Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Tatizo la Waamuzi siyo la Tanzania tu, ni dunia nzima

WAAMUZI 645454 Tatizo la Waamuzi siyo la Tanzania tu, ni dunia nzima

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sijui kwa nini mashabiki wa soka hapa Tanzania wamejawa na mihemko sana. Kila kitu wanajua wao. Wanajua kuliko kitu chochote duniani. Yaani baada ya Mungu ni wao.

Nimeona namna msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania ambavyo mashabiki wa soka wamekuwa wakiwashukia waamuzi. Ni kama vile hawafanyi chochote cha maana.

Ukisikia namna waamuzi wa Tanzania wanazungumzwa huko mitaani ni kama vile ‘takataka’ na hawajui chochote. Inaumiza sana.

Ni kweli waamuzi wetu wana changamoto zao lakini siyo kama zinavyokuzwa huko mitaani. Ni changamoto za kawaida kwenye soka.

Tatizo la Waamuzi liko dunia nzima. Ndio sababu kwa wenzetu waliopiga hatua waliamua kuja na teknolojia mbalimbali ili kuwasaidia Waamuzi kuamua kwa ufasaha.

Walianza na ile ya ‘goal line’. Hii ni teknolojia ya kumsaidia mwamuzi kufahamu kama mpira umevuka mstari wa goli ama la. Tumeona mara nyingi ikiwasaidia waamuzi.

Lakini hapa kwetu waamuzi hawana teknolojia hiyo. Kuna nyakati wanapata wakati mgumu kuona kama mpira umevuka mstari wa goli ama la.

Iliwahi kutokea kwenye mechi moja ya Lipuli na Yanga pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Golikipa alidaka mpira na kuuzungusha kwenye mlingoti wa goli. Refa akaamua iwe kona. Lakini kwa picha za marejeo haikuwa kona bali goli halali.

Iliwahi kutokea pia pale Azam Complex Chamazi. Mwamuzi wa kati alikuwa Jonesia Rukya. Likafungwa goli la utata. Haikufahamika kama mpira umevuka mstari ama la. Lakini mwamuzi msaidizi namba moja alisema ni goli halali. Na kweli ilikuwa goli halali.

Ndio changamoto ya kukosa teknolojia. Lakini pale England ingekuwa jambo rahisi. Teknolojia ya ‘goal line’ ingewasaidia kuamua kwa ufasaha. Tumeona ikitokea mara nyingi.

Hivi karibuni wamekuja na hii teknolojia ya VAR (Video Assistant Referee). Ni teknolojia ya kuamua matukio kwa usaidizi wa picha za Video. Lakini bado imekuwa na changamoto lukuki. Siku hizi waamuzi wa Ulaya na maeneo mengine inakotumika teknolojia hiyo wamekuwa na unafuu wa kufanya maamuzi. Lakini bado huwachukua muda mrefu kuamua kwa usahihi pindi wanapokwenda kutazama video hizo.

Hivi majuzi tu kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia za Afrika tuliona namna mwamuzi alivyotumia faida ya VAR kuwapa penalti Nigeria. Pengine bila teknolojia hiyo angeamua vinginevyo. Lakini ilikuwa penalti halali.

Kwenye moja ya mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu pale Cameroon mwamuzi mmoja alipata sifa lukuki. Ni Bamlak Tessema wa Ethiopia. Huyu alichezesha mechi ya Burkina Faso na Senegal. Katika mechi hii Tessema alifanya maamuzi ya kimakosa mara mbili ya kuizawadia Senegal penalti lakini baadaye alisawazisha kwa msaada wa VAR. Vipi teknolojia hiyo isingekuwepo? Hilo halizungumzwi.

Wengi walimpongeza kwa madai kuwa pamoja na uwepo wa VAR bado waamuzi wengine wanafanya maamuzi yaliyojaa utata. Wamejaa utetezi kwa wageni, lakini Waamuzi wa Tanzania wakikosea wanawasema sana.

Pale England katika pambano la Manchester City na Manchester United lilitokea pia tukio la utata. Riyad Mahrez alifunga goli likaamuliwa kuwa ameotea lakini baada ya kutazama VAR ikabainika kuwa ni goli halali. Maamuzi yakabadilika.

Kwanini hatukumlaumu Mwamuzi msaidizi namba mbili kwa kuinyima City goli halali? Ni kwasababu haki ilitendeka palepale Uwanjani kwa msaada wa teknolojia. Sisi hatuna msaada huo.

Waamuzi wetu wanachezesha mechi katika mazingira magumu. Wanalipwa fedha kiduchu. Fedha hizo pia mpaka kuzipata watasubiri sana. Viwanja siyo rafiki.

Hawana faida ya teknolojia. Wanafanya kazi wakiwa na mawazo kibao vichwani kutokana na shida za maisha. Nani wa kuwasaidia? Hakuna. Wameachwa peke yao kama yatima.

Kila wanalokosea tunawasema kama ndio wao wanakosea tu Dunia nzima. Hatuoni kama makosa mengine ni ya kibinadamu tu. Japokuwa wapo wengine hatuwezi kuwatetea.

Mfano yule aliyewapa Yanga penalti dhidi ya Namungo pale Lindi. Yule anapaswa kurudi shule kidogo. Kuna yule aliyewapa Simba penalti dhidi ya Tanzania Prisons. Naye anapaswa kurudi shule. Lakini wengine wengi wanafanya makosa ya kawaida. Ni makosa yanayofanyika dunia nzima.

Badala ya kukaa na kuwatukana tu Waamuzi wetu, tutafakari namna ya kuwasaidia kufanya kazi yao kwa ufanisi katika mazingira yetu. Hatuwezi kuwa na VAR kwa sasa lakini kwa pamoja tunaweza kuona namna bora ya kuwasaidia kupandisha viwango vyao.

Mfano kila baada ya mechi wapewe video zao, wakae na mtathimini wa waamuzi na kuutazama mchezo upya. Waone makosa waliyofanya na watazame namna bora ya kuamua kwa wakati mwingine. Je kwa sasa wanafanya hivyo? Hapana.

Waamuzi wanaochezesha mechi za CAF hufanya hivyo. Kabla ya kuondoka katika nchi husika ni lazima wakae na mtathimini wa waamuzi ama kamisaa wa mchezo na kupitia upya video ya mchezo huo. Wanajadili mambo yote muhimu.

Mechi zinazofuata wanakuwa bora zaidi. Ila sisi tumekaa kuwalaumu tu. Mashabiki wanawalaumu. viongozi wao wanawalaumu. Wakimbilie kwa nani?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz