Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Baada ya haya, Ligi ijayo iwe hivi..

Rais Karia Rais wa TFF, Wallace Karia

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mpapaso kwa mara nyingine naangazia changamoto kadhaa katika msimu wa Ligi Kuu Bara 2021 ambao umemalizika ambazo zinahitaji marekebisho ili kuifanya iwe bora zaidi.

Ratiba ngumu ya mbanano kwa mtazamo wa Mpapaso ilikuwa moja ya changamoto katika Ligi Kuu Bara iliyosababisha baadhi ya klabu kushindwa kufanya vizuri baadhi ya mechi kutokana na uchovu.

Kama mnakumbuka huko nyuma mechi za Ligi Kuu Bara zilikuwa zikichezwa siku za mwisho wa juma - Jumapili na Jumamosi ili kuwapa wachezaji nafasi nzuri ya kupumzika kabla ya mchezo unaofuata.

Mfumo na ratiba hiyo ya mechi za ligi kuchezwa Jumapili na Jumamosi ulionekana mzuri na bora kwa wacheza na klabu kwa ujumla kwani, mbali na kutoa nafasi ya wachezaji kupumzika, klabu zilipata muda wa kujiandaa, kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita na ushindani ulikuwa mkubwa.

Kama walivyosema wahenga, hakuna zuri lisilo na kasoro, kama ambavyo barabara ndefu haikosi kona, baadhi ya wadau wa soka nchini waliukosoa mfumo huo wa ratiba, mechi kuchezwa Jumapili na Jumamosi pekee, wakadai inachelewesha ligi kumalizika.

Kamati husika za TFF, TPLB kupitia vikao vyao, waliketi kuchakata hoja hiyo ya wadau, kwa wakati huo, ilionekana kuwa na mashiko, ikapitishwa ligi kuchezwa siku za mwisho wa juma, lakini pia, siku za kawaida.

Hoja kubwa iliyolibeba hilo, mechi kuchezwa na siku za kawaida badala ya Jumapili na Jumamosi tu ilikuwa, nafasi ya kupumzika kwa wachezaji, muda uliotajwa wa kupumzika kabla ya mchezo mwingine ni saa 72, lilizingatiwa hilo, mambo yakabadilika, mechi zikapangwa kuchezwa wikiendi na siku za kawaida ili ligi imalizike mapema.

Baada ya mabadiliko hayo ya ratiba, klabu sasa iliweza kucheza mchezo wake siku ya Jumamosi, ikapangiwa tena kucheze mchezo mwingine siku ya Jumatano, saa 72 za kupumzika kimahesabu zilipatikana.

Nadhani wakati uamuzi huo unapitishwa kucheza mechi wikiendi na siku za kawaida mazingira hayakuangaliwa vizuri yale ya namna ya baadhi ya klabu zitakavyoweza kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kuwahi mchezo unaofuata.

Klabu nyingi za Ligi Kuu zinatumia usafiri wa barabara na magari madogo aina ya Toyota Coaster ili ziwahi mchezo unaofuata wakati fulani zililazimika kusafiri mara tu baada ya mechi iliyochezwa kumalizika.

Ni kweli saa 72 kati ya mchezo na mchezo zilipatikana, lakini klabu zilikosa muda wa mazoezi, marekebisho na maandalizi kwa ajili ya mchezo uliofuata kwani saa hizo 72 ziliishia njiani. Katika mazingira hayo ya kucheza mechi katikati ya wiki, yaliyozilazimisha baadhi ya klabu kusafiri mara tu baada ya mechi kumalizika ili kuwahi mechi inayofuata, wachezaji walicheza wakiwa wamechoka sana na kusababisha kucheza chini ya viwango vyao. Benchi la ufundi pia liliathirika pakubwa kwa sababu baadhi ya mechi hawakupata muda kabisa wa kufanya mazoezi, kurekebisha upungufu uliojionyesha katika mchezo uliochezwa kabla ya ule utakaochezwa hali ambayo ilipunguza ubora na ufanisi wa wachezaji, klabu na ligi kwa ujumla.

Mifano michezo michache iliyoshuhudiwa na Mpapaso ambayo klabu hazikupata muda wa kupumzika baada ya mechi timu ilisafiri kuwahi mechi iliyofuata, ikafika siku moja kabla ya mechi na kushindwa kufanya mazoezi kujiandaa na mechi hiyo ni pamoja na mechi ya Simba SC dhidi ya Ruvu Shooting FC iliyochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 7, 2022.

Kabla ya mchezo huo, Ruvu Shooting FC ilicheza dhidi ya Yanga SC, Mei 4, 2022 katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, ilisafiri kwa njia ya barabara ilifika Dar es Salaam Mei 6. Kesho yake ilicheza mchezo huo dhidi ya Simba bila mazoezi wachezaji wakiwa na mchoko (fatigue) wa kutisha matokeo ikafungwa mabao 4-1.

Mchezo mwingine ulikuwa ni kati ya Ruvu Shooting FC dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mabatini, Mei 24, 2022. Ruvu Shooting kabla ya mchezo huo, Mei 21, 2022 kuanzia saa 3.00 usiku ilicheza na Kagera Sugar - mchezo uliomalizika saa 5 usiku. Usiku huohuo timu ilianza safari na kufika Mabatini - Kibaha usiku wa kuamkia Mei 23 ikaingia uwanjani Mei 24 kucheza na Azam ikaambulia sare ya bao 1-1. Saa 72 za kupumzika kwa timu ya Ruvu Shooting FC kabla ya mchezo dhidi ya Azam hazikutimia.

Kagera baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting FC huko Kaitaba ilisafiri usiku huohuo kwenda Songea ambapo ilifika huko Mei 24, 2022 ikacheza dhidi ya Mbeya Kwanza Mei 25, 2022 katika Uwanja wa Majimaji na kuambulia kichapo cha bao 1-0.

Zipo klabu nyingi ambazo ratiba ilizibana kwa kiasi kikubwa na kusababisha kupata matokeo mabaya kutokana kwa sababu ya uchovu wa safari ndefu bila kupumzika.

Mpapaso kwa mtazamo unaishauri Bodi ya Ligi (TPLB) kama itawezekana, ligi ya msimu ujao, 2022, mechi zichezwe wikiendi ili kuwapa mapumziko ya kutosha wachezaji na maandalizi mazuri ya timu kuelekea mchezo unaofuata. Hiyo itaipa ubora zaidi ligi na ushindani utakuwa mkubwa zaidi. Jambo jingine la kufanyiwa marekebisho katika ratiba ya ligi ijayo kama itawezekana ni klabu kucheza ligi za ukanda mmoja mfululizo ili kuzipunguzia gharama. Timu ikienda kwa mfano Mbeya, icheze mechi zote za ukanda huo.

Ligi Kuu Bara ni tegemeo la wadau wengi ndani na nje ya nchi kwamba itaendelea kuwa bora kila msimu kutokana na usimamizi mzuri unaofanywa na TFF, TPLB kwa kushirikiana na wadau wengine.

Kwa kuwa TFF na TPLB zina viongozi wasikivu, washirikishaji, Mpapaso unaamini mawazo na maoni ya wadau wanayoyatoa kwa nia ya kuboresha zaidi, yatajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi chanya kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz