Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Inawezekana Bocco mwenyewe hajui kimempata nini

John Rafael  Bocco John Bocco

Mon, 18 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kuna nyakati maisha yanashangaza. Ni kama nyakati hizi zinazomkumba nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’. Ni nyakati ngumu hata kuzielewa tu. Bocco ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita. Bahati nzuri pia alikuwa mfungaji bora wa msimu huo.

Licha ya kukumbwa na majeraha kwa nyakati tofauti alisimama imara na kuibeba Simba katika nyakati ngumu. Pamoja na ukweli kwamba ile tuzo ya mchezaji bora ilipaswa zaidi kwenda kwa Clatous Chama, bado Bocco alikuwa imara msimu jana.

Ulikuwa msimu wa saba kwa Bocco kufunga mabao 10 ama zaidi kwenye Ligi Kuu achilia mbali mashindano mengine. Nini kimemkuta Bocco msimu huu? Hapo ndipo panaposhangaza. Bocco ameanza akiwa ovyo kwelikweli. Hana makali na hatishi tena. Utulivu na hesabu zake mbele ya lango havipo tena.

Wakati Ligi Kuu ikiingia raundi ya 20, Bocco bado hajafunga. Sina hakika kama amefunga hata la kuotea likakataliwa. Sina hakika.

Nani aliyawaza haya? Mfungaji na mchezaji bora wa msimu uliopita anawezaje kukaa miezi saba sasa bila

kufunga bao? Inaumiza sana. Bocco ndiye straika hatari zaidi kuwahi kutokea katika ligi yetu. Namba zinajieleza. Katika miaka 14 aliyocheza amefunga mabao 143. Nani anaweza kufikia rekodi hiyo? Hakuna, lakini Bocco ameweza. Pamoja na rekodi hizo msimu huu Bocco amekuwa wa kawaida. Amekuwa butu kuliko Michael Sarpong aliyekuwa Yanga msimu uliopita.

Yaani imefikia hatua sasa Bocco na Heritier Makambo wa Yanga wamekuwa wachezaji wa daraja moja. Nyakati bora za Bocco zimekwenda wapi? Bahati mbaya zaidi ni kwamba hata Bocco mwenyewe hajui nini kimemkuta. Haelewi kabisa. Alishasahau nyakati hizi. Alikuwa na changamoto kama hii katika msimu wake wa kwanza tu wa ligi ambapo alimaliza akiw-a na bao moja pekee. Ilikuwa 2008/09. Tangu hapo alikuwa moto wa kuotea mbali.

Ni kweli sasa Bocco amekwisha? Sitaki kuamini hivyo. Ni kweli mastraika hufanya vizuri na kisha kupotea, lakini haitokei haraka hivyo. Kwa Bocco imekuja ghafla mno.

Kuna kitu hakipo sawa. Kuna baadhi ya watu waliamini kuondoka kwa Chama na Luis Miquissone kumechangia Bocco kukwama, lakini bado ni ngumu kuamini hilo. Chama amerudi na ana miezi mitatu sasa, Bocco amefunga mabao mangapi? Hakuna. Hii ni ishara kuwa tatizo la Bocco ni zaidi ya kukosekana kwa Chama. Kwa tathmini yangu kitu kikubwa ambacho kimemkuta Bocco msimu huu ni mabadiliko ya kocha na ujio wa huyu Pablo Franco. Makocha wengi kutoka Uhispania hawaamini katika mfumo wa mastraika. Wanaamini zaidi katika viungo na mawinga.

Ndio sababu tangu ujio wa Pablo mastraika wote wa Simba hawajaweza kuwa tishio. Ni Meddie Kagere ambaye anajitahidi kwa mbali. Lakini hata Mugalu naye anapitia nyakati ngumu kama za Bocco.

Simba hii ya Pablo inawapa zaidi nguvu viungo na mawinga. Ndio maana Pape Sakho, Kibu Denis, Bernard Morrison na Peter Banda wamefunga zaidi ya Bocco na Mugalu. Ndio maana Chama ndani ya muda mfupi tu amefunga kuliko Bocco na Mugalu.

Unaikumbuka mechi ya Kagera Sugar na Simba pale Kaitaba? Pablo aliamua kucheza mechi hiyo bila straika halisi. Alianza na viungo watupu. Hawa ndio makocha wa Kihispania. Wanaamini zaidi katika falsafa za Pep Guardiola.

Wanaamini ili wafanikiwe zaidi wanahitaji kutumia viungo kuliko mastraika. Ndio soka la Pep pale Manchester City. Pep sio muumini sana wa mastraika na timu yake bado ni tishio Ulaya.

Tatizo ni kwamba mazingira ya Afrika na Ulaya ni tofauti. Ili ufanikiwe Tanzania hasa katika viwanja ya mikoani unahitaji ubora wa Bocco, Mugalu na Kagere.

Katika misimu hii minne ambayo Simba ilishinda taji la Ligi Kuu, Kagere na Bocco walikuwa roho ya timu. Alikuwepo pia Emmanuel Okwi na msimu uliopita aliongezeka Mugalu.

Pamoja na ubora wa Chama, alitegemea pia kazi yake kurahisishwa na umaliziaji mzuri wa mastraika. Ndio maana kwa misimu miwili mfululizo Chama aliongoza kwa pasi za mabao maana nyota hao walikuwa wakifunga.

Bahati mbaya kama taifa, bado tunahitaji ubora wa Bocco. Hatuna mastraika wengi wa ligi ya ndani wanaoweza kuvaa viatu vyake. Angalau msimu huu tumeona Reliants Lusajo wa Namungo na George Mpole wakijitahidi. Vinginevyo hakuna mwingine.

Tunamsaidia vipi Bocco kurejea katika makali yake? Ama tumpe video za mabao ya Fiston Mayele awe akitazama kila siku?

Hata Manara anamkubali Ahmed Ally kimoyomoyo

Kila falme na zama zake. Kila utawala na zama zake. Ndicho unachoweza kusema ukimzungumzia Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

Baada ya Haji Manara kutamba kwa maneno ya shombo, kejeli na dharau kwa miaka mingi, hatimaye Ahmed ameibuka na kuondoka na kijiji chote.

Hakuna mtu aliyetazamia Tanzania anaweza kutokea mtu mwingine na kuifanya kazi ya habari ndani ya klabu kwa ufasaha kuliko Manara. Wengi waliishia kuzikumbuka nyakati za Jerry Muro. Huyu ndiye mtu aliyefanya vyema kuliko Manara katika miaka ya karibuni. Nani mwingine angeweza? Hakuna. Ila sasa amekuja Ahmed. Ndani ya siku 100 tu kazini amemfunika kabisa Manara na wafuasi wake. Ahmed yupo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Anavuta hewa na upepo wa peke yake.

Uzuri ni kwamba Ahmed ametafuta njia bora zaidi ya kuifanya yake. Anakwenda mtaa kwa mtaa. Anawafuata wana Simba walipo. Baada ya hapo anatembelea vyombo vya habari kimoja baada ya kingine. Habagui.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz