Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Hii Ruvu wala msiichukulie poa

Ruvu Shootring Hii Ruvu wala msiichukulie poa

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Pamoja na kujitokeza kwa changamoto kadhaa ikiwemo ya wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza kuondoka kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi, timu yetu ya Ruvu Shooting Star Co Ltd, inazidi kuimarika na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Ligi Kuu Bara inayoendelea.

Leo, katika safu hii ya Mpapaso, nimeona niitumie kuzungumza na Watanzania, wadau wa mpira, hasa wapenzi na mashabiki wa Ruvu Shooting kuhusu timu yetu hii na mwenendo wake katika Ligi Kuu, kuwaondoa hofu na shaka, kwamba, timu huenda ikashuka daraja. Niwahakikishie, timu imerejea kwenye ubora, wazo la kushuka lipotee kabisa katika mawazo yenu, kwa sasa siyo tu kupapasa, tunampapasa mtu na kumfukunyua, hakuna atakayesalimika, wote ni kupapaswa na kufukunyuliwa hadi majumbani mwao. Kazi imeanza, itaendelea vivyo hivyo, tutamaliza salama.

Katikati ya ligi, timu haikufanya vizuri baada ya changamoto hiyo, ya kuondoka wachezaji hao, timu ilifanya vibaya katika michezo kadhaa na kuleta minong’ono kwa baadhi ya Watanzania, wapenzi, wadau na mashabiki wake, wanaoipenda na kuifuatilia kwa ukaribu sana, kwamba, huenda ikashuka daraja msimu huu wa mwaka 2021/22.

Nakiri kwamba, msimu huu, timu imepitia changamoto nyingi na ngumu, wengine naamini wasingeweza kusimama, kwani, wakati uongozi na benchi la ufundi tukijipanga kusajili wachezaji kupitia dirisha dogo, kujaza nafasi na kuziba mapengo ya wachezaji hao 11, ghafla mchezaji mahiri, beki wa kutumainiwa, Ally Mtoni ‘Sonso’ alifariki na kuongeza majonzi na machungu ndani ya kikosi kizima cha timu yetu hii pendwa.

Ngumu zaidi ilikuwa mchezo dhidi ya Simba SC, tukiwa bado tuko kwenye majonzi na maombolezo ya kifo cha Sonso, siku mbili tu baada ya kumzika ratiba ilitulazimisha kucheza mchezo huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuupoteza kwa kufungwa magoli mengi 0-7.

Simba SC haikuwa bora na uwezo kiasi hicho kuifunga timu nzuri na yenye ushindani wa kweli Ruvu Shooting (Barcelona ya Bongo) bali, ilipata ushindi huo kwa sababu ilicheza na wafiwa, waliokuwa katika majonzi, mawazo yao yakawa tu kumuwaza mchezaji mwenzao aliyefariki ghafla, Simba SC wakakosa huruma, kupitia shida hiyo wakatutungua magoli mengi, hawapaswi kujivuna sana kuhusu ushindi huo kwani, walicheza na timu ambayo haikuwepo mchezoni, walicheza na wafiwa wasio na nguvu, tunawasubiri kwa hamu sana katika mchezo wa mzunguko wa pili, ili tuheshimiane.

Baada ya mchezo huo, na matokeo yake timu nyingine nazo zikatuchukulia poa, wakadhani kweli sisi ni wabovu kiasi hicho, wakatubadili na majina, wakatukejeli sana, wengine wakatuita ‘Wazee wa saba bila’, wapo waliotuita kwa jina la soda - ‘7up’, hata walipokwenda dukani kununua soda hiyo, hawakutamka jina la soda yenyewe, eti waliomba muuzaji awapatie Masau Bwire baridiiiiii, wakimaanisha soda hiyo ya 7up, hatukuwa na raha, barabarani walipoliona gari letu, tuliitwa Wazee wa Saba Bila, walitukebehi na kutukejeli sana!

Mechi iliyofuata baada ya hiyo ya Simba SC, ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons, Sokoine, Mbeya, mashemeji zangu hao, pamoja na uchovu wao, eti nao wakatuona sisi wachovu, kipimo chao kuhusu uchovu wetu, zile goli saba za Simba, wakatubeza sana, uwanjani, pale Sokoine, Mbeya, kabla na wakati wa mchezo, mashabiki wao wakawa wanahanikiza kwa kuimba wimbo wa msanii mmoja nchini uliovuma enzi hizo, wimbo wa saba bila!

Wimbo huo wa saba bila, kadiri muda ulivyosonga, ndivyo sauti zilivyozidi kupungua, baadaye kupotea kabisa, kwani, walipigiwa mpira ambao hawakuutarajia, walitafutana na kupishana uwanjani mithili ya watalii waliopoteana wakielekea katika kilele cha mlima mrefu, Kilimanjaro, walipigishwa kwata la Kihispania, ambalo liliwashinda kucheza, walichoka, buti zikawashinda kunyanyua, tukawapapasa na kuwafukunyua kirahisi mno, tena kwa staili iliyotustarehesha, hawakuthubutu tena kutuita au kuimba wimbo wa saba bila!

Wagosi wa Kaya, Coastal Union, wakijivunia ushindi wa ugenini dhidi ya KMC FC wa magoli 2-3, nao wakaanza dharau, kejeli na kebehi kwa timu yetu, yale yale ya saba bila, ikatawala vinywa vyao, baadhi ya mashabiki wao, siku ya mchezo pale Mkwakwani, nyumbani kwao, wakakosa uungwana, wakamtukana sana Mwalimu wetu Charles Mkwasa, wakatutukana viongozi na hata wachezaji. Wazalendo sisi tulipiga kimya tu, tukisubiri tuwajibu uwanjani kwa vitendo, nyie, acha kabisa, baada ya mechi, njiani tukipita, waliokuwa wanatuita Wazee wa Saba Bila, sasa wakatuita kwa heshima, tena wakipunga na mikono, wakituita, Wazee wa Kupapasa, Barcelona ya Bongo, yaani bila unafiki na wanafiki, raha ya soka haijakamilika, heshima ilikuja, baada ya kuwaaibisha kwa mipapaso na mifukunyuo ya magoli 1-3.

Lengo letu katika mchezo dhidi ya Coastal Union, tuwatoboe saba, ili badala ya kutuita sisi wazee wa saba bila, wajiite wao, na wajue, sisi ni zaidi yao, tumewazidi mbali kisoka, ila, nguvu fulani hivi ikawaepusha na kipigo hicho tulichokidhamiria.

Unajua, wakati wachezaji wetu wakipasha, beki Paul Ngalema aliumia, mwalimu akapangua kikosi alichokipanga kuanza, akamtoa Ngalema, mbadala wake akamuingiza Eradius Mfulebe, ambaye naye, akiwa kwenye kupasha, aliumia, hapakua na beki mwingine wa ziada, ikabidi mshambuliaji, Abdulrahman Musa apangwe kucheza beki, uliona wapi tukio kama hilo, wachezaji wawili, namba moja, wanahumia kabla ya mchezo, wakati wakipasha tu!

Pamoja na changamoto hiyo, Coastal Union, walipwaya, tuliwalegeza, tukawapapasa na kuwafukunyua tulivyotaka sisi, dakika 90, wakatoka uwanjani kwao Mkwakwani, wametota na kuchoka sana, furaha yetu, pamoja na ushindi, ni heshima na matokeo tunayoyapata kuwalazimisha wapinzani wetu kutuheshimu, na kuondoa dhana ya saba bila, wakiamini sisi ni bora, tunao uwezo mkubwa wa kucheza mpira.

Ruvu Shooting hatukubaliani sana na dhana ya kila mtu ashinde nyumbani kwake, kushinda tu nyumbani, ni kukosa uwezo na ubora, ukiwa bora zaidi kuliko mpinzani wako, utamshinda popote, sisi ni bora, tutaendelea kushinda popote, unyumbani wako hautakupatia ushindi dhidi ya aliyebora kukuzidi, kama tulivyofanya kwa Tanzania Prisons pale Sokoine, Mkwakwani dhidi ya Coastal Union, ndivyo tutakavyofanya kwa hao wanaofuata, huko huko majumbani kwao, wajiandae, tunakuja kuwapapasa.

Kwa sasa, tunazatazama kipekee, kwa uzito na umuhimu mkubwa, mechi nne zinazofuata, mechi ambazo zitatuinua na kutuheshimisha sana katika soka ndani na nje ya nchi, katika mechi hizo, makusudio yetu ni kuvuna pointi 12, yaani kushinda mechi hizo zote.

Katika mechi hizo nne, mechi ya awali itakuwa dhidi ya Polisi Tanzania, Ushirika-Moshi, Namungo FC, Ilulu-Lindi, Young Africans, kwenye uwanja tutakaoutangaza hivi karibuni, na Simba SC, Benjamin Mkapa-Dar es Salaam, mechi hizi zitatuheshimisha na kutufanya tuishi mjini kama wafalme, mpapaso wake tunalenga usiwe wa kawaida, umlazimishe Spika wa Bunge letu, atuite Dodoma, wabunge watuone na kutushangilia kwa kazi nzuri.

Ruvu Shooting, kwa sasa ni timu kubwa, inatambulika kila kona ya Tanzania, baadhi ya mataifa Afrika na Ulaya, wanaijua na kuifuatilia, kwa hiyo, lazima tufanye mambo makubwa yanayoendana na ukubwa wetu.

Katika uchunguzi na tathimini ndogo ya kitaalamu tuliyoifanya, kwa ukubwa ndani ya nchi, timu yetu inashika nafasi ya nne, baada ya Simba SC, Young Africans, na Azam FC.

Ruvu Shooting, tumefungua matawi ya mashabiki wetu maeneo tofauti katika mikoa sita Tanzania Bara, ambayo ni Pwani, Mtwara, Lindi, Mwanza, Morogoro na Mara, maeneo ya mikoa mingine wametupatia mwaliko kwenda kufungua matawi ya mashabiki wetu huko ikiwemo wilaya ya Mbinga-Ruvuma kupitia kwa mkuu wake wa wilaya, Bi Aziza Mangasongo.

Lakini pia, tumekuwa tukipokea simu kutoka mataifa mbalimbali, raia wa huko wakiomba kuja kufanya kazi pamoja nasi, aidha kufundisha (kocha) au kucheza (mchezaji), miongoni mwa mataifa hayo ni Ufaransa, England, Afrika Kusini, Rwanda, Burundi, Kongo, Kenya na Uganda.

Kipindi wachezaji wetu 11 walipoondoka kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi, tulipokea simu kutoka Uingereza, wakiomba watuletee wachezaji sita kutoka Nigeria kwa gharama zao ili kuisaidia timu iweze kufanya vizuri, sera yetu, haikuruhusu hayo kufanyika.

Kwa uwekezaji tulioufanya kwenye hii timu, na namna ilivyojitangaza ndani na nje ya nchi, itakuwa aibu na fedheha kubwa, timu hii kushuka daraja, tutapambana kwa uwezo wetu wote, kuhakikisha tunamaliza ligi tukiwa katika nafasi bora kabisa, kwa mfumo wetu huu wa PTK +Fukunyua, ondoeni shaka, tutapapasa, tutatingisha, tutakung’uta na kufukunyua kwa sana, tuko salama.

Columnist: Mwanaspoti