Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Mapro wa kigeni freshi, ila vigezo vizingatiwe

Phiri Simba Jj Mapro wa kigeni freshi, ila vigezo vizingatiwe

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi Kuu Bara imekuwa na ongezeko kubwa la wachezaji wa kigeni ambao wanaelezwa kuiongezea ushindani na kuifanya iwe bora zaidi.

Pamoja na mijadala mingi mikubwa na mizito iliyowahi kuwepo na inayoendelea miongoni mwa Watanzania kuhusu kanuni inayoruhusu matumizi ya wachezaji wa kigeni katika ligi hiyo, wengi wanadai wachezaji wa kigeni wameiongezea ubora na ushindani.

Watanzania wamekuwa wakitoa maoni tofauti wakiwepo wanaosapoti matumizi ya wachezaji wengi wa kigeni katika ligi, lakini wengine wakipinga idadi kubwa ya wachezaji hao katika timu zinazoshiriki.

Wapo wanaoona sawa kanuni kuruhusu idadi yoyote ya wachezaji wa kigeni kutumiwa na klabu yenye uwezo wa fedha kuwanunua, kuwalipa mishahara na kuwahudumia isajili wachezaji wote wa kigeni kwa madai ya kuipa ligi msisimko, kuiongezea ubora na ushindani.

Wanaopinga kanuni hiyo inayoruhusu matumizi ya wachezaji wengi wanadai itaua uwezo na vipaji vya wachezaji wazawa na kuidhoofisha timu ya Taifa.

Kanuni ya 62 ya Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika kuhusu wachezaji wa kigeni iliruhusu klabu kusajili nyota 12 kutoka sehemu yoyote duniani. Pamoja na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni kuruhusiwa kusajiliwa na klabu kanuni iliweka ukomo wa idadi ya wanaoruhusiwa kuchezeshwa, kuwatumia au kuwemo kwenye orodha ya nyota wa mchezo kwa siku husika wasizidi wanane.

Lakini kanuni pia iliweka aina na sifa za mchezaji wa kigeni atakayeruhusiwa kusajiliwa kwenye Ligi Kuu kuwa ni yule anayecheza timu ya taifa ya nchi yake au Ligi Kuu ya nchi husika.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni kutoka Amerika Kusini na Ulaya watakaosajiliwa kwenye Ligi Kuu Bara lazima wawe wanacheza angalau kuanzia Ligi Daraja la Tatu kitaifa kutegemea na mfumo wa nchi husika.

Mazingatio ya daraja mchezaji analocheza Amerika Kusini na Ulaya kabla ya usajili wake kwenye Ligi Kuu Bara kanuni ilisema ni kwa wakati husika au kipindi kisichozidi miezi sita tangu aachane na timu yake ya mwisho kwa mchezaji aliye huru.

Kanuni pia iliweka ada maalumu ya Sh4 milioni atakazolipiwa mchezaji wa kigeni anayesajiliwa Ligi Kuu Bara kwa msimu, ili usajili wake uthibitishwe na kuruhusiwa kucheza.

Kanuni iliweka masharti ambayo yalizingatia ubora wa mchezaji wa kigeni atakayeruhusiwa kusajiliwa na kucheza katika ligi kuwa awe bora isiwe tu bora mchezaji eti tu kwa kuwa ni wa kigeni.

Kipindi cha nyuma kidogo klabu zilizokuwa zikisajili wachezaji wa kigeni zilikuwa mbili tu - Simba na Yanga tena wachache - wawili au watatu hivi.

Kwa sasa idadi ya klabu zinazosajili na kutumia wachezaji wa kigeni zimeongezeka na hata idadi ya wachezaji wanaosajiliwa imekuwa kubwa. Katika msimu uliomalizika klabu za ligi zilizosajili wachezaji wa kigeni na idadi yao kwenye mabano ilikuwa ni pamoja na Simba (12) na Azam (12).

Nyingine ni Yanga (10), Kagera Sugar (7), Biashara United (6), Coastal Union (6), Namungo (5), KMC (3) na Mbeya City (1).

Utafiti uliofanywa na Mpapaso unaonyesha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022-23 idadi ya klabu zitakazosajili na kutumia wachezaji wa kigeni zimeongezeka. Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji tayari zimethibitisha kufanya usajili wa nyota wa kigeni.

Mpapaso ulifukunyua kutoka kwa baadhi ya viongozi wa baadhi ya klabu zinazosajili na kutumia wachezaji wa kigeni sababu hasa za kusajili ni zipi na wengi wao pamoja na sababu nyingine walidai wachezaji wazawa yaani wa kizazi hiki hawajitambui.

Wanasema wengi wao wameweka mbele maslahi binafsi kiasi cha kukubali kupokea rushwa hata Sh50,000 kutoka klabu pinzani na kuhujumu klabu zao kwa kuzifungisha kwa makusudi.

Hata kujituma na kujitolea (commitment) kwao wakati wa mechi imeshuka kidogo na wengi wao ni wavivu wa mazoezi, walalamishi na wenye kupenda starehe kuliko kuchapa kazi.

Wanaongeza kuwa baadhi ya wachezaji wa Bongo mbali na kuuza mechi, wakifanikiwa kidogo labda kutangazwa kuwa bora huanza kubadilika ghafla, wanapandisha mabega, kuringa kwingi na kutaka kufanya kazi kwa kubembelezwa.

“Ligi imekuwa ngumu yenye ushindani mkubwa ukiwategemea wachezaji wazawa wa Kibongo huwezi kutoboa. Wengi wamekuwa wasanii, rushwa imewatawala, wanafungisha sana makusudi, hawajitumi kabisa bora tutumie gharama kubwa. Tusajili wageni watakaotuletea mafanikio katika klabu yetu,” anasema kiongozi mmoja wa klabu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Anawasifia na kuwaponda wachezaji wazawa kwamba wapo wengi, tena wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka, ila tatizo lao kubwa hawajielewi wala hawajitambui. Ubora wao kwa tabia zao haudumu. Ni muda mfupi tu wanapotea kisoka.

Mpapaso kwa maoni, mtazamo na ushauri wake unaona bado ipo haja ya wadau kuendelea kujadili pamoja ili kuiboresha kanuni inayohusu idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi maboresho ambayo yatakuwa na tija kwa klabu, ligi na taifa kwa ujumla.

Lakini, Mpapaso unashauri matakwa ya kanuni yazingatiwe hasa sifa na aina ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwenye ligi tusikofyekofwe tu hata wasio na ubora tutakuwa tunajidhalilisha wenyewe na ligi pia.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz