Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Simba na Yanga sasa igeni kwa Ruvu Shooting

Mpapaso Pic Data MPAPASO WA MASAU BWIRE: Simba na Yanga sasa igeni kwa Ruvu Shooting

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Taifa Stars imeitwa kambini na kocha Kim Poulsen kujiandaa na mechi mbili za kirafiki dhidi ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini. Wote hao watapapaswa kwenye Uwanja wa Mkapa. Wachezaji 21 walioitwa wanacheza ligi ya ndani kutoka timu nane zinazoshiriki Ligi Kuu. Wachezaji saba wanacheza soka nje ya nchi. Wa ligi ya ndani ni kutoka katika timu za Simba SC (7), Young Africans(6), Azam (2), na Namungo FC (2).

Mmoja anatoka Mbeya City (1), Geita Gold (1), KMC (1) na Polisi Tanzania (1). Haiwezekani popote duniani wakachaguliwa wachezaji wote kuwakilisha nchi katika mchezo au mashindano fulani, lazima wateuliwe wachache ambao kwa wakati huo uchezaji wao utaonekana ni bora kuliko wengine.

Hata falsafa ya kocha na aina ya mchezo wanaokwenda kucheza inaamua aina ya kikosi.

Uteuzi wa wachezaji hao hauzingatii anachezea Ruvu Shooting ya Massau Bwire au timu nyingine yoyote.Huzingatia kiwango na ubora wao. Wakati mwingine inawezekana hata wachezaji wakagongana kwa ubora, lakini lazima kocha achague mmoja ndio maana Ruvu Shooting tumekubaliana na uteuzi wa Kim na kuahidi kuendelea kuishangilia kwa nguvu zote timu yetu ya Taifa kwa masilahi mapana ya nchi.

Tuna mastaa kibao wenye viwango vya kucheza mpaka timu kubwa za Ulaya, wote mnaelewa hilo. Lakini inapofika suala la timu ya Taifa ni uzalendo kwanza. Kumekuwepo na kasumba kwa baadhi ya mashabiki wa soka hapa nchini timu ya Taifa inapotangazwa wanachokimbilia ni kuhesabu idadi ya wachezaji kutoka timu yao wanayoishabikia wakilenga wawe wengi zaidi kuliko wachezaji wa timu nyingine. Hii haitusaidii.

Mashabiki wa Simba SC na wale wa mahasimu wao, Young Africans, wamekuwa wakati fulani wachezaji wa timu yao wakiwa wengi kwenye timu ya Taifa, wanajaribu kujifanya kwamba timu hiyo ni yao na hasa inapofanya vizuri. Dah!

Wakati upande mmoja ukifurahia uwepo wa wachezaji wao, upande mwingine huchukia na kuhoji kwa nini timu yao iwe na wachezaji wachache kuliko upande wa pili, hali ambayo husababisha mashabiki kutokuiunga mkono timu ya Taifa lao, wakati fulani kuiombea ifanye vibaya, eti tu, wachezaji wa timu yake wameitwa wachache kujiunga na timu hiyo wakilinganishwa na wale walioitwa kutoka kwa mtani. Kwanini msiige mfano wa uzalendo kama Ruvu Shooting na timu zingine zinazoupiga mwingi kwenye ligi. Kuweni waungwana kwa Taifa, kila mmoja akiwa na takwimu zake na kulalamika mambo hayataenda. Tuache wataalam wa mpira wafanye kazi yao na mipapaso iendelee.

Hiki kikosi kilichoitwa naamini kitampapasa yoyote. Ni aibu kuendelea kukariri majina ya wachezaji tuache miguu iseme. Hii nchi ni yetu sote. Mashabiki wa Simba na Yanga zinazojiita timu kubwa nchini, wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu na ya aibu, kwa kuwazomea wachezaji wa timu ya Taifa ambao wametoka upande mwingine, mbaya zaidi, wakati fulani baadhi ya mashabiki wa moja ya timu hizo, wanawapokea, na kuwashangilia wachezaji wa timu ya Taifa jingine, wakicheza na timu ya Taifa lake, tena akiwa amevalia jezi za timu ya Taifa hilo jingine, huko ni kukosa uzalendo.

Simba SC na Young Africans wangekuwa dira ya maendeleo ya soka katika nchi yetu, ukongwe na ukubwa wao wakautumia kuwaonyesha klabu nyingine changa namna ya ushindani, mchezo wa kiungwana (fair play) na namna ya kushirikiana katika kuisapoti timu ya Taifa.

Viongozi, wanachama na mashabiki wa timu hizo tunatarajia linapokuja suala la timu ya Taifa waungane, wawe kitu kimoja, washirikiane na Watanzania wengine kuhakikisha kwamba timu yetu ya Taifa inafanikiwa. Wachezaji wanapoitwa kujiunga katika timu ya Taifa - wachezaji wa timu yako wakaitwa wachache au wasiitwe kabisa kama ilivyotokea kwetu Ruvu Shooting, kwa wenye kutaka maendeleo ya soka wangejiuliza na kujifunza kwamba ubora wa wachezaji wao umechoka kiasi cha kutomshawishi mwalimu kuwaita katika timu ya Taifa, hivyo kutafuta njia mbadala ya kuboresha ubora wa uchezaji wa wachezaji wao ili kipindi kingine waweze kuitwa kwa ubora na uwezo wao wa kucheza mpira.

Wakati wanatafakari namna ya kuwafanya wachezaji wa timu yao wawe bora zaidi katika kucheza mpira, ili waweze kuitwa kipindi kingine katika timu ya Taifa, waisapoti timu ya Taifa iliyopo hata kama haina mchezaji hata mmoja kutoka katika timu yake au ina wachezaji wachache ikilinganishwa na wachezaji wa timu nyingine, huo ndio uzalendo kwa nchi yako.

Binafsi huwa nashangaa na kusikitika kwa nini ukichukie cha kwenu na kukipenda cha wengine. Hiyo ni roho ngumu na mbaya ambayo, kamwe huwezi kubarikiwa na Mungu na ni vigumu sana mtu wa namna hiyo kufikia mafanikio ya kweli.

Mchezaji wa Tanzania anapochaguliwa kujiunga na timu ya Taifa amechaguliwa kwa sababu yeye ni Mtanzania na hiyo timu ni ya Tanzania, lazima iundwe na Watanzania. Hachaguliwi kwa sababu ni mchezaji wa Simba SC au mchezaji wa Young Africans. Kwa hiyo niombe tufikiri vizuri kuhusu timu ya Taifa na wechezaji wanaochaguliwa, hasa mashabiki wa wakongwe hao katika soka la nchi nchi yetu. Najua siyo mashabiki wote wenye tabia hizi za ajabu zisizofurahisha hata kidogo kuibagua timu ya Taifa letu eti kwa sababu tu wachezaji wa timu yao hawakuitwa au wameitwa wachache. Wapo waungwana - wazalendo ambao linapokuja suala la timu ya Taifa huweka kando timu zao na kuisapoti kikamilifu timu yetu ya Taifa bila kuangalia mchezaji anayecheza anatoka timu ipi kwa wakati huo. Huiweka mbele Tanzania huo ndio uzalendo na dhana ya kuifia nchi.

Ni vizuri Watanzania tukakumbushana wajibu wetu kwa timu zetu tunazozishabikia, lakini wajibu na majukumu yetu kwa timu yetu ya Taifa.

Watanzania tukishikamana tukaungana kwa pamoja, tukaondoa tofauti zetu za Msimbazi na Jangwani tukaisapoti kwa nguvu zote timu yetu ya Taifa, hakika nakuthibitishieni mataifa mengi mno kwenye soka, tutayapapasa vya kutosha.

Ni busara kwa mwenye busara kujifunza na kutafakari yale yote yanayomfikia kwa njia yoyote ile ili akitambua na kufahamu aweze kubadilika badiliko chanya lenye tija kwake binafsi na Taifa kwa ujumla. Hili la Taifa Stars, Usimba na Uyanga linahitaji tafakuri ya kina, ya moyo na ubongo.

Wachache wenye kuchukulia mambo juu juu kabla ya kuelewa, wanaelewa wasichokielewa kwa uelewa wao huo wasiouelewa watakurupuka na kutoa lugha zisizo na staha katika jamii. Hao wapo ni kuwasamehe na kuendelea kuwafundisha taratibu. Ipo siku wataelewa, tutakwenda pamoja. Wapendwa Watanzania wenzangu, mpapaso wa leo, umejikita zaidi kututaka tuwe wamoja zaidi, timu yetu ya Taifa inapocheza, tuungane. Jumatano ijayo Taifa Stars itacheza na Afrika ya Kati katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Machi 29, 2022, katika uwanja huo huo dhidi ya Sudan. Tuache mipapaso iendelee. Jumamosi ijayo nimeandaa uchambuzi mzito hapahapa. Usikubali kuukosa wala kuhadithiwa na yeyote. Utadanganywa.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz