Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA PWANI: Ghana, Cameroon ziipe hasira Simba Jumapili

Ghana Pic Data Ghana, Cameroon ziipe hasira Simba Jumapili

Sat, 2 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 yamefikia tamati juzi Jumanne ambapo timu tano za taifa zitakazopeperusha bendera ya Afrika katika fainali hizo zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 21 hadi Disemba 18 mwaka huu.

Timu hizo tano za Afrika ambazo zitapambana na mataifa mengine 27 huko Qatar kuwania taji hilo lenye thamani kubwa zaidi kisoka duniani ni Ghana, Cameroon, Senegal, Tunisia na Morocco ambazo zimefanya vizuri katika hatua ya mwisho ya mashindano ya kuwania kufuzu kwa kanda ya Afrika.

Morocco imekata tiketi yake baada ya kuitupa nje DR Congo, Ghana imeitoa, Nigeria, Tunisia ikiinyima fursa Mali, Senegal ikiizuia Misri wakati Cameroon yenyewe imekata tiketi ya kwenda Qatar baada ya kuitoa Algeria.

Kati ya timu hizo tano zilifuzu, Cameroon na Ghana ndizo zimeonekana kushangaza wengi zaidi kutokana na namna zilivyoweza kupata matokeo mazuri ugenini licha ya kufanya vibaya katika mechi zao za kwanza nyumbani jambo ambalo liliaaminisha wengi kuwa zisingeweza kwenda Kombe la Dunia mwaka huu.

Baada ya kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani katika mechi ya mkondo wa kwanza, Cameroon iliweza kupindua meza ugenini kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambao uliwafanya wakate tiketi ya kwenda Qatar kwa kunufaika na kanuni ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Kwa upande wao Ghana ambao awali walionekana ni miongoni mwa timu dhaifu katika kundi la timu zilizotinga hatua ya mwisho ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa Kanda ya Afrika walilazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Nigeria na kusonga mbele kufuatia mchezo wa kwanza baina yao ambao ulichezwa huko Ghana kumalizika kwa sare tasa.

Kitendo cha Ghana kufanya vibaya katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika mwaka huu huko Cameroon ambazo iliishia hatua ya makundi lakini pia sare ya mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Nigeria, ni sababu zilizopelekea imani kuwa timu hiyo ya taifa ingekwenda kuwazuia Nigeria katika ardhi ya kwa Mkapa.

Hapana shaka baada ya mechi zao za kwanza, Ghana na Cameroon zilifanya tathmini ya kina ya kipi kilichowafanya washindwe kupata ushindi katika mechi zao za nyumbani na wakarudi katika viwanja vya mazoezi kufanyia kazi udhaifu na uimara wao kulingana na namna walivyocheza mechi walizoshindwa kupata ushindi na kisha wakajipanga kimbinu jambo ambalo limekuja kuzaa matunda kwao.

Hawakukubali kukata tamaa kirahisi kisa walipoteza mechi zao za nyumbani na waliamua kupambana hadi tone la mwisho la damu kujaribu kupata matokeo mazuri ambayo mwisho wa siku yamekuwa na faida kwa upande wao.

Siku tano baada ya Cameroon na Ghana kushtua wadau wa mpira wa miguu kwa kufuzu Kombe la Dunia huu zikiwa hazipewi nafasi kubwa, wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba watakuwa nyumbani kuikaribisha US Gendarmerie Nationale ya Niger katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Katika mchezo huo, Simba inayoshika nafasi ya tatu katika kundi hilo itahitaji ushindi wa aina yoyote ili ijihakikishie kutinga robo fainali ya mashindano hayo pasipo kutegemea matokeo ya mchezo mwingine baina ya RS Berkane na Asec Mimosas ambao utachezwa huko Morocco, muda na siku sawa na ule wa hapa wa Simba.

Simba ina pointi saba sawa na Berkane huku Asec Mimosas ikiongoza kundi hilo na pointi zake tisa na US Gendarmerie Nationale ikiburuza mkia kutokana na pointi tano ilizonazo.

Iwapo Simba itapoteza dhidi ya Gendarmerie itashindwa kufuzu robo fainali na ikiwa itatoka sare katika mechi hiyo, inaweza kufuzu hatua inayofuata ikiwa tu RS Berkane watapoteza nyumbani dhidi ya Asec Mimosas.

Gendarmerie wao wana kibarua kigumu kidogo kwani wanahitajika kushinda dhidi ya Simba na kuombea Asec Mimosas iifunge Berkane au timu hizo zitoke sare katika mechi yao ya mwisho ili yenyewe isonge mbele.

Hata hivyo kwa kuangalia kile kilichotokea kwa Cameroon na Ghana, Simba haipaswi kwa namna yoyote kujiona iko katika nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi nyumbani dhidi ya Gendarmerie, Jumapili kwani kwa kufanya hivyo itajikuta ikifuata nyayo za Nigeria na Algeria ambazo ilionekana kama zitaenda Kombe la Dunia kirahisi baada ya kupata matokeo mazuri ugenini

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz