Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Hili la waamuzi dawa yake ni hii

Refa Hili la waamuzi dawa yake ni hii

Mon, 29 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa klabu na mashabiki wakiwalalamikia baadhi ya waamuzi wa mpira wa miguu katika Ligi Kuu Bara msimu huu wakidai wanachezesha kwa upendeleo.

Viongozi na mashabiki hao wanadai waamuzi walioaminiwa kuzitafsiri sheria za soka kwa haki na usawa uwanjani wamekuwa wakizikandamiza klabu zao na kuzipendelea timu pinzani wakati wa michezo.

Katika madai yao wanasema waamuzi hao kwa makusudi wanatoa uamuzi unaolenga klabu zao zifungwe na timu nyingine. Pia wanadai kwamba waamuzi hupewa maelekezo ili wazipendelee klabu pinzani na kuzikandamiza zao kwa kulazimisha kupindisha sheria ili zifungwe.

Malalamiko hayo yamekuja ikiwa nd’o mwanzo tu wa ligi katika mzunguko wa pili, hali ambayo inaweza kuitia doa ligi ambayo imesifika kwa ubora hata kwa mataifa ya nje.

Mpapaso katika kuweka sawa mambo, Jumamosi ya leo ukaona ni vyema tushirikishane wadau ili soka letu liendelee kuwa bora na burudani kwa wote.

Mpapaso haupingi wala kukubaliana moja kwa moja na madai au malalamiko hayo ya viongozi wa baadhi ya klabu na mashabiki kuhusu uwepo wa upendeleo wa waamuzi katika uamuzi wao wanaokandamiza klabu zao.

Malalamiko hayakosekani popote. Siyo tu katika soka hata kwenye sekta nyingine. Ila inategemea ni malalamiko gani na yanatolewa katika sura gani.

Inawezekana kinacholalamikiwa kikawa na ukweli kwa kiasi fulani, lakini njia zinazotumika kuwasilisha ujumbe sehemu husika ili kutafuta namna ya kuondoa tatizo ziko katika mtazamo upi. Zina lengo hilo kweli au tu kuleta uchochezi, uadui, chuki na uhasama?

Waamuzi nao ni binadamu. Wana utashi na upungufu wao. Inawezekana katika hali hiyo ya kibinadamu wakajikuta wamefanya ama kwa kudhamiria au isivyo tu bahati (bahati mbaya) makosa hayo ya kimaamuzi. Viongozi na mashabiki wa klabu pamoja wadau wa soka nchini tunapaswa kuwakumbusha waamuzi kuzingatia sheria na kuongeza umakini katika kuzitafsiri.

Mpapaso unajua wadau pia wanajua namna klabu zinavyotumia fedha nyingi kujiandaa kwa ajili ya kufanya vizuri na ikitokea upungufu wa uamuzi wa waamuzi ukamkosesha ushindi aliyestahili inauma na inaumiza.

Ni kweli inapobainika kwamba mwamuzi amevurunda huadhibiwa, lakini adhabu yake haibadili chochote kwenye matokeo. Matokeo yatabaki vivyo hivyo klabu itaendelea kuumia kwa uamuzi mbaya wa mwamuzi husika.

Waamuzi kama wapo wanaofanya kwa makusudi kuzionea baadhi ya timu na kuzipendelea zingine Mpapaso unawasihi waache. Mchezo huo ni mbaya na hauna afya katika maendeleo ya soka nchini.

Mwamuzi akichezesha kwa upendeleo ikionekana na kuthibitika hivyo, italeta mijadala mingi hasi kwenye ligi ambayo tayari ubora wake umeonekana mpaka nje ya mipaka ya nchi yetu.

Itawafanya viongozi wa TFF na TPLB waonekane hawafai pengine kufikia kuingizwa kwenye shida wasiohusika na kuonekana ndio kweli wanatoa maelekezo kwa waamuzi kupendelea na kukandamiza baadhi ya klabu.

Uamuzi wowote mbovu mbali ya kuipunguzia ligi ubora, ushindani na msisimko utasababisha tumpate mshindi na bingwa ambaye hakustahili.

Pia uamuzi usiozingatia matakwa ya sheria utasababisha chuki, uhasama na uadui kati ya klabu na waamuzi, klabu na TFF pamoja na TPLB hasa kwa watu wanaodhani na kudai vyombo hivyo ndivyo vinavyotoa maelezo kwa waamuzi kufanya upendeleo kwa baadhi ya klabu.

Mpapaso unawaomba viongozi wa klabu pale wanapoona hawakutendewa haki katika uamuzi wafuate mifumo ya malalamiko na kimashtaka iliyowekwa kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza na kuendesha ligi.

Kulaumu hadharani kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni kusababisha taharuki, chuki, uhasama na kutoelewana miongoni mwa wadau wa mpira wa miguu.

Viongozi wa TFF na TPLB wamefanya kwa sehemu yao katika kuifanya ligi iwe bora, lakini na wao ni binadamu. Wana upungufu wao. Tunapobaini upungufu wao tuuseme kwa kufuata taratibu zilizopo za kikanuni ili tuwasaidie kuujua na kujirekebisha. Waupokee upungufu wao na wakubali kubadilika.

Wadau wa mpira wa miguu na Watanzania wote ifike wakati sasa tuutumie mpira wa miguu kama kiunganishi cha kutuweka pamoja tushikamane na tushirikiane.

Mpira wa miguu iwe sehemu ya burudani na umoja wetu. Mapenzi na ushabiki katika klabu fulani visitufanye tuwe maadui na mashabiki wa timu nyingine. Tukosoane pale inapobidi kwa upole na upendo kwa lengo hasa la kujenga. Kamwe tusigombane.

Kila mdau wa mpira wa miguu nchini afanye sehemu yake kwa kuzingatia sheria na kanuni. Kwa kufanya hivyo soka letu litazidi kuwa bora. Tutatangazika kimataifa zaidi. Tusibaguane, tuungane na tuwe wamoja.

Ni wazi kwamba, kila timu inapokuwa uwanjani inacheza mpira, laki nje ya uwanja kunakuwa na mambo ambayo hayapaswi kuufanya mchezo unaochezwa uwanjani - watu wakitoka jasho kwa ajili ya timu zao mwisho wa siku ije kuonekana kwamba hakukuwa na maana yoyote kwa jasho la wachezaji.

Columnist: Mwanaspoti