Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MASHABIKI: Samatta, Msuva wameweza, nyie mnashindwaje kwani?

Samata Pic Mbwana Samatta na Simon Msuva

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dunia inaenda kwa kasi sana. Katika zama hizi, kila kitu kimebadilika. Kuanzia maisha ya kawaida hadi yale ya soka. Soka la kisasa limelainishwa na kurahisishwa mno tofauti na lile la kina Pele. Leo makipa wanalindwa dhidi ya hila za washambuliaji watukutu. Washambuliaji wanalindwa dhidi ya mabeki wenye roho mbaya. Mabeki wakorofi ambao kuna wakati huweka utu kando na kuuvaa uhayawani, kiasi cha kudiriki kuwarukia wenzao miguu ya shingo.

Hawa kina Pascal Wawa, Aggrey Morris au Kelvin Yondani kama sio Juma Nyosso wanaodaiwa wana matukio ya kitemi, ni sehemu ndogo sana ya mabeki wa kipindi cha nyuma. Salum Kabunda ‘Ninja’ hakupewa jina kishabiki tu. Alikuwa Ninja kweli. Kuna mtu aliitwa Roster Ndunguru. Aliichezea Nyota Nyekundu. Alikuwa mbabe kwelikweli na asiyeishiwa vituko uwanjani. Ieleweke tu, sio kama wachezaji wakorofi na wenye roho mbaya katika soka la kisasa hawapo. La, wapo tele, ila sheria zinawabana. Wachezaji wakorofi walianza kitambo, lakini zilitengenezwa sheria kuwabana, ndio maana leo, Sergio Ramos, Diego Costa, Pepe na wengine na ubabe wake kuna wakati wanalainika. Wanabanwa na mabadiliko ya sheria na kanuni za soka. Kuna wakati wanatamani kufanya yao, lakini wanaogopa kibano!

Kuna marekebisho makubwa ya sheria katika soka. Mabadiliko yaliyogusa hadi soko la nyota wa mchezaji huo. Soko la wachezaji nalo limerahisishwa na kupanuliwa mno. Leo wachezaji wanauzwa na kununuliwa kama bidhaa nyingine sokoni. Inategemea tu ubora wake. Wachezaji nao wameijua thamani yao na kuvitumia vyema vipaji vyao kupiga fedha.

Japo mkoloni aliwalemaza wengi kwa kuwaaminisha mtu kuwa na elimu nzuri ndio kujitengenezea maisha, lakini ukweli haupo hivyo. Asilimia kubwa ya wanamichezo wanaishi kitajiri kuliko hata waliobukua vitabu mashuleni. Ukoloni uliwatia ujinga wengi. Walitengeneza mfumo wa kuwaaminisha watawaliwa kuwa ukisoma utaajiriwa na wengi wamelemaa hivyo. Hata hapa nchini bado elimu haijawa msaada mkubwa kwa wasomi. Haiwajengi wasomi kujiajiri kwa vile mitaala ya kikoloni imebaki kama ilivyo, yaani soma uajiriwe. Lakini kwenye soka hali ni tofauti. Mambo yamebadilika. Kadri unavyokuwa na kipaji kikubwa ndivyo unavyoweza kuvuna mamilioni ya fedha na kuuzwa au kununuliwa kokote na yeyote! Wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea na hata katika barani Afrika, wanajua soka kwa sasa ni ajira na biashara. Biashara inayolipa, ndio maana matajiri wameamua kuwekeza katika biashara hiyo na wamekuwa wakivuna faida ya kutosha.

Ni bahati mbaya tu, Watanzania walio wengi hasa vijana wenye vipaji vya soka wameshindwa kuelewa ukweli huo.

Wengi wao bado somo halijawaingia. Ndio maana unaweza kushangazwa na mambo wanayofanya baadhi ya nyota. Nyota ambao kwa kuviangalia vipaji vyao na bahati wanazozipata, unaweza kuwabashiria watafika mbali katika muda mfupi, lakini wapi!

Achana na Mbwana Samatta au Simon Msuva na wengineo ambao walipopata nafasi ya kutoka nje ya nchi, wametumia vyema na kuzifungua akili zao. Kuonja kwao utamu wa kucheza nje ya nchi kumewafanya wasitamani kurudi nyuma. Hawafikirii kurudi Tanzania. Hakuna ubishi hata kina Samatta, tunajua kuna siku watarudi nyumbani. Lakini ni kipindi hicho watakuwa wamemaliza kile walichokifuata huko nje. Ni kama walivyowahi kufanya Danny Mrwanda, Henry Joseph ama Abdi Kassim ‘Babi’.

Ila bado kuna tatizo la wachezaji wengi. Wasiojua thamani ya miguu yao. Hawajui kama miguu na vipaji walivyonavyo ni dhahabu kama si almasi wanaotembea nazo, zinazoweza kuwatajirisha na kuwatoa kwenye lindi la umaskini!

Hawa ni wale wanaoenda kucheza soka la kulipwa, kisha ghafla wanarudi na visingizio kibao. Huwa unajiuliza iweje kina Samatta wameweza na wapo wanashindwaje?!

Ni kama hawajui thamani ya miguu yao na pengine wanachukulia poa. Mtu wa Mashabiki, nataka kuwatonya wachezaji wenye vipaji vyao. Wajiongeze. Wawaangalie kina Meddie Kagere, Chris Mugalu, David Molinga na mastaa wengine wa kigeni wanavyokomaa nchini.

Najua kupanga ni kuchagua, simlaumu yeyote wala kumsimanga mtu hasa kwa wale walioamua kurudi nyumbani ili waendelee kuwa wa hapa hapa. Lakini naiangalia fursa wanayoipoteza nje. Kucheza nje kuna raha yake, japo kuna changamoto ya upweke. Kama Samatta, Msuva, Kelvin John, Haji Mnonga na wengine wameimudu. Wao kinawashinda nini?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz