Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MASHABIKI: Nafasi nyingine kwa Simba kuthibitisha ukubwa

Simbaz Nafasi nyingine kwa Simba kuthibitisha ukubwa

Sun, 10 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Vijana wa zamani wanakumbuka majina ziliyopewa klabu za soka nchini. Yanga iliitwa Umoja wa Mataifa. Simba ‘Taifa Kubwa’ na Milambo ‘Taifa Jipya’. Pia kulikuwa na Taifa Teule, Taifa Jeuri na kadhalika.

Jina la Taifa Kubwa lilibeba uhalisia wa Simba kwani imejitofautisha na timu nyingine nchini.

Simba ni taifa kubwa kweli zinapokuja mechi za kimataifa. Huwa inashangaza sana. Hata iwe mbovu kiasi gani katika ligi ya ndani, ikishiriki kimataifa huwa ni kali, hasa ikicheza nyumbani. Ni nadra kuikuta ikipoteza nyumbani. Ni mara chache inafungwa kizembe katika mechi hizo.

Najua kuna watakaohoji mbona ilipigwa hamsa mara mbili mfululizo 2019 na timu za AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri? Kuna watakaosema mbona ililala 4-0 kwa Recreativo do Libolo ya Angola 2013. Pia mwaka jana ilipasuliwa 4-0 na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na mbona ilipigwa nyumbani na Mufulira Wanderers ya Zambia 4-0? Nieleweke mapema, Simba huwa haifungwi kizembe kimataifa. Mwaka 1979 licha ya kipigo cha Wazambia nyumbani ilienda kushinda ugenini 5-0.

Timu gani iliwahi kupindua meza kibabe namna hiyo? Ni kweli ilifungwa 5-0 na AS Vita na Al Ahly, lakini ikiwa ugenini iliporudi nyumbani zote hizo zilichezea kichapo na Simba kutinga robo fainali. Kitendo hicho kilikuwa ni rekodi kwao na kwa timu za Tanzania, kwani tangu Ligi ya Mabingwa ilipobadilishwa kimfumo 1997, hakuna iliyowahi kutinga robo fainali. Yanga ilikuwa ya kwanza kutinga makundi 1998, lakini ilichapika na kumaliza mkiani ikizidiwa na Manning Rangers, Raja Casabalanca na Asec Mimosas kwa kuvuna pointi mbili tu. Simba ilitinga makundi 2003 na kumaliza ya tatu ikiizidi Asec kwa kukusanya pointi 7, ikiwa nyuma ya Enyimba na Ismaily.

2019 ikaandika rekodi mpya ikitinga robo fainali na kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo baada ya suluhu nyumbani na kulala 4-1 ugenini. Mwaka jana ilirudia tena kutinga hatua hiyo baada ya kumaliza kinara wa Kundi A ikiwa ni rekodi, ikiiacha nyuma Al Ahly iliyobeba taji hilo. Japo ilikwama mbele ya Kaizer Chiefs kwa kulazwa 4-0 ugenini na kushinda nyumbani mabao 3-0. Simba imeendeleza maajabu katika michuano ya kimataifa, licha ya kung’olewa Ligi ya Mabingwa kwa faida ya bao la ugenini lililowabeba Jwaneg Galaxy ya Botswana, wanaume wamepambana katika Kombe la Shirikisho na kutinga makundi. Kutinga kwao makundi haikuwa ajabu sana, kwani tayari Yanga ilishaandika rekodi kwa timu za Tanzania katika michuano hiyo tangu ibadilishwe na kuchezwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2004. Ilishatinga 2016 na kurudia tena 2018. Pia hata Namungo ilishatinga hatua hiyo japo ilimaliza kwa aibu kwa kucheza mechi sita bila ushindi wala kufunga bao lolote. Simba sasa inajiandaa kucheza mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Tayari imeandika rekodi nyingine ya kibabe ya kufuzu robo fainali za CAF kwa mara tatu mfululizo ndani ya misimu minne. Hakuna timu ya Tanzania imewahi kufanya hivyo.

Mtu wa Mashabiki nawapa heko Wekundu kwa kazi kubwa na namna ilivyothibitisha kuwa kweli wao ni Taifa Kubwa kwa kuigonga USGN mabao 4-0.

Tayari yameanza maneno ya kejeli kwamba safari ya Mnyama imefikia mwisho kwa Orlando wakirejea kilichoikuta Simba msimu uliopita kwa Kaizer Chiefs. Licha ya baadhi ya wadau kuiponda Simba, lakini ukweli ni kwamba inastahili pongezi, kwani ilichokifanya sio heshima kwao tu, lakini imesaidia kuipeperusha zaidi Tanzania katika anga hilo la kimataifa.

Kuna nchi zilizokuwa zikiitazama Tanzania kama nchi kibonde, ila kwa sasa akili zimewakaa sawa zikijua zinacheza na Simba zinatetemeka. Hata Orlando huenda huko ilipo presha imeanza kuwapanda na wanakuna kichwa kuifikiria Simba.

Licha ya kuwa hii ni mara ya kwanza kwao kukutana bado Wasauzi watatishwa na ubabe wa Simba. Ni wakati wa Wekundu kuitumia kama faida kwa kuiduwaza Orlando kwa kuutumia vyema mchezo wao wa nyumbani kupata matokeo mazuri ili kwenda kumaliza kazi ugenini.

Kwa rekodi za Orlando ni wazi Simba inajua inaenda kukutana na kigogo, lakini silaha yao kubwa ni kuhakikisha inapata ushindi mnono nyumbani ili hata kama itaenda kuanguka ugenini, basi ibebwe na ushindi wa awali na kuandika historia nyingine.

Historia ya kutinga nusu fainali katika michuano ya Shirikisho, baada ya awali kufanya hivyo katika Klabu Bingwa Afrika 1974 na kurudia ilichokifanya 1993 kwa kutinga fainali za Kombe la CAF na kupoteza kwa Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz