Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Mastaa wa kigeni wanawazidi wazawa kwa hili

Simba SC Review Mastaa wa kigeni wanawazidi wazawa kwa hili

Sun, 21 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wachezaji wa mpira wa miguu hasa wa Ligi Kuu ambao ni wazawa wanadaiwa kutojitambua na kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu uwanjani. Baadhi ya wadau wa mpira wa miguu nchini waliuambia Mpapaso kwamba kutojitambua na nidhamu mbovu kwa baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu nchini kumesababisha ubora na viwango vya uchezaji kuporomoka.

Walidai wengi wa wachezaji wazawa wamekuwa wanaopenda starehe, walevi, wasiojithamini na kujiheshimu katika kufanya kazi yao. Pia wadau hao walidai baadhi ya wachezaji wazawa wamekuwa wakiambukizana kuvuta bangi wakidai ni moja ya mbinu ya kuwafanya wacheze kwa nguvu kumbe wanauua taratibu uwezo na ubora wao.

Ikadaiwa wamekuwa wenye tamaa kiasi kwamba wako tayari kuzisaliti timu zao kwa senti kidogo kutoka timu pinzani na kuruhusu wafungwe kucheza kwa makusudi chini ya kiwango. Kwa kutojitambua baadhi ya wechezaji wazawa wamekuwa wavivu wa kufanya mazoezi hawajitumi mpaka wasimamiwe wahimizwe na kusukumwa na makocha wao.

Wengine hata kambini wanatoroka, wakipatiwa mapumziko ya siku mbili hawarudi kwa wakati ni lazima wachelewe sababu za kuchelewa kwao kurudi kambini kuendelea na mazoezi wengi zinakuwa za uongo na visingizio lukuki. Walieleza kwamba wachezaji wengine wakifanikiwa kidogo kupitia uchezaji wanaanza maringo, wanapandisha mabega na hawachezi tena kwa kujituma wakihitaji kubembelezwa. Hiyo inawafanya wavume muda mfupi wa msimu mmoja hadi miwili na kupoteza kabisa uwezo na ubora wao.

Kwa vitendo vya utovu wa nidhamu na kutojitambua kwa baadhi ya wachezaji wazawa miongoni mwa wamiliki, viongozi wa klabu na mashabiki wa soka matakwa yao ni kanuni ziruhusu timu zenye uwezo wa kusajili wachezaji wote wa kigeni zifanye hivyo ili waachane na wachezaji wazawa ambao wanadaiwa mpira wanauona kama sehemu tu ya kupumzika na hawauheshimu kama ajira na kazi kama zilivyo kazi nyingine.

“Binafsi natamani klabu yangu iwe na wachezaji wote wa kigeni. Kama kanuni zingeruhusu ningefanya hivyo, wachezaji wazawa wengi hawako serious na kazi. Ni maduka wanatugharimu na kutufanya tusifikie malengo yetu,” anasema mmoja wa viongozi wa timu ya Ligi Kuu.

Anasema kwamba wanaweza kuiandaa timu vizuri kwa ajili ya ushindi, lakini wachezaji wachache waliokubali kupokea ‘kitu kidogo’ kutoka timu pinzani wakaisaliti, kucheza chini ya kiwango na kuifungisha kwa makusudi, akisema hiyo ipo sana na inaumiza na kusababisha timu nyingi zisifikie malengo.

Wadau hao wanadai kwamba wachezaji wa kigeni hawana ujinga huo na ni vyema kuwasajili kama klabu ina malengo ya kufanya vizuri kuliko wazawa ambao wengi wamegeuka maduka ya biashara.

“Wachezaji wa kigeni watacheza sana tena kwa wingi kwenye ligi yetu. Kwanza gharama zao ni ndogo hawahitaji ada kubwa ya kusaini (signing fee) wala mishahara mikubwa kama wa hapa nyumbani. Ndio maana klabu nyingi nchini kwa sasa zinawatumia kutoka mataifa mbalimbali hususan Nigeria. Wana nidhamu, wanajitambua na kujituma,” anasema kiongozi mwingine wa klabu ya Ligi Kuu.

Anasema gharama za wachezaji wa kigeni ni ndogo. Ni ada ya TFF Sh4,000,000, ada ya kibali cha ajira na makazi ambavyo kwa pamoja havizidi Sh2,000,000, mishahara midogo, wanacheza kwa malengo, wanazisaidia timu na hawapo tayari kwa usaliti.

Baadhi ya viongozi hao wa klabu wanasema siku ya mchezo inapokaribia hupata shida kuwachunga na kuwalinda wachezaji kama watoto ili wasipokee rushwa na kuwasaliti, hali ambayo wanasema kuiepuka ni kuachana nao wakati ukiruhusu na kusajili wageni watupu wasiofanya upuuzi huo.

Mpapaso ulishangaa zaidi pale ulipoambiwa kwamba, hata baadhi ya wachezaji wazawa wa hizo timu pendwa karata hizo pia huzichanga - tena kwa dau kubwa hasa wanapokutana wenyewe. Hivyo nao huwa katika ulinzi mkali.

“Ukiona mchezaji mzuri kila msimu anacheza klabu tofauti mfuatilie tu kwa karibu, utabaini mbali ya kufuata maslahi bora atakuwa na tatizo. Kama siyo duka, basi nidhamu mbovu, bangi sana,” anasema kiongozi mmoja wa klabu.

Lakini pia inaelezwa kwamba wachezaji wengi wazawa wana mapenzi ya Simba na Yanga na kwamba wapo tayari timu wanazochezea zifungwe na timu hizo ili kuzisaidia kutwaa ubingwa. Hiyo nayo ni aina nyingine ya wachezaji wetu kutojitambua. Kutokana na tabia hizo za baadhi ya wachezaji ushindani na ushindi wa kweli unakosekana, hivyo kuwakosesha ushindi na ubingwa waliostahili.

Ifike wakati sasa wachezaji wetu wabadilike, wajitume na wawe waaminifu wakicheza kwa ushindani na wakatae malipo ya aibu yanayowadhalilisha na kuzigharimu klabu zao. Ni aibu ligi yetu kutawaliwa na wachezaji wageni. Siyo kwamba wazawa hawapo au hawana uwezo, eti tu hawajitambui na ni wapiga dili.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz