Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MTU WA MASHABIKI: Msiposhtuka mapema mtaburuzwa sana!

Shtuka Pic Data Lusajo

Sat, 7 May 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Unapowasikia wanavyokuwa mbele ya vinasa sauti kwa waandishi wa habari wakihojiwa, huwa wanajishaua sana!

Utasikia wakizungumza kwa mbwembwe, kwamba wana ndoto kibao ikiwamo kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Wanatamani sana kucheza Ulaya. Wanatamani kukipiga England. Wanatamani wawe kama Messi au CR7. Pia hawaachi kutaumu kwamba wanabaniwa sana na makocha wao. Baadhi yao huvuka mipaka na kufikia kusema kwamba eti wanapigwa juju. Yaani kwa mtu muelewa anajua zote hizo ni fiksi tupu.

Wanalaumu sana kubaniwa. Nawazungumzia wachezaji wa soka wa Kibongo. Huwa wana mbwembwe sana mdomoni, lakini ukweli miguuni hawana kitu. Ni wachache sana wanaojitambua na wanaovitumia vipaji vyao kwa ufanisi. Sio siri kuna wachezaji wa Kitanzania wamejaliwa vipaji vya hali ya juu katika soka. Wakipewa nafasi wanajua kuuwasha, lakini huwa hawana muendelezo. Wanafunika leo, kesho wanakera. Lakini sasa wasikie wanavyotamba pale wanapotupia nyavuni mara chache katika Ligi Kuu Bara na michuano mingine inayoshiriki timu yao.

Ndio, wale wanaotamba wanataka kucheza soka nje ya nchi. Wanaotamani kufanana na Karim Benzema au Erling Haaland kwa kucheka na nyavu. Wanatamani kukipiga kama Marcelo kama sio Son Heung Min. Nenda sasa kawadekshie uwanjani wanapocheza, ndo utajua jamaa ni fiksi na manjegeka flani hivi. Yaani ni kama watu wanaotamani pepo, lakini wanahofia kufa. Wanasahu kuwa soka ni mchezo wa hadharani, kama unajua na unaupiga mwingi, huna sababu ya kupiga vuvuzela. Watu watakuona tu uwanjani na kujua wewe ni nani na utafika wapi?!

Hata mawakala huwa wanawafuatilia uwanjani na ukiupiga mwingi, mjue kabisa ni rahisi kuja kubebwa na kupelekwa ughaibuni kukipiga. Unabisha nini? Samagol yu wapi? Msuva je? Himid Mao na wengine sio mmewaona walivyopata michongo ya haraka nje ya nchi.

Masakaunti waliwaona na ndiki lao likawabeba na leo wanaendelea kula shavu ughaibuni, hata kama Msuva ameuchuna kwa sasa nyumbani baada ya kuzinguana na Wamorocco? Hawakupiga blabla kujinadi!

Hata hawa kina MK14, Mwamba wa Lusaka, Mzee wa Kutetema, Prince Dube na wengineo, kwani walipiga vuvuzela? Wanene waliuona mziki wao huko walipo wakawavutia wanya na kuwatumia tiketi fasta wakatinga Bongo kukinukisha. Soka la kisasa halitaki blabla. Hizi blabla na kelele pamoja na mipasho ni bora waachiwe kina Mzee Yusuf, Prince Amigo na Mashauzi kwenye taarabu zao!

Mnajua nini? Kuna wachezaji kibao wa Kitanzania wenye vipaji vyao wamekuwa wakiishia kucheza na kumalizia soka lao hapa hapa, lakini ukisikia saundi zao utashangaa. Wana ndoto kubwa, lakini wanashindwa kuzifanikisha.

Wanashindwa kwenda sambamba na wachezaji wa kigeni ambao baadhi yao wanakuja wakiwa wameshazeeka, lakini wanaendelea kukiwasha kama kawaida.

We angalia orodha ya wachana nyavu ndo utajua nazungumza nini...orodha imejaa wageni wenye mabao yao, huku wazawa wakiwa wanaunga unga, ukiwaondoa Reliants Lusajo wa Namungo, George Mpole wa Geita Gold ama Vitalis Mayanga wa Polisi ambaye naya ana masiku kibao hajawaka tena.

Kina Mayele, Kagere na Kola wanatupia, huku wao wanaishia kupiga blabla tu na visingizio kibao, sijui wanabaniwa na makocha... fiksi tupu!

Mtu wa Mashabiki nilitaka kuwakumbusha wazawa, kwamba umefika muda wa kubadilika. Wajiongeze ili wasiendelee kuburuzwa.

Hakuna kocha hasa hawa wanaotoka nje ya nchi kuja kuvuna fedha wanaoweza kuwapiga chini wachezaji wanaompa matokeo uwanjani na kuwabeba wazawa wasio na mzuka wala kujielewa wapo katika soka kufanya nini?

Hivi unadhani Profesa Nabi anaweza kumpiga chini Mayele ili ampe nafasi Ngushi kama haonyeshi maajabu? Hawezi kumpiga chini Saido ili ampishe Yusuf Athuman au Pablo Franco ampige chini Kagere au Chama ili Mhilu au Kibu waliamshe?! Maweee...!

Sio siri naona kuna tatizo mahali, wachezaji wazawa wanajifelisha sana, ila hawajui! Ndo maana nawashtua waamke sasa ili waliamshe dude na kujitengenezea mazingira mazuri ya kupata mashavu nje ya nchi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz