Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Mpira miguu uanzie hapa kwenda juu

Taifa Stars TT Mpira miguu uanzie hapa kwenda juu

Mon, 12 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Moja ya sababu kubwa inayoifanya timu ya Taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa Stars’ isifanye vizuri katika mashindano mbalimbali ni uwepo wa klabu za Simba na Yanga.

Wapo ambao kwao itakuwa vigumu kuielewa na kuikubali hoja hii, lakini ukweli ndio huo. Usimba na Uyanga kama hautatafutiwa tiba kuhusu timu ya Taifa itakuwa vigumu kufikia mafanikio tunayoyataka katika medani ya soka.

Watanzania tunahitaji tuishuhudie timu ya Taifa ikitwaa kombe la ubingwa katika mashindano mbalimbali Afrika, lakini hilo limekuwa gumu mno na wengi wanaamini haiwezekani na haitawezekana kwa kuwa wanaiona ni dhaifu ikilinganishwa na timu za mataifa mengine.

Ukijiuliza ni vigumu kupata majibu kwa nini Taifa lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 50 likose wachezaji 11 tu wa mpira wa miguu wenye uwezo na mahiri wanaoweza kucheza kwa ushindani na kutwaa ubingwa katika mashindano mbalimbali Afrika.

Mpapaso katika papasapapasa ya huku na kule umebaini moja ya sababu inayosababisha timu ya Taifa iendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu - ishindwe kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali Afrika ni klabu hizo mbili - Simba na Yanga.

Zipo sababu kadhaa ambazo zinazifanya Simba na Yanga ziwe kikwazo katika mafanikio ya Taifa Starts, ambazo chache Mpapaso wa leo utazibainisha.

Kwa waungwana, Wazalendo kwa Taifa lao wanapoambiwa jambo fulani linalokwamisha maendeleo ya Taifa hukaa na kujadili kwa pamoja nini kifanyike ili kuondokana na kikwazo ili kuyafikia mafanikio yanayohitajika. Katika hoja ya Jumamosi ya leo kupitia Mpapaso huu natarajia Watanzania tulio wengi tutaungana ili kuondoa vikwazo katika mafanikio ya timu yetu hiyo tuwe na timu bora, imara, yenye viwango itakayocheza kwa ushindani na kutwaa ubingwa wa mashindano mbalimbali ya Afrika.

Katika soka la nchi yetu walio wengi wanaamini kwamba ili mchezaji awe bora, awe na sifa isiyo na shaka kucheza katika timu ya Taifa ni lazima acheze Simba au Yanga. Hivyo hata uundaji wa timu ya Taifa wanaangaliwa kwanza wachezaji katika klabu hizo na kutoka klabu nyingine ni kujazia tu.

Kutoka Simba na Yanga wakati fulani wanachaguliwa wachezaji kuiunda timu ya Taifa ambao kwenye klabu zao hizo hawachezi mara kwa mara. Muda mrefu wanakaa benchi tu, lakini kwa sababu ni wachezaji wa Simba na Yanga. Hiyo tu inatosha kuwapa sifa ya kucheza timu ya Taifa hata kama kwenye klabu zao hizo hawachezi.

Ni ukweli usiopingika kwamba Simba na Yanga zina mashabiki wengi kuliko klabu nyingine yoyote Tanzania mpaka wengine hudai kwamba, Watanzania wote ni mashabiki wa klabu hizo. Kwamba kama siyo Simba, basi ni Yanga, Huko kwingineko ni kutafuta tu tonge watoto waende msalani!

Kuna wakati mashabiki wa Simba na Yanga kila mmoja kwa wakati wake wanaiombea mabaya timu ya Taifa ili ifungwe, watajitahidi wafanye wawezalo kuhakikisha inafungwa na taifa jingine hata kwa Mkapa. Huthubutu kuishangilia timu ya Taifa geni na kuzomea wachezaji wa timu ya taifa lao!

Ikitokea kati ya Simba na Yanga mojawapo ikawa na wachezaji wengi katika timu ya Taifa, wale wenye wachezaji wachache wataichukia. Furaha yao ifungwe na timu ya taifa jingine ili wazomee kwamba klabu, kati ya hizo pendwa iliyokuwa na wachezaji wengi katika timu ya Taifa ndiyo iliyofungwa.

Siku chache zilizopita waliitwa wachezaji 25 kuunda kikosi cha timu ya Taifa kwa ajili ya michezo miwili ya kufuzu Chan dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda. Katika kikosi hicho wachezaji kutoka Simba walikuwa tisa na Yanga sita.

Kutoka Simba walioitwa ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Kibu Denis na Habibu Kyombo, ilhali kutoka Yanga wameitwa Abutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Feisal Salum, Farid Mussa na Salum Abubakar.

Baada ya kikosi hicho kuitwa maneno kutoka kwa mashabiki wa klabu hizo yalianza kusikika. Hawa wa huku wakijisifu wachezaji wao wengi kuitwa timu ya Taifa wa kule wakinung’unika kwa nini wachezaji wao wameitwa wachache kuliko wale wa kule wakati wao ndio mabingwa wa nchi. Mgawanyiko tayari!

Baada ya mchezo wa awali dhidi ya Uganda kumalizika uliochezwa Agosti 28, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uganda wakashinda bao 0-1 mtandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari tulishuhudia mashabiki wakisema na kuandika matokeo hayo kwamba Simba 0-1 Uganda.

Matokeo hayo yalizungumzwa Simba 0-1 Uganda kwa sababu hasa mbili. Mosi, Simba wachezaji wake waliitwa wengi katika timu ya Taifa, pili eti bao walilolifunga Uganda lilipitia kwa mchezaji wa Simba. Hapa umoja wa kitaifa unakosekana.

Kadhalika kama Yanga wachezaji wake wangeitwa wengi katika kikosi hicho maneno yangekuwa hayohayo upande wa pili, hiyo tayari imezoweleka hivyo. Kwa mgawanyiko na tofauti hizo katika taifa ni vigumu timu kufikia mafanikio makubwa bila umoja. Hakuna maendeleo.

Zipo sababu lukuki ambazo zinatokana na Simba na Yanga ambazo kwa namna moja au nyingine zinaweza kusababisha timu ya Taifa, kwa mtazamo wa Mpapaso ishindwe kufanya vizuri na kufanikiwa katika soka la Afrika. Viongozi wa Serikali, TFF na wadau wengine wa mpira Mpapaso unawasihi fanyeni mfanyavyo muondoe Usimba na Uyanga katika timu yetu ya Taifa mtufanye Watanzania wote kuwa wamoja, tuungane na kushikamana kwenye timu ya Taifa. Umoja huo na dhamira ya kweli itatufikisha katika mafanikio mapana.

Lakini pia, ondoeni kasumba na mawazo mabovu miongoni mwa Watanzania kwamba, mchezaji mzuri na bora ni yule aliyesajiliwa Simba au Yanga na ndio wenye uwezo wa kucheza timu ya Taifa.

Ushauri na maoni ya Mpapaso niwaombe wenye mamlaka - TFF na wadau wengine wanaohusika ebu jaribuni mashindano fulani muwaite wachezaji wa timu ya Taifa bila kuwashirikisha wachezaji wa Simba na Yanga muone watafanya nini.

kama wakijumuishwa bado tunafungwa na maneno yanakuwa mengi, wasipokuwepo wao tukafungwa ni sawa tu maana hata wakiwepo tunafungwa na kugawanyika.

Kumbukeni leo Septemba 3, 2022 timu yetu ya Taifa inacheza ugenini, Uganda katika mchezo wa marudiano na timu ya taifa hilo. Mshindi atafuzu fainali za mashindano ya Chan zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Tuungane Watanzania tuwe wamoja. Tuiombee timu ya Taifa ishinde mchezo wa leo iweze kufuzu na kuliletea taifa heshima katika soka la Afrika.

Chini ya makocha wapya Honour Janza, raia wa Zambia ambaye ni kocha mkuu; Mecky Maxime, kocha msaidizi na Juma Kaseja, kocha wa makipa tuamini kwamba kwa mshikamano na umoja wetu itafanya vizuri.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz