Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MPIRA: Azam FC ina shida gani?

Azam FC Ratba Bara Azam FC ina shida gani?

Mon, 13 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ghafla sana Azam FC imeondoka kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Ghafla sana wakati ndio kwanza mambo yameanza kuchanganya.

Azam imeondoka kwenye mbio za ubingwa mapema kuliko ilivyotarajiwa. Ni katika msimu ambao watu wengi waliona kama wamebadilika na kudhamiria kufanya jambo. Lakini wapi, wameishia kwenye kiwango cha aftatu. Inachekesha sana.

Wakati huu zikiwa zimesalia raundi nane kabla ya Ligi kumalizika, Azam FC tayari imeachwa alama 16 na vinara Yanga. Ni alama nyingi sana kwa timu kama Azam ambayo ina kila kitu.

Ubaya ni kwamba Azam FC imeshindwa kuwa na kiwango bora katika msimu ambao imejaribu kila kitu kwa ukubwa wake.

Kama ni usajili Azam FC imefanya usajili mkubwa mno. Ilishusha wachezaji wawili bora kutoka Ligi ya Ivory Coast ambao ni Tape Edinho na Kipre Junior. Kwenye Ligi ya Ivory nyota hawa pamoja na Stephane Aziz Ki walivyafanya vizuri sana. Azam ikasepa na wawili.

Ikasajili kiungo James Akaminko. Nani asiyejua uwezo wa Anaminko? Bonge moja la fundi. Kama anapiga kama anazima. Kila timu kubwa nchini inammezea mate.

Baada ya hapo ikamchukua Issah Ndala kutoka pale Nigeria na beki Malikou Ndoye. Kwa kifupi Azam FC ilisajili wanaume wa shoka kwaajili ya msimu huu.

Bahati mbaya ni yule kipa wao Ali Ahmada ameshindwa kuwa katika ubora wake. Ndiye kipa mwenye wasifu mkubwa zaidi nchini. Amecheza mpaka Ligi Kuu Ufaransa. Lakini bahati mbaya ametua kwenye Ligi ya Bongo akawa na kiwango cha kawaida. Ukipiga tu, imo.

Azam FC imetumia fedha nyingi sana kwa huyu kipa. Usajili wake pekee uligharibu karibu milioni 500. Analipwa Sh 23 milioni kwa mwezi.

Ana marupurupu kibao na hadi watoto wake wanasomeshwa shule za gharama. Wamempa gari ya kifahari ya kutembelea jijini Dar es Salaam.

Azam FC iliamini tiba golini kwao sasa imepatikana. Ni maajabu makubwa.

Msimu huu Azam FC imerejesha zile posho wachambuzi walizokuwa wakiwapigia kelele kwa siku nyingi. Timu ikishinda mechi moja ya Ligi wachezaji wanapewa hadi 25 milioni.

Achana na ahadi ya kushinda mechi kubwa. Lakini bado matokeo kwao yamekuwa magumu kama maisha ya sasa.

Wakanunua basi la kisasa aina ya Irizar. Wachezaji wanasafiri kwa ndege safari zote za mikoani. Wanalala hoteli nzuri. Wamerudisha makomandoo wao wote kupambana nje ya Uwanja lakini wapi. Inaumiza sana.

Kwa kifupi Azam FC msimu huu imefanya karibu kila kitu walichopaswa kukifanya lakini mambo bado hayajaenda kama yalivyopaswa kwenda.

Kwa namna walivyowekeza walipaswa angalau kuwa wameachwa alama mbili ama tatu tu na Yanga. Walistahili hilo.

Ila pamoja na yote bado naona changamoto kadhaa za kufanyia kazi pale Chamazi. Unajua ni zipi? Subiri nitakueleza taratibu.

Changamoto ya kwanza ni benchi la ufundi. Azam inahitaji makocha angalau wawili wa maana. Msimu huu imefundishwa na Kally Ongala na Aggrey Morris kwa muda mwingi.

Hawa ni makocha ambao vyeti vyao vya sasa havitoshi hata kuwa makocha wasaidizi. Wana leseni C za CAF ambazo ni ndogo mno. Ni leseni ambayo hata Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe anayo. Ni aibu.

Azam inahitaji kocha wa maana mwenye uzoefu na soka la Afrika. Kocha ambaye anafanya mambo kwa kushirikiana na wenzake. Sio kuendelea na huu ubabaishaji wa sasa.

Pili, Azam inahitaji washambuliaji wa maana zaidi. Wale kina Prince Dube na Rodgers Kola wanawapotezea muda tu.

Yule Dube alifanya vizuri msimu wa kwanza lakini kusema kweli majeraha yamemrudisha nyuma sana. Msimu wa pili anaitafuta fomu yake bado hajaipata. Timu kubwa hazihitaji mchezaji anayetafuta fomu yake kwani kila wiki wanahitaji mabao.

Tazama kilichotokea pale Dodoma majuzi. Dube anakosa mabao hadi wewe uliyeko nyumbani unaona aibu.

Sina mashaka sana na uwezo wa Idris Mbombo ila sijui kwanini makocha hawamwamini sana. Sijui kwanini hawampi nafasi ya kutosha. Huyu anajua zaidi kufunga.

Eneo la mwisho ni usimamizi wa timu. Azam inatakiwa kuendelea kuboresha ufanisi wa watendaji wake na wasimamizi wa timu. Kuna mahali panavuja itakuwa. Wanahitaji kuziba.

Columnist: Mwanaspoti