Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Unamjua au ulimsikia Maulid Dilunga ‘Mexico’?

Maulid Pic Unamjua au ulimsikia Maulid Dilunga ‘Mexico’?

Tue, 30 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna stori huwa tunawaambia vijana wa sasa zamani kulikuwa na wachezaji wa kwelikweli.

Mdogo wangu mmoja aliwahi kuniuliza kwa nini kila kitu cha zamani kilikuwa kizuri kuliko cha sasa? Swali lake nimelikumbuka leo wakati naandika makala haya, ya kipaji hiki kilichowahi kutokea Tanzania.

ALISTAHILI MSHAHARA WA ULAYA

Maulid Bakar Dilunga alipata sifa nyingi wakati alipocheza dhidi ya timu ya Ligi ya England, West Bromwich Albion ilipofanya ziara nchini na kucheza dhidi ya Kombaini ya Dar es Salaam.

Siku hiyo, Dilunga alikuwa amevaa jezi namba tisa mgongoni aliwatesa sana na wazungu hao walimkumbuka sana mchezaji huyo kutokana na jinsi alivyokuwa akiwanyanyasa kwa chenga za maudhi na pasi zake za ajabu.

Meneja wa West Bromwich Albion, Ashman alisema Dilunga angekuwa na uwezo wa kufika Ulaya angepata kazi bila ya wasiwasi wowote.

Bosi huyo aliongeza hakuona tofauti kubwa kati yake na wachezaji waliokuwa wakilipwa mshahara wa Pauni 400 (wakati huo ilikuwa sawa na Sh1,600) kwa wiki.

AZUIWA KWENDA ULAYA

Klabu West Bromwich Albion iliyokuwa Ligi Daraja la Pili England ambayo ilikuja nchini 1974 kwa mwaliko wa Yanga ilitaka kuondoka naye, lakini taarifa zinasema Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Said El Maamry alimzuia kuondoka nchini.

El- Maamry alimzuia Dilunga kuondoka kwa sababu ya kutaka aitumikie Stars. Kipindi kile uzalendo kilikuwa kitu kikubwa sana na mwamko wa wachezaji kwenda kucheza Ulaya ulikuwa mdogo. Kilikuwa kitu kigeni kabisa la sivyo, historia ingeandikwa kuwa angekuwa mchezaji wa kwanza kucheza Ligi ya England.

Mbali na kuzuiwa, Dilunga alipewa mwaliko rasmi na maalumu na timu hiyo ya West Bromwich Albion, lakini aliipuuza ofa hiyo.

SAFARI YA MEXICO

Chanzo cha Dilunga kupewa jina la Mexico ni safari ya kwenda katika nchi hiyo mwaka 1973.

Lakini safari hiyo ilianzia kwenye Michezo ya Afrika (All African Games) iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.

TAIFA STARS YA MOTO!

Leo hii ni ajabu kusikia Taifa Stars ikiifunga Ghana au taifa lolote la Afrika Magharibi, lakini zamani kilikuwa ni kitu cha kawaida sana.

Taifa Stars ilifika nusu fainali ya michezo ya All Africans Games kwanza ilitoka sare ya kutofungana na kikosi cha kwanza cha Nigeria. Ikakichapa kikosi cha pili cha Nigeria mabao 2-1. Stars ikazifunga Ghana na Togo bao 1-0 kila moja. Ikatoka sare ya bao 1-1 na Misri kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Algeria.

DILUNGA KINARA WA MABAO

Dilunga ndiye aliyeibuka mchezaji nyota wa Stars katika michezo hiyo baada ya kuifungia mabao yote katika kila mechi.

Licha ya Stars kutolewa hatua ya nusu fainali, Dilunga na kipa Omari Mahadhi ‘Bin Jabir’ waliteuliwa kwenye kikosi cha kombani ya Afrika.

Mara baada ya uteuzi huo, kikosi hicho kilifanya ziara katika mabara ya Ulaya na Amerika na kucheza mechi kadhaa za kirafiki. Baadhi ya mataifa hayo ni Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru, Hungary na Bulgaria.

Katika ziara hiyo, kikosi hicho cha Afrika kilishinda mechi tatu, kilitoka sare mbili na kufungwa mchezo mmoja.

Kama ulikuwa hujui ni kabla ya kuteuliwa timu ya Afrika, nyota ya Dilunga ilishaanza kung’ara mapema, kwani mwaka 1972, mkali huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji wanne waliochaguliwa kuunda kombaini ya Afrika Mashariki akiwa na wachezaji Arthur Mwambeta na Kitwana Manara ‘Popat’.

DILUNGA AU KIBADENI?

Kabla ya Dilunga kuteuliwa kwenye kikosi hicho uliibuka utata mkubwa baada ya FAT kudhani mchezaji aliyeteuliwa ni Abdallah ‘King’ Kibadeni.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa FAT ilisema inamhitaji mchezaji aliyekuwa akivaa jezi Namba 10. Na katika kikosi cha Stars wachezaji wawili tu ndio waliokuwa wakivaa jezi hiyo ni Dilunga na Kibadeni.

Hii inaonyesha kwa kiasi gani kipindi hicho mastaa wetu walikuwa wakirandana kwa uwezo. Maana hata vimo vya Kibadeni na Dilunga havikupishana sana.

FAT iliomba ufafanuzi CAF na ndipo ilipobainika, mchezaji aliyekuwa akihitajika ni Dilunga na sio Kibadeni.

MABAO YAMPA SAFARI

CAF ilimteua Dilunga katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao. Katika mchezo dhidi ya Nigeria B, Dilunga alipachika mabao mawili.

Mbali na kuitumikia Yanga, Dilunga alikuwa akifanya kazi Landing, katika Bandari ya Dar es Salaam pia alikuwa akiichezea timu yake ya kazini ya Hydra.

Dilunga ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa ni mfupi kiasi wa kimo alikuwa na uwezo wa kucheza winga zote mbili, straika wa katikati na mwenyewe alipenda zaidi kucheza namba 10.

Mengi yanasemwa kuhusu Dabi ya Kariakoo ikiwamo hat-trick moja ya Abdallah Kibadeni. Hata hivyo, Dilunga naye inasemekana aliwahi kufanya hivyo akiwa Yanga. Pamoja na mengine motomoto kuhusu nyota huyu wa zamani, fuatilia mwendelezo wake wiki ijayo.

Columnist: Mwanaspoti