Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Vungi ni balaa zaidi ya Mayele, Phiri

Mayephiri Pic MJUAJI: Vungi ni balaa zaidi ya Mayele, Phiri

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita niliandika kuhusu kauli aliyoitoa kipa wa Simba, Aishi Manula.

Manula alisema: “Tangu nchi hii imeumbwa hajawahi kutokea beki kama Mohammed Hussein wa Simba.” Binafsi niliona kauli hii ilikuwa ni ya kuwavunjia heshima mabeki wengine mahiri walimtangulia Tshabalala ndani ya Simba na timu nyingine.

Kwa kweli nilipokea simu na meseji nyingi sana kutokana na mifano ya mabeki kadhaa niliyoitoa kwa kuwataja baadhi ya wachezaji waliokuwa wakali zaidi ya Tshabalala.

Wengi hususan wakongwe wenzangu walipongeza lakini watoto wa juzi wachache walileta dharau kwa kutetea kauli ya Manula kwa sababu za Usimba na Uyanga.

Baada ya makala yale nimeona kuna umuhimu wa kuanza kuwaelezea ukali wa wachezaji wa zamani ili kuwapa somo hawa vijana ambao hawakuwahi kuwaona wala kuwasikia.

YUNGI MWANANSALI

Binasfi niseme ukweli kwamba huyu mwamba sikuwahi kumuona habari zake nilizisikia nilipoenda kusoma Tabora.

Unaambiwa mwamba alikuwa na nguvu sana.

Sitaki kusema stori zake zilikuwa na ukweli wa kiasi gani, lakini unaambiwa alikuwa na uwezo wa kupiga mashuti ya hatari.

Moja ya stori zinasema Yungi Mwanansali pandikizi ya mtu alikuwa akipiga penalti ya ndani ya dakika 90 katika dakika za mwisho kabisa na laiti kama angefunga basi timu yake ingekuwa bingwa.

Na baada ya penalti hiyo mwamuzi alikuwa analazimika kumaliza mchezo. Ilikuwa ikisubiriwa penalti hiyo tu ili filimbi ya mwisho ipulizwe.

Wachezaji wote 10 wa timu yake wakaenda kujipanga mstari kwa mgeni rasmi tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kombe.

Walikuwa wakiamini Yungi Mwanansali hawezi kukosa penalti na dakika zilikuwa zimeisha kabisa.

Unaambiwa Yungi alijivuta na kuachia kombora la hatari lakini mpira ukagonga mwambo wa juu na kurudi hadi golini kwao na ukaingia na likahesabiwa kuwa ni bao la timu pinzani.

Stori hii inaonyesha wachezaji wa zamani walivyokuwa na nguvu na uwezo mkubwa. Ukibisha shauri yako.

HUYU HAPA SEMBULI

Achana na stori ya Yungi mwamba mwingine aliyesifika kwa mashuti makali na stori nyingi juu yake za kuchana nyavu ni Gibson Sembuli. Jamaa alikuwa mtu kweli, umbile kubwa mrefu na mweusi, makipa walikuwa wakimwogopa kwa mashuti yake makali. Sembuli alisifika sana kwa kuchana nyavu za makipa.

VIPI KUHUSU GAGARINHO?

Hamis Thobias ‘Gaga Gagarinho’ akiwa anaitumikia Simba Sports Club dhidi ya Yanga. Oktoba 20, 1990, Simba ilipata penatli baada ya Rajabu Rashid ‘Double R’ kuushika mpira kwa bahati mbaya. Gaga alienda kupiga penalti, alikuwa akisifika kwa mashuti sana, unaambiwa alipiga shuti lililogonga mwamba na mpira kurudi hadi katikati ya uwanja na kuchukuliwa na wachezaji wa Yanga, Thomas Kipesye aliyeenda kupigilia msumari wa pili kwa Yanga ambayo ilishinda mechi hiyo kwa mabao 3-1.

HESHIMA KWA WAKONGWE

Wakati huu wa fainali za Kombe la Dunia zikiendelea kule Qatar, kuna video ilionekana ikisambaa katika mitandao ya kijamii ikiwaonyesha staa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima akiwa na nyota wa sasa wa taifa hilo, Rodrygo.

Ilionekana Ronaldo de Lima akimwonyesha Rodrygo staili ya kushangilia. Ni kama vile alimwonyesha staili ya kushangilia ya ‘kuku kishingo’ inayotumiwa na Tanzania Prisons.

Kabla ya wawili hao kuachana, Rodrygo aliishika miguu ya Ronaldo de Lima kisha akapangusa mikono yake kwenye miguu yake. Ni kama vile alikuwa akichukua baraka za miguu ya staa huyo wa zamani ambaye alikuwa anajua sana kufunga.

Kalidou Koulibaly katika usajili wa dirisha kubwa wakati alipotoka Napoli ya Italia na kujiunga na Chelsea ya England alikuta jezi namba 26 ikiwa haina mtu.

Hata hivyo, Koulibaly alisita kuichukua jezi hiyo baada ya kuambiwa kuwa ilikuwa ikitumiwa na beki aliyestaafu John Terry.

Mabosi wa Chelsea walimwambia, Terry hakuwa ametoa maagizo yoyote kuhusu jezi hiyo kama istaafishwe au la.

Koulibaly alisema atazungumza kwanza na Terry ili ampatie ruksa kabla ya kuichukua jezi hiyo. Baada ya usajili alienda kwao Senegal na wakati akirudi alimpigia simu Terry lakini beki huyo wa zamani wa Chelsea alishangaa kupigwa simu na Koulibay. Hakuipokea.

Baadaye, Terry alifanya mahojiano na kuambiwa kuwa alipigiwa simu na Koulibaly akakubali, hapo ndipo alipoambiwa kuwa lengo la beki kuwa alikuwa akitaka kumuomba Jezi Namba 26.

Juzi kati iliandikwa habari ya mkongwe wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgoal’ akililamika kwamba staa wa sasa wa Simba, Ousmane Sakho haitendei haki jezi yake Namba 10. Enzi zake Gabriel alikuwa mkali wa mabao alifunga ya kutosha pale Msimbazi.

Itaendelea toleo lijalo.

Columnist: Mwanaspoti