Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Hili la Hersi kugombea Urais Yanga limekaaje?

Injinia Hersi Said, Caamil Mkurugenzi wa Uendeshaji wa GSM, Hersi Said

Mon, 13 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mchakato wa uchaguzi umepamba moto pale Yanga. Umefunguliwa kwa haraka na zoezi la kuchukua na kurudisha fomu limekwisha.

Ila jambo kubwa limenishtua katika mchakato wa awali. Ni kitendo cha Mkurugenzi wa Uendeshaji wa GSM, Hersi Said kuchukua fomu ya kugombea urais.

Hersi amechukua fomu ya kugombea urais kwa upande wa wanachama. Ni kweli kama mwanachama ana haki. Ni kama ilivyo kwa wanachama wengine wa Yanga.

Ila ni wazi kitendo hicho kinaacha maswali mengi kuliko majibu. Kwanini? Subiri nitakwambia.

Kwanza, Hersi ndiye aliyesimamia mchakato wote wa mabadiliko pale Yanga. Ndiye aliyefanya kazi kwa karibu na La Liga pamoja na Sevilla katika mchakato huo.

Ndiye aliyekwenda Hispania kupewa darasa. Ndiye aliyerudi nchini kuwafundisha wenzake juu ya mabadiliko hayo. Picha na kumbukumbu zote zipo.

Ni jambo zuri kuwa Hersi anayafahamu mabadiliko ya Yanga kuliko mtu yeyote yule. Mwalimu atabaki kuwa mwalimu tu.

Hersi na GSM ndio wamesimamia huu mchakato wa usajili wa wanachama. Ndiye roho ya mradi mzima. Mradi ambao umekuwa na mafanikio makubwa.

Kwa kifupi haya mabadiliko yote ya Yanga yamefanikiwa kwa usimamizi wa Hersi. Kina Senzo Mbatha, Wakili Simon Patrick, Haji Mfikirwa na wengineo wamekuwa wasimamizi wa mchakato tu. Lakini akili yote ameibeba Hersi.

Pili, mradi mzima wa GSM pale Yanga umekuwa ukisimamiwa na Hersi. Ndiye anayefanya usajili. Ndiye anasimamia bajeti. Ndiye anazungumza na makocha. Kwa kifupi ni mtu mwenye uamuzi mkubwa. Huwezi kuyatenganisha mafanikio ya Yanga kwa misimu hii miwili na Hersi. Amekuwa na mchango na usimamizi mkubwa.

Yanga ilishaanguka ila imenyanyuliwa na GSM kwa usimamizi wa Hersi. Ni jambo la kupongezwa. Lakini bado swali linabaki kuwa ni sahihi Hersi kugombea urais Yanga? Kuna tatizo? Twende pamoja nitakueleza. Yawezekana kuna tatizo ama lisiwepo. Inategemea unatazamaje.

Wasiwasi ni kwamba isije ikawa Hersi alifanya haya yote ili kujitengenezea mfumo rahisi wa yeye kuwa rais wa Yanga. Hapa kunafikirisha kiasi.

Pili, Hersi ni mtu wa GSM ambao wamekuwa wafadhili wa Yanga kwa muda. GSM ni wadhamini pia wa Yanga kupitia magodoro yao. Pia ndio washindi wa zabuni ya jezi pale Yanga.

Pia watu wengi wanatarajia GSM watakuwa wawekezaji pale Yanga. Je hakutakuwa na mgongano wa kimaslahi?

Yaani Hersi ambaye ni mtu wa GSM anagombea upande wa wanachama ambako kuna asilimia 51 za hisa. Halafu itokee GSM wanachukua uwekezaji upande wa pili. Hii itakuwaje?

Lakini hatuwezi kumhukumu Hersi kwa hilo maana bado GSM hajaomba zabuni ya kuwa mwekezaji. Lakini pia kama ataomba zabuni bado Hersi ana mambo ya kufanya ili kuondoa mgongano huu. Anaweza kuachia nafasi zake pale GSM ili kuwa rais wa Yanga. Ataweza kufanya hivyo? Ni kusubiri na kuona.

Yote kwa yote mfumo mpya wa mabadiliko pale Yanga unahitaji rais imara na makini. Inahitaji mtu anayefahamu mabadiliko vizuri na kuyasimamia.

Anaweza kuwa Hersi ama mtu mwingine. Muhimu ni kwamba mtu atakayekuwepo asimamie zaidi maslahi ya Yanga kuliko maslahi binafsi ama ya mtu fulani.

Soka la sasa linahitaji fedha. Soka la sasa linahitaji watu ambao wanaweza kutafuta fedha na kuzisimamia. Vinginevyo Simba na Yanga zitabaki kulekule.

Miaka yote kila mtu ametamani kuona Simba na Yanga zikijiendesha na kuacha kutegemea fadhila za watu. Watu wanatamani kuona zinamiliki viwanja vyao. Ni kweli viongozi wanaokuja sasa wana nia hiyo? Tusubiri tuone. Ni jambo la muda tu.

Columnist: Mwanaspoti