Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Yanga, Simba hili ni lenu

Mashabiki Wa Simba V Yanga Mashabiki wa Simba na Yanga

Sun, 31 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Najua baadhi yenu mtakataa, lakini unajua unakataa unachokijua kuwa ndivyo ilivyo ila tu kujikosha. Ukweli unao ya kwamba utani wa Simba na Yanga uliokuwepo zamani, lakini kwa sasa wawili hao ni mahasimu na maadui wakubwa.

Hali kwa klabu hizo kongwe kuhusu utani na uhusiano wa kiungwana katika soka inazidi kuwa mbaya endapo hakutachukuliwa hatua za makusudi na za haraka kuidhibiti. Ipo siku yatazuka machafuko yatakayohatarisha maisha ya watu na soka lenyewe.

Aliyesema mdharau mwiba mguu huota tende hakukosea na ukilea uovu taratibu utaongezeka na hatimaye utasababisha uharibifu mkubwa utakaogharimu uhai na maisha ya watu.

Simba na Yanga wamekuwa wa ajabu mno. Hawataniani tena, bali wanatengeneza uhasama na uadui kati yao hali ambayo kama haitadhibitiwa mapema inaweza kuzua balaa kwa sababu ya ushabiki na mashabiki wa timu hizo.

Baadhi ya viongozi na mashabiki wa timu hizo wamekuwa wakitengeneza uhasama na uadui kati yao kwa maneno ya kejeli na ya kuudhi wakidhani kufanya hivyo ni ushindi na umaarufu kwao.

Klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikikoleza uhasimu na uadui kwa kuitana majina ya hovyo mfano Makolo, Chura na Utopolo - majina yanayohudhi, kukera, kuchochea hasira na kufanya uhasama na uadui dhidi yao uwe mkubwa.

Imefikia hatua kwa sasa mashabiki wengi wa timu hizo hawaendi viwanjani kama mmojawapo anacheza. Mashabiki wa Simba hawaendi uwanjani kuangalia mechi ya Yanga kadhalika wa Yanga haendi kuangalia mechi ya Simba.

Ikitokea mashabiki wa timu hizo wakaenda uwanjani kuangalia mechi za timu zisizo zao watakuwa na mashaka, hawatakuwa huru uwanjani na wanaweza kufanyiwa vurugu, kushambuliwa na pengine kupigwa na kufukuzwa wanapokuwa wamekaa.

“Nilikwenda Arusha kuangalia mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), nilipoingia uwanjani niliulizwa nimefuata nini hapo uwanjani. Nikaitwa mchawi wa kuwaroga Yanga ili wafungwe,” anasema mmoja wa mashabiki wa soka aliyewahi kuwa kiongozi mkubwa wa klabu ya Simba.

Anaongeza kuwa, “kwa kuwa mimi ni kiongozi, viongozi wa Yanga walinisaidia nikakaa kuangalia mpira. Sikuwa na raha wala amani. Muda wote nilikuwa nikisali kimoyomoyo kuiombea Yanga ishinde maana tofauti na hapo niliona dalili za kushambuliwa na kupigwa.”

Zamani huko na miaka ya zamani kidogo, hali ilikuwa shwari klabu hizo zilikuwa zikitaniana, uhasama na uadui unaotengenezwa na kujengwa leo haukuwepo.

Kwenye mechi ya Simba, mashabiki wa Yanga walikwenda uwanjani kwa wingi kuangalia vivyo hivyo Simba walikwenda kwa wingi kwenye mechi ya Yanga. Mashabiki waliupenda mpira tofauti na sasa wanazipenda timu zao.

Nakumbuka 1993 Simba ilicheza kimataifa na timu ya Manzini kutoka Swaziland katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mashabiki wa Yanga waliingia kwa wingi wakawashangilia wageni, lakini baada ya mechi waliwapongeza Simba kwa ushindi wa mabao 2-0 ambayo yote yalifungwa na Malota Soma. Huo ndio ulikuwa utani wa watani wenye tija.

Leo hii mshabiki wa Simba hawezi kumsifia na kumpongeza mchezaji wa Yanga anayefanya vizuri na wa Yanga naye hathubutu kumsifia au kumpongeza mchezaji wa Simba hata awe mzuri kiasi gani. Akijaribu kufanya hivyo ataitwa majina yote asiyostahili kama msaliti, mamluki na anaweza kutengwa na timu yake.

Uhasama na uadui huo unaletwa na kusababishwa na watu wachache. Kwa mtazamo wa Mpapaso watu wanaopenda sifa na kusifiwa, wanaodhani maneno makali ya kuudhi, kukera, uchonganishi na yanayowatia watu hasira ndiyo huwajenga na kuwainua kuwa maarufu zaidi.

Ifike wakati sasa tabia hizo zikemewe. Wahusika waambiwe wazi kwamba wanachofanya kinatishia amani kwa mashabiki wa mpira wa miguu wa klabu hizo na Watanzania. Wasipo rekebika wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha hali hiyo kabla hawajasababisha maafa.

Kumekuwepo na tabia ambazo si rafiki kwa maendeleo ya mpira. Tabia za kinafiki zaidi. Leo yakizungumzwa maneno ya kejeli, yasiyofaa katika familia ya soka na kiongozi mfano wa Simba mashabiki wa Simba watayafurahia na kuyashabikia eti kwa sababu yanawaumiza Yanga.

Maneno hayohayo yakisemwa na kiongozi wa Yanga mashabiki wake wanashabikia kwa kuwa yanawachoma na kuwaumiza Simba. Hii ni hatari itatuletea vita kwenye mpira wa miguu na kwa pamoja ni vyema tuikemee.

Mpira wa miguu lengo lake hasa ni burudani. Kuwaunganisha watu na kuwafanya wawe wamoja zaidi. Tabia za kutafuta sifa na umaarufu kupitia mpira wa miguu kwa kutoa kauli za kufarakanisha na kuwagawa watu zikemewe na kuachwa kwa ajili ya maendeleo ya soka.

Watanzania wapenda soka na amani ya nchi, mashabiki wa Simba na Yanga msiteteane kishabiki. Yakataeni na yapingeni yale yote yanayolenga kuwagawa na kuwafanya kuwa maadui ili mpira wa miguu uongeze upendo kwa Watanzania usitugawe.

Columnist: Mwanaspoti