Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Kuna ushamba mwingi kwenye usajili Bongo

Azizi Usajili Stephen Aziz Ki amesajiliwa Yanga

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Usajli kwa timu za Ligi Kuu umeshika kasi. Kila timu inajipambanua kushusha kifaa kipya. Kila timu inajinasibu kushusha wachezaji wa maana zaidi ya wapinzani wao.

Kasi ni kubwa zaidi kwa Simba, Yanga na Azam FC. Hawa ndio wababe wa soka letu. Kila mmoja anajinasibu kufanya usajili wa mashindano ya kimataifa. Inafurahisha sana.

Hata hivyo, kumekuwa na ushamba mwingi na ulimbukeni katika usajili wa timu zetu. Kwanza, timu inaona isiposajili itakuwa haijajiandaa na msimu mpya. Halafu kila timu inaamini kwenye kusajili wachezaji wengi.

Ushamba mkubwa sasa umekuja kwa mashabiki kuamini wachezaji wa kigeni ni bora kuliko wazawa. Yaani akisajiliwa mzawa watasema mchezaji wa kawaida, ila mgeni sasa watasema ni mashine ya soka. Inachekesha sana.

Tuanze na huu ushamba wa kusajili wachezaji wengi. Simba msimu uliopita ilisajili wachezaji wapya 12. Ilifanya usajili huo mkubwa ikiwa imetoka kushinda mataji yote ya ndani pamoja na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu iliyotoka kutwaa Ngao ya Hisani, Kombe la FA na Ligi Kuu inahitaji usajili wa nyota wote hao? Hapana. Kuna ushamba na ulimbukeni mwingi hapa. Watu wanaamini zaidi kwenye wachezaji wapya kuliko kujenga timu.

Nini kilitokea? Baada ya muda mfupi Duncan Nyoni akaachwa. Wachezaji wengine kama Jimmyson Mwanuke, Yusuf Mhilu, Israel Mwenda hawakuwa na chochote cha maana. Huu sasa ndio ulimbukeni wenyewe wa kusajili.

Mfano kulikuwa na haja gani ya kumsajili Jeremiah Kisubi kwenye timu yenye Aishi Manula na Beno Kakolanya? Pengine huu ni ubadhilifu tu wa pesa. Ni matumizi mabaya. Unaweza kukuta Kisubi ambaye hakudaka hata mechi ya kirafiki pale Simba kavuna mamilioni tu ya kutosha.

Msimu huu Simba imetangaza kusajili wachezaji nane. Pengine wanaweza kuongezeka. Swali ni je Simba inahitaji wachezaji wote hao? Sidhani.

Timu iliyotoka kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu. Imefika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Inahitaji wachezaji nane wapya? Hapana. Kuna ulimbukeni wa kusajili hapa.

Twende kwa Yanga. Msimu uliopita nayo ilisajili wachezaji zaidi ya 12. Ni wangapi waliotumika vizuri? Ni wachache tu.

Kuna wachezaji kama Eric Johola, David Bryson, Yusuph Athuman, Crispin Ngushi, Chiko Ushindi na wengineo hawajawa na lolote la maana. Ni wachezaji wa kawaida tu. Lakini walisajiliwa kwasababu ya ushamba na ulimbukeni.

Ukweli ni kwamba Simba na Yanga zinaamini zaidi kwenye kusajili wachezaji wapya na siyo kujenga timu.

Yanga pamoja na kutwaa ubingwa bado imesajili wachezaji watano wapya. Pengine wanaweza kuongezeka huko mbeleni. Kwa nini? Kwa sababu wanapenda kusajili.

Tazama namna usajili wa Stephane Aziz Ki ulivyofanyika. Ni kama vile filamu ya kibongo. Kiongozi amekwenda kupiga picha na mchezaji kabla hawajakubaliana lolote.

Nini kimetokea? Mwishowe Yanga imelazimika kulipa fedha nyingi kuliko thamani halisi ya mchezaji mwenyewe. Kwanini? Kwasababu ya ushamba na ulimbukeni.

Mchezaji akafahamu kabisa Yanga haiwezi kuishi bila yeye. Akaikamua kisawasawa. Narudia tena, Yanga wameumia kwenye usajili wa Aziz Ki kwasababu tu ya ushamba. Wangekwenda kwa weledi, wangempata kwa bei nafuu tu.

Ubaya ni kwamba unaweza kusajili mchezaji kwa madoido mengi na bado akashindwa kufanya vizuri. Nini kilitokea kwa Michael Sarpong na Carlos Carlinhos? Walisajiliwa kwa mbwembwe na hawakufanya chochote cha maana.

Ushamba na ulimbukeni huu wa kusajili wachezaji wapya sasa umehamia hata timu za daraja la kati. Tazama timu kama Dodoma Jiji tayari imesajili wachezaji kibao kuelekea msimu mpya. Na bado ipo bize kusajili.

Kwa nini wanafanya hivyo? Kwa sababu nao wameanza kuamini katika usajili kuliko kujenga timu. Wachezaji siku hizi wanasajiliwa kwa mikataba ya mwaka mmoja mmoja. Yaani msimu ukiisha, mkataba umeisha.

Sasa utajengaje timu kwa kusajili wachezaji kwa mwaka mmoja? Huwezi. Kwa nini wanafanya hivyo? Pengine kuna kamisheni wanazipata kwa kusajili wachezaji wapya. Pengine kula ya viongozi wengi imekaa kwenye usajili. Watu labda wanakula asilimia 10 ama 20.

Ushamba huu wa usajili sasa umekwenda hadi kwa mashabiki. Nao wanashindana kwenye tambo za usajili. Utawasikia wakisema ‘Umeona kifaa hicho?’ Wakimaanisha kuwa timu yao inajipanga zaidi ya nyingine.

Imefikia hatua sasa timu isiposajili inaonekana kama haifai na haijajipanga. Ni ushamba ulioje. Kuna timu wala hazina haja ya kusajili hasa kama zinabaki na wachezaji waliokuwepo.

Kuna timu zinahitaji wachezaji wawili tu kujiimarisha. Lakini utashangaa timu hizo zikasajili wachezaji hata saba kisa tu wameona wenzao wanasajili.

Tazama kama Kagera Sugar imeachana na wachezaji tisa. Unadhani hapo itasajili wangapi?

Columnist: Mwanaspoti