Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: GSM, Mo Dewji ndio wakombozi wa soka letu

Gsm,mo GSM, Mo Dewji ndio wakombozi wa soka letu

Mon, 28 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tunaishi katika nyakati bora sana katika soka la Tanzania. Nyakati ambazo matajiri wameamua kukunjua nafsi na kuwekeza katika soka. Wanamwaga fedha kama mchanga.

Walipita matajiri wengi kipindi cha nyuma kama Abbas Gulamali, Azim Dewji, Yusuph Manji na wengineo. Ni watu ambao walitumia fedha zao nyingi kuendesha soka. Ila baada ya muda wakaamua kuacha.

Baadaye akaja Said Salim Bakhresa na sasa tunao pia Mohammed Dewji ‘Mo’ na Gharib Said Mohammed (GSM). Watu wenye fedha kweli kweli. Wingi wa fedha kwao ni kama ilivyo wingi wa shida kwetu.

Bahati mbaya ni Watanzania wengi hatuna heshima na uwekezaji unaofanywa na matajiri hawa katika soka. Tunaona kama wanafanya jambo la kawaida, lakini ukweli, wanajitoa sana kwa ajili ya soka letu.

Gharama za kuendesha timu ya soka ni kubwa mno kwa sasa. Kumnunua mchezaji mmoja wa maana kama Fiston Mayele si chini ya Sh200 milioni. Fikiria kuwa na wachezaji wengi wa maana inabidi utumie kiasi gani cha fedha.

Klabu ya Yanga ndani ya miaka miwili tu iliyopita imetumia mabilioni ya fedha kwenye usajili. Bahati mbaya ni unaweza kununua wachezaji kwa fedha nyingi na bado wakashindwa kufanya vizuri. Ndicho kilichowakuta Yanga msimu uliopita.

Walikwenda kutafuta mchezaji aina ya Mayele wakakutana na Michael Sarpong. Mchezaji mgumu na asiyenyumbulika uwanjani. Ikawa ni hasara. Akakaa Yanga mwaka mmoja akila pesa za bure na baadaye ikabidi tena kumlipa fedha za kumvunjia mkataba.

Lakini fedha hizi matajiri wetu wanazitoa na wamekubali kubeba huo mzigo. Ni kama vile Simba walivyokwenda kutafuta straika bora zaidi ya Meddie Kagere halafu wakakutana na Junior Lokosa. Straika butu kweli kweli. Akala pesa za bure na kusepa zake. Ndio hasara za soka.

Bado hatujazungumza gharama za mishahara kila mwezi. Mfano mzuri Simba na Yanga mishahara yao ni mikubwa. Yanga kwa mwezi mmoja inalipa mishahara inayozidi Sh350 milioni. Simba nao wanacheza mule mule. Hizi fedha zinatoka wapi?

Udhamini wa kampuni unazoziona kwenye klabu hizi kubwa fedha zake hazitoshi kulipa mishahara kwa angalau miezi mitano tu. Haziwezi. Fedha nyingine zinatoka wapi? Ni kwenye mifuko ya Mo Dewji na GSM.

Vipi kuhusu kambi? Bosi mmoja wa Simba aliwahi kuniambia gharama za mwezi mmoja katika kambi yao kule Mbweni si chini ya Sh80 milioni. Yanga pia wana gharama zinazofikia ama kuzidi hapo katika kambi yao pale Avic Town. Fedha hizi anatoa nani? Ni hao hao matajiri wa timu hizo.

Turudi katika mashindano ya kimataifa. Safari moja tu ya Simba kwenda kucheza nje ya Tanzania inagharimu hadi Sh300 milioni ikiwemo posho na masilahi ya wachezaji pamoja na watendaji wengine.

Simba msimu huu tayari imesafiri kwenda nje mara tano. Wametumia kiasi gani cha fedha?

Ni pesa nyingi hata kwa kuzitamka tu. Lakini bilionea kijana zaidi Afrika, Mo Dewji anatoa bila kinyongo chochote na maisha yanakwenda. Fedha itakayopewa Simba kwa kufika hatua ya makundi haitoshi hata nusu ya gharama walizotumia katika mashindano hayo. Bila uwepo wa Mo Dewji ingekuwaje?

Ndio maana nasema hawa matajiri wanahitaji heshima. Soka linakula pesa kweli kweli. Ni kama vile mchwa anavyotafuna mbao. Ni zaidi ya pombe na wanawake.

Kama tajiri hana mapenzi na soka, hawezi kudumu kwenye klabu kwa muda mrefu. Kwa mwaka mmoja anaweza kutumia fedha kwenye soka kuliko sehemu nyingine yoyote. Bahati mbaya ni kwamba fedha hizi zinatoka tu, hazirudi.

Ndio sababu kila siku Mo Dewji huwa anasema Simba inajiendesha kwa hasara.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz