ya Botswana na Jumanne itafunga kwa kukabiliana na timu ya taifa ya Sudan.

Uteuzi wa kundi kubwa la wachezaji wenye umri mdogo (vijana) katika kikosi hicho cha Stars kwa ajili ya mechi hizo tatu kulinganisha na wale wenye umri mkubwa kisoka ambao ni ule wa zaidi ya miaka 28.

Zaidi ya nusu ya wachezaji walioitwa katika kikosi hicho cha Stars chenye wachezaji 29 wana umri chini ya miaka 23 na wengine wasiopungua watano hawazidi umri wa miaka 25 na hao ni wachezaji wanaocheza katika nafasi tofauti tofauti uwanjani.

Vijana walioitwa kikosini ambao wapo chini ya umri wa miaka 23 ni Metacha Mnata, Abuutwalib Mshery, Israel mwenda, Haji Mnoga, Dickson Job, Lusajo Mwaikenda, Abdulrazack Hamza, Nickson Kibabage, Novatus Dismas, Aziz Andabwile, Kelvin John, Ben Starkie, Tepsi Evance, Kibu Denis na Ibrahim Joshua.

Kitendo cha kocha wa Stars, Kim Poulsen kuita kundi kubwa la wachezaji wenye umri mdogo ni ishara kwamba kocha huyo na benchi lake la ufundi wanaifikiria zaidi kesho ya timu hiyo.

Ingawa wengi kati ya vijana hao hawatopata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya Stars, uwepo wao katika kipindi hiki unasaidia kuwajengea uzoefu na ukomavu wa kucheza mechi za ushindi jambo litakalowafanya waimarike zaidi kiakili na kwa uwezo wa uwanjani.

Anachokifanya Poulsen sio kitu kigeni na ndio kimekuwa chachu ya mafanikio kwa mataifa mengi ambayo yamefanya vizuri katika mashindano ya soka ya timu za taifa kwani yamekuwa yakiwaandaa na kuwatumia wachezaji ambao wamepevuka mapema wakiwa katika umri mdogo.

Kina Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Erasto Nyoni, John Bocco, Simon Msuva, Aggrey Morris na wengineo ambao umri umeenda, ndani ya muda mfupi ujao watajiweka kando kuitumikia Stars na hata klabu zao kwa baadhi na nyakati tofauti.

Wanahitaji watu ambao wataziba nafasi zao kwa muda mrefu na hao hawawezi kuibuka tu kutoka pasipo julikana hadi kuichezea timu ya taifa na badala yake wanatakiwa kuandaliwa mapema kwa kipindi hiki cha sasa ambacho ni sahihi kwao kwani wapo katika umri wa kupokea kile wanachoelekezwa na kukifanyia kazi.

Kwa bahati nzuri wachezaji vijana wengi walioitwa kikosini wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri katika mechi za mashindano mbalimbali ambayo timu zao zimekuwa zikishiriki jambo ambalo linatia matumaini.

Na kama kwamba haitoshi, wapo wengine wenye umri mdogo ambao wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri katika mechi za timu zao japo hawajaitwa katika kikosi cha Stars kama vile Abdul Seleman ‘Sopu’, Rashid Chambo, Denis Nkane, Jimmyson Mwanuke na Deogratias Mafie.

Hata hivyo malengo hayo mazuri ya benchi la ufundi la Stars ili yafanikiwe yanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa klabu ambazo zinapaswa kuwapa nafasi ya kutosha ya kucheza wachezaji vijana katika vikosi vyao tofauti na hali ya sasa ambapo nyota wengi wa umri mdogo wamekuwa hawachezi mara kwa mara.

Wachezaji hao vijana wakichezeshwa mara kwa mara katika klabu zao, watapata uzoefu wa ushindani na itawajengea hali ya kujiamini sambamba na kuimarika kimbinu na kiufundi kinyume na wanapokaa nje kwa muda mrefu.

Mafanikio ya timu za taifa hayawezi kupatikana kama klabu ambazo ndizo zinamiliki wachezaji, hazioni umuhimu wa kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wenye umri mdogo.

Ni lazima kuwe na ushirikiano chanya kati ya timu za taifa na klabu ili kila upande uwe chachu ya mafanikio kwa mwingine.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz