Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Hivi mnajua kuna marefa wanaroga hapa bongo!

Uchawi Pic Hivi mnajua kuna marefa wanaroga hapa bongo!

Sun, 17 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Uchawi katika soka imekuwa miongoni mwa changamoto kubwa ambazo kwa mtazamo wangu zinatukwamisha. Ushirikina na uchawi unaaminiwa na baadhi ya klabu kwamba, ndicho chanzo cha mafanikio ya timu, wachezaji na hata waamuzi wa mchezo huo.

Bila kuroga na kurogana baadhi wanaamini huwezi kufanikiwa. Bila ushirikina na uchawi, timu haiwezi kushinda mchezaji hawezi kucheza vizuri na hata mwamuzi hawezi kuchezesha vizuri au kupata fursa ya kutumika katika nafasi hiyo.

Unaweza usinielewe ninapozungumzia waamuzi lakini ndiyo ukweli kwamba hili kundi nalo kwa uchache limeingia kwenye mambo haya ya ushirikina. Nakaa nao huku kwenye mpira naelewa na wao wenyewe wananiambia.

Ni kwamba kuna baadhi ya waamuzi wanaamini kwamba wanarogwa na baadhi ya timu ili watoe uamuzi ambao unaibeba timu husika.

Kwa hiyo mwamuzi anavyoharibu mchezo mpaka kufikia hatua ya kufungiwa baadhi wanaamini ni ushirikina. Na hata wakati mwingine baadhi waliniambia kwamba kuna wenzao wanawaendea kwa waganga ili wapate mechi nyingi na wafanye vizuri zaidi.

Huu ndio mpira wetu, tulia kwenye mpapaso kila Jumamosi nikujuze tunayoyaona huku mitaani. Nieleze japo kwa ufupi kwa tafsiri nyepesi na ya kawaida kuhusu ushirikina na uchawi, ili tupate mwanga na dira kuhusu mambo hayo, tuweze kuona mantiki ya kinachomaanishwa katika mpapaso huu.

Uchawi ni ufundi wa kutumia dawa au maandishi maalumu ya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe. Pia tunaweza kuuita kwa jina la sihiri; ni dawa zinazotumika kurogea, wakati ushirikina ni tabia ya kuamini mambo ya ramli na uchawi.

Katika imani zetu za kidini, naamini kila mmoja, Mkristo na Mwislamu anaamini mambo hayo yapo kwa sababu hata kwenye maandiko yameandikwa.

Pamoja na uwepo wa ushirikina na uchawi na kuthibika uwepo wake kupitia vitabu tunavyoamini ni vya Mungu hatupaswi kuyatumia kama chanzo cha mafanikio yetu, kwa kuwa ni yenye madhara na hayakubaliki popote.

Ushirikina na uchawi hudumaza maendeleo ya jambo lolote lile ambalo utaamua - kwa fikra finyu kulifanya kwa kutumia ushirikina na uchawi kwamba ndiko kutalifanikisha.

Lakini pia katika kuthibitisha kwamba ushirikina na uchawi haufai, hautakiwi na hauna maana kwenye soka kanuni zetu za Ligi Kuu zinadhibiti na kukataza kuwepo kwa vitendo vyovyote vinavyouashiria katika mchezo wowote.

Mara kadhaa tumeshuhudia klabu kadhaa zikiadhibiwa kwa kushiriki vitendo vya kishirikina na uchawi.

Vitendo hivyo vinavyoashiria ushirikina na uchawi ambavyo hufanyika hasa kabla na wakati wa mchezo, tumevishuhudia mara kadhaa vikifanywa hadharani katika michezo na viwanja mbalimbali bila kuangalia, kubagua, udogo na ukubwa wa timu.

Kuna baadhi ya timu ambazo hugoma kabisa wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kupitia mlango wa kawaida, huruka ukuta au kutumia mabavu kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi na kusababisha uharibifu, kwani wengine ili wapite kwa maguvu yao hayo hupitia mlango usio rasmi, huvunja milango na mageti.

Pia huibua ugomvi na wakati mwingine kuumizana kati ya mashabiki na hata viongozi wa timu ngeni na mwenyeji.

Baadhi ya timu hutegeana nani aanze kuzigusa nyasi za uwanja, wengine kuwahi sana kuingia uwanjani hata kabla ya muda wa kikanuni, kwa kuwa tu mganga kawaelekeza wafike mapema uwanjani kabla ya timu pinzani.

Wengine tumewashuhudia wakitumia hata viumbe hai hasa njiwa na paka ambao huingia nao uwanjani na kuwatumia katika harakati za kishirikina na uchawi. Wapo wanaochinja kondoo, mbuzi na hata ng’ombe na kuwafukia viwanjani, wakati fulani inadaiwa viumbe hao hufukiwa wakiwa hai.

Kuna wengine hadharani kabisa, hunyunyiza na kumwaga dawa za kishirikina na uchawi uwanjani. Wapo wanaoelekezwa wachezaji wote kuingia uwanjani kwa mfumo fulani wa kufanana. Wengine huzunguka kibendera kimojawapo cha kona.

Wengine huingia kinyumenyume uwanjani mfano wa mdudu mmoja hivi anayejulikana kwa jina la viringisha mavi, yaani mchezaji wa Ligi Kuu na wa kimataifa anageuka viringisha kwa kutii masharti ya mganga ili timu yake eti ipate ushindi.

Hayo yote cha mtoto, kali na kubwa kuliko ni pale wachezaji wanapoamriwa wakalale makaburini.

Yale makaburi tuliyowafukia ndugu zetu wafu wao wanayageuza vitanda na magodoro ya kulalia katika tu kuusaka ushindi dhidi ya mpinzani kupitia uchawi na ushirikina.

Wengine inasemekana wamekuwa wakifukua maiti kaburini, kuiiba mochwari hospitalini au kukubaliana na walinzi wa mochwari husika na kupewa miili ya marehemu ambayo huifanyia uganga.

Wakati fulani ikidaiwa kufukiwa uwanjani ili tu wapate ushindi.

“Siku hizi imekuwa ngumu kuiba au kupewa maiti na walinzi wa mochwari kwa makubaliano fulani ili wakaitumie kwa kazi ya mpira kufanya uganga ili timu ishinde, baada ya ushindi wairudishe maiti hiyo.

Hata makaburini kuifukua imekuwa ngumu sana - kwa makaburi ya huku kwetu, ulinzi umeimarishwa tofauti na kipindi cha nyuma. Kazi hiyo ilikuwa nyepesi na rahisi mno”, kauli ya mtu mmoja aliyedai ni mganga wa kienyeji akijaribu kunishawishi nimpe kazi ya kuroga timu yangu ipate ushindi kwenye mechi moja ya mkoani.

Wakati fulani, wachezaji wamekuwa wakiogeshwa na kupakwa dawa ya uganga kabla ya mchezo, wanabebeshwa vitu vya ajabu katika miili yao, wanachanjwa chale za ajabu hadi sehemu za faragha za miili yao.

Mchezaji akikataa timu ikafungwa anabebeshwa zigo la lawama kwamba ndiye kafungisha, hivyo wanalazimika kutii.Siku moja rafiki yangu mmoja, kiongozi wa timu fulani ya Ligi Kuu alinisimulia namna mchezaji wa timu yake alivyodhurika na kusababisha timu yake ifungwe kwa kuwa eti alikataa kutekeleza maelekezo ya ‘mtaalamu’.

Mchezaji huyo mshambuliaji wa kigeni, kwa darubini ya mtaalamu ilielezwa ndiye alikuwa nyota na bahati ya ushindi kwa timu yake katika mchezo huo endapo tu atakubali kushika na kucheza akiwa na ‘kidude wezeshi’ cha ushindi huo atakachokabidhiwa na mtaalamu.

Masharti yaliyotolewa na mtaalamu huyo ilikuwa kwamba kama atakataa kidude hicho wezeshi asipangwe kucheza, akicheza lazima ataumia muda mfupi baada ya mchezo kuanza.

Hataweza kuendelea na mchezo, atatolewa nje, itamchukua muda mrefu kupona na kurudi uwanjani kucheza.

Kwa imani yake, mchezaji huyo alikikitaa kidude hicho wezeshi kwa maelezo ya huyo rafiki yangu, mmoja wa viongozi wa timu hiyo.

Ni kweli mchezaji huyo aliumia hakuendelea na mchezo na alikaa nje kwa muda mrefu kidogo bila kuingia uwanjani. Kweli hilo la kutocheza muda mrefu nami nililithibisha, alisota sana na majeraha.

Huwa najiuliza kama kweli uchawi na ushirikina upo kwenye mpira unafanya kazi na kuwezesha ushindi, kuna haja gani ya kuhangaika kusajili wachezaji na makocha kutoka mataifa ya nje, walipwe fedha nyingi kiasi hicho.

Kama ushirikina na uchawi una nafasi katika ushindi wa timu zetu kwa nini tusiachane na wachezaji na makocha hao wa kigeni, tukawatumia vijana wetu wazawa tukabusti uwezo wao kwa hizo ‘power bank’ za asili.

Inafika wakati tunawaaminisha wachezaji kwamba bila ushirikina na uchawi matokeo chanya sio rahisi kupatikana, hivyo wakiwa uwanjani wanakosa nguvu ya kujituma wakiamini sangoma yupo ataleta ushindi.

Kwa wachezaji wasiojitambua, wenye kuamini uchawi na ushirikina kwamba ni chanzo cha ushindi wa michezo yao wanaweza wasifanye mazoezi kwa nguvu wakiamini kwa vyovyote watashinda tu - mtaalam yupo, ushindi lazima upatikane.

Lakini pia, siku akikosekana mtaalamu wakajua kwamba wako kavukavu, uwezo wao tu utawapatia ushindi kwa imani waliyojijengea na kuizoea, wataamini hakuna ushindi wakuwezesha ushindi - mtaalamu hakufanya kazi yake.

Ni aibu na fedheha kubwa kuamini, kukumbatia na kutumia ushirikina na uchawi katika mpira wa miguu tukiamini kwamba kupitia huko tutafanikiwa.

Wanapiga pesa bila jasho rohoni wakijua wanakula vya wajinga. Wajinga ndio waliwao na wanaliwa kweli.

Nimegusia tu kwa ufupi namna baadhi ya klabu zetu za Ligi Kuu zinavyojidhalilisha na kuidhalilisha ligi kwa kushiriki vitendo vya kishirikina na uchawi.

Changamoto hiyo ni kubwa imegusa maeneo mengi. Jumamosi ijayo, nitachambua kiundani ushirikina na uchawi ulivyowaathiri wachezaji mmoja mmoja na ikibidi mifano nitatoa. Ni hatari, usikose Jumamosi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz