Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Tuache ushabiki twenzetuni kwa Mkapa

Kwa Mkapa Simba SC.png Tuache ushabiki twenzetuni kwa Mkapa

Sun, 13 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kabla ya kukitoa nilichokusudia kwa ajili yenu wasomaji leo, nitumie fursa hii kutoa hamasa kwa Watanzania tuiunge mkono Simba katika mchezo wa kimataifa dhidi ya RS Berkane ya Morocco utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliosalia katika mashindano ya kimataifa watashuka uwanjani kukipiga na RS Berkane katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kufuzu robo fainali.

Najua upo ugumu - tena mkubwa tu kuwashawishi Watanzania wote kuisapoti na kuishangilia Simba ili ipate ushindi kutokana na ushabiki wa Simba na Yanga ambao umedumu kuombeana mabaya.

Mashabiki wa Simba na Yanga wametengeneza aina fulani ya ushabiki ambao sioni afya yake katika maendeleo ya soka nchini - ushabiki wa chuki, visasi, uhasama, kubaguana, wenye kusababisha ugomvi, wakati mwingine huchaniana jezi na kurushiana makonde. Hali hiini hatari kwa mafanikio ya mpira wetu wa miguu.

Nnatamani sana kuona upendo, umoja na mshikamano wa Watanzania unaimarika katika soka. Tunapocheza ligi yetu ya ndani tushindane, tupingane, tutaniane katika hali ya kawaida ya mchezo, furaha na burudani vitawale zaidi. Pia timu zetu kadhaa zikiwa katika ushiriki wa mashindano ya kimataifa tuzisapoti, tuzipe ushirikiano ili zifanye vizuri mafanikio yake itakuwa heshima kwa timu husika na Taifa kwa ujumla.

Ujue hakuna familia ambayo wote wanaishabikia timu moja tu - Simba au Yanga. Kaka atakuwa Simba, mdogo wake atakuwa Yanga au wewe ukiwa Yanga, shangazi, mjomba, mtoto wa baba au mama mdogo atakuwa Simba.

Hivyo kutengeneza chuki, uhasama na ugomvi kati ya mashabiki wa timu hizo ni kujaribu kukataana watu wa familia moja.

Kwa msingi huo wa udugu ndio maana nasema kwa sasa Watanzania tuungane, tuisapoti, tuishangilie Simba katika uwakilishi wake wa mashindano ya kimataifa. Tuanze na mchezo wa kesho tuliopo Dar es Salaam na maeneo mengine jirani. Tujitokeze twende uwanjani tukawashangilie, wale wasioweza kufika uwanjani kule waliko waiombee Simba ishinde mchezo huo na kujiwekea matumaini ya kusonga mbele hatua inayofuata.

Simba ni ya Tanzania, nasi ni Watanzania, Wananchi wa Tanzania. Ni vizuri tukawapenda wa kwetu tuwaombee mafanikio kwani tukiwa na matatizo, misiba, sherehe na furaha tunasaidiana. Hao wageni mchezo ukikamilika wanatimkia kwao hatutawaona. Tupende chetu. Mtazamo na maoni yangu hayo ya kuisapoti Simba, japo najua watakaokerwa nayo huo utakuwa ufahamu wao. Pia najua wengine watasema mimi ni shabiki wa Simba ndiyo sababu nahamasisha Watanzania wakaisapoti.

Hao nao ni mtazamo wao. Ni kusameheana tu. Siku moja kwa neema ya Mungu wataelewa na watabadilika.

Baada ya kuuzungumzia uzalendo kwa nchi na timu zetu ndani ya nchi nirudi kwenye hoja yangu ya leo. Mpapaso ukalie kitako, tulizana ubongo ukae mahala pake ili unielewe barabara.

Wiki iliyopita nilieleza maisha yangu binafsi na kujitambulisha kwenu ili mnapopapaswa na mpapaso huu muwe na ufahamu anayekupapasa ni mtu wa aina gani. Naamini hapo tupo sawa.

Mpapaso wa leo ni kama utambulisho hivi, lakini sio halisi utambulisho. Nataka ufahamu mimi ni nani kwa timu zetu pendwa na kongwe za soka Tanzania, Simba na Yanga. Nimekuwa nikipata shida na tabu kubwa kwenye mitandao ya kijamii na mazingira ninayoishi na jamii ya Watanzania wenzangu. Watanzania kama sio wote, basi walio wengi wanaamini Mtanzania yeyote lazima kwenye ushabiki wa soka kama sio Simba, basi ni Yanga.

Yaani hata kama ni kiongozi au mchezaji wa timu fulani eti huko anazuga tu, anasaka tonge, lazima awe na mapenzi ya Simba au Yanga ndivyo wanavyoamini wananchi, Watanzania wa Tanzania.

Inawezekana mawazo yao yakawa kweli, lakini, japo wengi watabisha na kupinga kwamba, wapo ambao sio Simba wala Yanga, ukweli wao utabaki kuwa kweli kwa kuujua ukweli wa kilicho kweli kuhusu Simba na Yanga katika maisha ya kifutiboli.

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu amini kwamba sina ushabiki wa Simba na Yanga. Ndivyo nilivyo na nitaendelea kuwa hivyo, kwani ndivyo nilivyo nazipenda timu zote hizo mbili lakini si mpenzi wala shabiki wa timu yoyote kati ya timu hizo zenye mashabiki wengi Tanzania.

Yanga ikishiriki mashindano ya kimataifa kipindi fulani nikiisifia na kuhamasisha Watanzania kuisapoti nilikuwa nikishambuliwa - tena kwa maneno makali na matusi nadhani na mashabiki wa Simba walisema mimi ni Yanga kwa sababu tu kupitia maneno yangu nilikuwa nikiipongeza, nikiisifia na kuhamasisha Watanzania wenzangu waipende, waisapoti na kuishangilia timu hiyo ilipokuwa ikishiriki na kucheza mechi za kimataifa na timu za nje.

Hata, wakati timu hiyo ya Jangwani ilipopitia wakati mgumu maneno yakawa mengi, viongozi wakashutumiwa, wakasutana na kulaumiana wao kwa wao nilijitokeza kuwatia moyo, kuwaelekeza na kuwasihi wadumu katika umoja na mshikamano watasimama timu yao ni nzuri na itafanya vizuri.

Katika ukurasa wangu wa Facebook (masau bwire), kwa miaka na nyakati tofauti niliwahi kuandika mengi kuhusu Yanga nikiitakia na kuiombea mafanikio - machache kati ya hayo ni andiko langu la Aprili 6, 2018, saa 9.52 jioni lililosema, ‘Kesho ni Yanga Vs Dicha ya Ethiopia, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam’. Nilihamasisha mno Watanzania kuiombea Yanga ishinde mchezo huo. Pia nilihimiza kufika uwanjani kuwashangilia wachezaji, kuwatia moyo na nguvu, ili kupitia wao ushindi upatikane.

Julai 29, 2018, saa 3.16 asubuhi niliandika andiko jingine lililosema, ‘Yanga, uvumilivu na umoja utawafikisha Kanani’.

Siku hiyo walikuwa wakicheza mechi ya kimataifa, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Gor Mahia ya Kenya - timu yetu ya Yanga ikiwa na pointi moja tu na katika kundi lao ikishika mkia.

Yanga tayari walionyesha kukata tamaa, wakashikana uchawi, wakawaona viongozi wao hawafai kuiongoza klabu hiyo na ili kuwatia moyo, kuwaleta pamoja nikaja na hilo andiko nikiwaambia, uvumilivu na umoja utawafikisha Kanani.

Kama wana wa Israeli katika safari ya kutoka utumwani Misri walifika Kanani baada ya dhoruba na changamoto nyingi lakini, walivumilia wakafika salama.Wakati nikiyaandika hayo kuhusu Yanga nilipendwa sana na mashabiki wake, niliungwa kwenye magrupu mengi ya WhatsApp ya mashabiki wa timu hiyo wakaamini mimi ni wao. Wakanipa ushirikiano wote kama mtu wao wa karibu na mwenzao.

Wakati mashabiki wa Yanga wakinipa dole wakiamini ni wa zizi la kwao, mamba katika msafara wa mamba wenye kenge wachache upande wa pili, Simba SC waliniona na kunichukulia hivyo. Kwamba mie ni Yanga. Wapo walionitukana, kunitolea maneno makali yenye kuudhi, kukera na kudhalilisha, huku wengine wakidai najipendekeza ili niajiriwe Yanga!

Leo hii, Simba nalazimika kuipongeza, kuisifia na kuwa sehemu ya hamasa katika mashindano ya kimataifa inayoshiriki, upande wa pili wananitukana, kunikashifu na kuninenea maneno ya kuudhi, kufedhehesha, kudhalilisha na kejeli kwa kuwa eti naisapoti Simba.

Vilevile walivyokuwa wakinishambulia Simba SC wakati nikiisapoti Yanga, ndivyo vivyo hivyo wanavyonishambulia Yanga wakati naisapoti Simba. Yote tuliyoshirikiana huko nyuma yametoweka katika kumbukumbu zao na kusahaulika. Nao (Yanga) wanadai najipendekeza Simba ili niajiriwe bila kujua nina ajira na siko tayari mpaka sasa kuajiriwa popote - ajira niliyonayo ni nzuri na bora kuliko ajira wanazofikiria katika klabu zao.

Hapa napenda nieleweke kwa Watanzania, wadau, wapenzi na mashabiki wote wa mpira wa miguu kwamba sina ushabiki wa Simba na Yanga na sipo popote Simba wala Yanga, ila, kwa nyakati tofauti zinapokuwa katika mashindano ya kimataifa na matukio makubwa ya kitaifa nitazisapoti.

Timu zote mbili, Simba na Yanga niliwahi kuzishabikia kwa nyakati tofauti na kwa mapenzi makubwa, ya dhati kabisa, lakini baadaye niliziacha. Nazipenda, lakini si shabiki wa Simba au Yanga.

Katika safu hii nahitaji kuwa na mtazamo tofauti na wengine. Siyo mchambuzi, bali uhalisia wa kilichopo katika mpira wetu - iwe mafanikio au changamoto. Nimeweka wazi kwamba mimi sio Simba wala Yanga ili isitokee nikausema ukweli fulani ukawa mchungu kwako ukauacha ili utusaidie ukakimbilia kwenye ushabiki wa Simba na Yanga. Tusifike huko, tulia upapaswe upate elimu na ufahamu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz