Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Udugu wa Simba na Al Hilal ulianzia hapa

Simba X Al Hilal Udugu wa Simba na Al Hilal ulianzia hapa

Mon, 30 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Al Hilal ya Sudan iko nchini kwa ajili ya michezo ya kirafiki ambapo tayari imecheza dhidi ya Namungo.

Katika mechi nyingine imepangiwa kucheza dhidi ya Azam na wenyeji wao Simba Sports Club.

Hii sio mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuja nchini kwa ajili ya michezo ya kirafiki. Ilishafika hapa pamoja na TP Mazembe na kucheza katika mashindano maalumu yaliyoandaliwa na Simba.

Pamoja na Al Hilal kutamani kucheza mchezo wa kirafiki na Yanga, lakini inakuwa vigumu kutokana na klabu hiyo kuwa na upinzani Simba SC.

UGOMVI WA SIMBA NA AL MERREIKH

Mwaka 1994 kulikuwa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (ilikuja kuitwa Kombe la Kagame) ambapo fainali zake zilichezwa nchini Sudan.

Simba ilikuwa Kundi A pamoja na Express ya Uganda, Gor Mahia ya Kenya na wenyeji El Merreikh ya Sudan.

Mchezo wa kwanza El Merreikh ilitoka sare na Gor Mahia bao 1-1, mchezo wa pili Simba ikafungwa 2-1 na Express. Katika michezo ya mwisho El Merreikh ikaifunga Express 2-1 na Simba ikaifunga Gor Mahia 2-0.

Hapo ukabaki mchezo mmoja ambao ungeweza kuamua hatima ya timu mbili za kwenda nusu fainali. El Merreikh ikiwa na pointi tano, Express pointi nne na Simba pointi mbili na mchezo uliokuwa ukiamua timu zitakazosonga mbele ulikuwa ni ule wa Simba na wenyeji, El Merreikh.

SIMBA YA MOTO

Unaambiwa soka lilitembea kisasawa hadi mapumziko Simba ilishafungwa bao 1-0. Kocha Dragan Popadic alipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo sijui aliwaambia nini wachezaji wake.

Simba ilirudi ikiwa ya moto na kusawazisha bao kupitia kwa Ramadhani Lenny lililokuwa bao la penalti.

Baada ya kufunga penalti mwamuzi Mzanzibar Hafidh Ali alikataa na kumtaka Lenny kurudia tena.

Haikuwa kazi ngumu kwa staa huyo aliyeitwa Abega akifananishwa na kiungo wa kimataifa wa Cameroon, Theophile Abega.

Kama vile haitoshi Simba ilitembeza boli na kuwakimbiza sana wenyeji. Kwa kuwa mchezo ulipigwa usiku, wenyeji wakaona isiwe tabu wakawapunguza nguvu wachezaji wa Simba kwa kuzima taa za uwanjani.

POPADIC AWAPA MBINU

Wakati taa zikiwa zimezimwa ili kuwatoa mchezoni Simba, Kocha Popadic akawaambia wachezaji wake wapashe miili yao moto kwa kufanya mazoezi ya viungo.

Taa zilipowaka mchezo ukawa uleule, Simba ikaikimbiza sana El Merreikh hadi ikapata bao la pili katika dakika ya 88.

Hapo sasa ndio mpira ukaisha, Waarabu wa Sudan hawakukubali waliwarushia mawe wachezaji wa Simba na kuwaumiza kwa kiasi kikubwa.

Hata mchezo ulipotakiwa urudiwe haikuwezekana kwa kuwa wachezaji watano wa Simba walikuwa wamejeruhiwa vibaya sana.

Taarifa zinasema kipa Mohammed Mwameja alilazimika kushonwa nyuzi 12 kichwani.

YANGA NAYO ILIKUWEPO

Kundi B zilikuwapo timu nne ambao ni Yanga ya Bara, Small Simba ya Zanzibar, Mebrat Hail ya Ethiopia na wenyeji, Al Hilal.

Al Hilal iliifunga Small Simba 1-0 Yanga haikufungana na Mebrat Hail. Small Simba ikakubali kichapo cha mabao 2-0 kwa Yanga na Al Hilal haikufungana na Mebrat Hail.

Mchezo wa Al Hilal na Yanga ukaisha kwa sare ya bao 1-1 na Mebrat Hail ikakubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Small Simba.

Yanga ikatoka kifua mbele kwenye kundi hilo kwa kuwa na pointi nne sawa na Al Hilal lakini iliongoza kundi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

KATIBU CECAFA AIPONDA SIMBA

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati, James Tirop aliiponda Simba kwa kugomea mchezo wa marudiano.

Tirop alipohojiwa na aliyekuwa mtangazaji wa Redio ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Tido Mhando alisema uwanja ulikuwa ‘natural’ huwezi kusema kama Simba ilipigwa na mashabiki wa El Merreikh.

Tido alimpohoji kwanini ni wachezi na viongozi wa Simba ndio walioshambuliwa, alijibu ni kwa kuwa walikuwa wakikimbia hovyo uwanjani.

“Simba haiwezi El Merreikh tutaona kwa kuwa timu hizo zimepangwa kucheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika,” alisema Tirop katika mahojiano hayo.

URAFIKI ULIANZIA HAPA SASA

Nusu fainali ilipaswa kuchezwa na timu nne ambazo ni El Merreikh, Express ilhali Yanga na Al Hilal.

Yanga ikaanza na mshindi wa pili wa Kundi A ambaye ni Express matokeo yakawa sare na timu hiyo ya Tanzania kutolewa kwenye matuta kwa kufungwa penalti 5-4.

Al Hilal ikagoma kucheza na wapinzani wao wakubwa wa Sudan, El Merreikh kwa kudai siyo timu iliyoshinda katika kundi lake.

Timu hiyo ilisema inataka kucheza na Simba ambayo ndiyo iliyoongoza kundi.

Tangu hapo Simba na Al Hilal zimekuwa marafiki wakubwa na kutembeleana mara kwa mara. Mwaka jana Simba ilienda Sudan kucheza michezo ya kirafiki iliyoandaliwa na timu hiyo.

El-Merreikh ikacheza na mchindi wa tatu wa Kundi B Small Simba (vyanzo vingine vya habari vinasema ni Shangani FC) na wenyeji wakashinda 1-0.

Fainali ikapigwa kati ya El Merreikh na Express na wenyeji wakashinda mabao 2-1 na kutawazwa kuwa mabingwa.

TURUDI KWA TIROP SASA

Baada ya michuano hiyo kuisha Simba na El Merreikh zikakutana kwenye Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika). Mchezo wa kwanza ukapigwa katika Uwanja wa Taifa a.k.a Shamba la Bibi jijini Dar es Salaam.

Ulikuwa ni mwezi wa Ramadhani, hapa mchezo uliisha kwa Simba kushinda bao 1-0 lililofungwa na Edward Chumila.

Mchezo wa pili, uliofanyika Sudan na kuwa na ulinzi mkali sana wa wanajeshi, Simba ilishinda tena kwa bao 1-0 kwa bao la Nteze John alilofunga baada ya kipa mahiri wa El Merreikh, Ahmed Brema kulitema shuti kali la kutoka katikati ya uwanja la Athuman Abdallah ‘China’.

Columnist: Mwanaspoti