Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Shafii Dauda amefungiwa kwa kusema ukweli

Dauda Pic Data Mchambuzi wa Soka, Shaffih Dauda

Mon, 21 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mpira wetu unakwenda wapi? Ni swali linaloumiza kichwa sana. Kuna mambo hayapo sawa na bahati mbaya wanaohoji wanaonekana maadui. Ndipo tulipofikia? Inaumiza sana.

Wiki hii nchi ilipata mshtuko baada ya mdau wa soka, Shafii Dauda kufungiwa kwa miaka mitano. Amefungiwa kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi. Inashangaza sana.

Mbali na kufungiwa, pia ametakiwa kulipa faini ya Sh6,000,000. Kwa kosa gani? Hapa ndipo panapofikirisha.

Dauda anadaiwa kutumia mtandao wake wa Instagram kuchapisha habari zinazodaiwa za uongo kuhusu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unamfungiaje mtu kujihusisha na soka kwa miaka mitano kwa kosa la kuchapisha habari mtandaoni?.

Wanachoshindwa kutambua wenye mamlaka ni kwamba kuna Dauda wawili. Wa kwanza ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutoka Chama Cha Soka Dar es Salaam (DRFA). Huyu ni kiongozi wa soka. Anahukumiwa kwa matendo ya soka.

Halafu kuna Dauda ambaye ni chombo cha habari. Huyu sasa hawajibiki kwa TFF wala DRFA. Huyu hawajibiki kwa watu wa mpira. Hiki ni chombo cha habari na kinaendeshwa kwa sheria zake. Kuna mamlaka zake. Huwezi kumhukumu Dauda wa DRFA kwa kosa lililofanywa katika chombo chake cha habari. Haya wenye mamlaka walipaswa kuyafahamu. Pengine pia wanayafahamu lakini hawakutaka kuyatilia maanani.

Pili turudi katika kosa la msingi. Nini Dauda alisema hadi kufungiwa? Ni kipi hicho kinachoitwa ‘chapisho la uongo’? Hapa ndipo penye mshtuko zaidi. Kwa kifupi, Dauda amefungiwa kwa sababu chombo chake kilisema ukweli kuhusu TFF na Bodi ya Ligi pamoja na mikataba ya udhamini.

Chombo cha Dauda kilihoji kwanini TFF ilizuia wadau wasihoji kuhusu mkataba wa GSM? Sasa hapo kuna kosa gani. Kwanini uzuie watu kuhoji? Hapa palikuwa na utata kweli.

Mkataba wa GSM na TFF ulionekana kuwa na dosari tangu siku ya kwanza. Ulionekana kuwa na mgongano wa kimaslahi, lakini watu walikatazwa kusema. Ukihoji ama kusema unaonekana adui. Ni ajabu na kweli. Uliona wapi kampuni moja inadhamini timu tatu kwenye ligi moja halafu wakati huohuo viongozi wa kampuni hiyo wanaonekana kuwa na maslahi binafsi na timu moja. Wapo Sportpesa wanadhamini timu tatu, lakini hawajawahi kuwa na maslahi binafsi na timu mojawapo.

Mwisho wa yote kampuni hiyohiyo inaingia tena mkataba wa kudhamini ligi halafu katika hafla ya utiliaji sahihi wanakuja wale viongozi walioko mstari wa mbele katika timu hiyo moja. Kulikuwa na ulazima gani wa kufanya hivyo?

Ni wazi kuwa mkataba huu ulikuwa na mgongano wa kimaslahi tangu mwanzo na ndiyo sababu umeshindwa kudumu. Ni timu chache tu zilifumba macho ili kupata pesa. Lakini mioyoni mwao waliona kuna tatizo. Nani wa kusema hili? Hakuna. Na ndiyo maana chombo cha Dauda kilipofanya hivyo mmiliki wake akafungiwa. Pia, suala la Bodi ya Ligi kutakiwa kuwa mtetezi wa klabu liko wazi kabisa. Lakini je Bodi ya Ligi inazitetea klabu ama TFF? Hapa ndipo penye shida.

Bodi ya Ligi kwa sasa ipo kwa maslahi ya TFF. Haina meno ya kuihoji TFF kwa maslahi ya klabu. Hiki ndicho kilichokuwa kinahojiwa, lakini kimeishia kumponza Dauda. Yote kwa yote, hata kama Dauda ‘amekosea’ bado adhabu iliyotolewa ni kali mno.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz