Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Manula ungewaona mabeki hawa, ungesemaje?

MANULA AISHI Aishi Salum Manula

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mara nyingi huwa nawaambia wenzangu kwamba nashukuru kuliona soka la mwisho la Tanzania.

Niliwaona wanasoka walioshiriki kuipeleka Tanzania kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Kombe la Mataifa la Mataifa Huru ya Afrika (Afcon) mwaka 1980.

Baada ya kizazi kile kustaafu kusakata soka kilichobaki sasa ni sawa na maigizo ya soka ambayo hayajifikia hata nusu ya kiwango cha wachezaji wale. Kwa hiyo navijua kuwaona wachezaji wale waliokuwa na viwango vikubwa sana tofauti na hawa wa sasa.

Nataka kusema nini? Wiki hii kulikuwa na video iliyokuwa ikisambaa katika mitandano ya kijamii. Kipa wa namba moja wa Simba, Aishi Manula alikuwa amesimama katika bwawa la kuogelea (swimming pool) sambamba na beki wa kushoto wa klabu hiyo, Mohammed Hussein Zimbwe ‘Tshabalala’.

Katika video hiyo iliyosambaa kwa kasi, Manula anasikika akimsifia Tshabalala.

Baadhi ya maneno ya Manula yalikuwa haya: “Kuanzia leo miye chawa wako…Kwenye nchi hii, tangu nchi hii imeumbwa hajawahi kutokea fulubeki kama Tshabalala,” kisha akaendelea kusema:

“Kama kuna mtu anabisha mimi naweka milioni yeye aweke jiwe.”

Kama vile haitoshi, Manula akaendelea kutoa sifa za Tshabalala kwa kusema jamaa anapandisha mashambulizi, anafunga na anakaba.

NI KUWAKOSEA HESHIMA WAKONGWE

Shida kubwa hapa sio kama Tshabalala ni beki mbaya, lakini tatizo ni Manula kusema kwamba tangu nchi hii imeumbwa hajapata kutokea fulubeki kama yeye.

Huku ni kuwakosea heshima wakongwe waliotangulia kabla ya Tshabalala.

Inawezekana kipa huyu namba moja wa Simba na tegemeo la Timu ya Taifa ya Tanzania ameteleza au amekengeuka. Ingekuwa vyema kama angewaomba radhi wakongwe hawa.

Hakuna mdau wa soka anayesema Tshabalala ni beki mbaya. Beki huyo wa Simba ana uwezo mkubwa, lakini alichotakiwa kusema Manula ni kwamba kwa sasa hakuna beki anayemfikia Tshabalala, labda hapo watu wengeweza kumshindanisha na wachezaji wa kiwango chake.

Lakini sio kusema “Tangu nchi hii imeumbwa… hajapata kutokea beki kama Tshabalala.” Huku ni kuukosea heshima mpira wetu. Hebu hapa tuwaangazie mabeki wachache tu ambao Tshabalala angepaswa kujifunza kutoka kwao.

WAKALI ZAIDI

Mohammed Kajole, Mwenyezi Mungu amrehemu. Jamaa alikuwa anajua soka. Beki namba tatu. Huyu alicheza Simba kwa mafanikio. Alikuwamo kwenye kikosi kilichoitoa Mufulira Wonderers 1979.

Alikuwa anakaba, anapandisha timu, pia alikuwa na uwezo wa kufunga kwa kona za moja kwa moja.

Yanga ilikuwa na mtu anayeitwa Ahmed Amasha ‘Mathematics’ alikuwa na uwezo wa kukaba na kupandisha timu. Pia alifunga kwa kona za moja kwa moja.

Amasha (Mwarabu wa Tabora) kabla ya kucheza beki wa pembeni alikuwa kiungo, aliunda ukuta wa Berlin wa Yanga kunzia mwaka 1981 chini ya Kocha Mjerumani Rudolf ‘Rudi’ Gutendorf.

Simba ilikuwa na beki mwingine kwenye nafasi ya Tshabalala aliyeitwa Twaha Hamidu ‘Noriega’ huyu alifananishwa na Rais wa Panama, Manuel Antonio Noriega kutokana na uwezo wake wa kukaba na kushambulia. Kumbuka kabla ya kucheza beki wa kushoto alikuwa winga. Kwa hiyo kupandisha mashambulizi halikuwa tatizo.

Timu ya Nyota ya Mtwara ilikuwa na beki wa kushoto, Mohammed Chuma. Mkongwe huyu aliitumikia Taifa Stars kwa mafanikio kwa miaka 10 mfululizo. Alikuwa na nguvu, uwezo mkubwa wa kupambana na washambuliaji watukutu na kupandisha mashambulizi.

Klabu ya Pan Afrika ilikuwa na beki wa kushoto aliyeitwa Mohammed Mkweche.

Huyu alitokea timu ya vijana ya Yanga na baadaye Breweries na Pan Afrika. Alikuwa na kipaji na uwezo mkubwa.

HAWA WALIKUWA WAKALI ZAIDI

Labda hawa wachezaji niliowataja hapo juu walikuwa wa zamani sana. Hebu niwataje wale ambao Tshabalala na Manula wanaweza kuwa wamewasikia hata kwenye redio.

Yanga ilikuwa na mtu aliyeitwa Kenneth Pius Mkapa. Jamaa alianza kucheza kama straika wa kati kisha akarudishwa beki wa kushoto. Haikuwa rahisi kumpita Mkapa alipocheza beki wa kushoto. Aliitumikia pia Stars. Zamani beki wa kushoto Yanga ilikuwa inarithiwa, Fredy Felix ‘Minziro’ naye aliwahi kurithi namba hii. Jamaa alikuwa mkali wa mipira iliyokufa ‘Banana Chop’. Klabu ya Coastal Union ya Tanga ilikuwa na beki wa kushoto aliyeitwa Joseph Lazaro. Achana na huyu mtu alikuwa anajua kukaba na hata kupandisha timu.

Pamba ya Mwanza ilikuwa na beki wa kushoto Abdallah Boli. Hakuwa mtu wa mchezo mchezo katika kukaba na kushambulia. Beki mwingine wa kushoto ambaye alikuwa mkali na Tshabalala anapaswa kujifunza kutoka kwake ni Alfonce Modest. Niseme nini kuhusu huyo mtu? Alikuwa anakaba na ana akili ya kushambulia.

Huyu alitamba na Pamba ya Mwanza, Simba, Yanga na Mtibwa Sugar. Aling’ara pia na Stars.

Katika listi hii nisingeweza kumsahau mchezaji kiraka kama Nurdin Bakary. Pindi alipocheza kama beki wa pembeni alikuwa na vitu vingi kama unavyomuona Erasto Nyoni anayeondoka na uwezo wake.

Beki Amiri Maftaha. Huyu alitokea kwenye ukoo wa mpira pale Mwanza.

Beki huyo alicheza Yanga na Simba kwa nyakati tofauti. Pia alikuwa na umbile dogo lakini uwezo wa hali ya juu. Achana naye alipokuwa kwenye ubora wake Maftaha alikuwa mtu kwelikweli. Hata kipaji chake kilipopotea wengi walisikitika. Tshabalala na Manula walipaswa kumuuliza kocha wao wa Simba, Juma Mgunda kwanza kuhusu wachezaji wa enzi zake.

Pia, walipaswa kumuuliza kocha wao msaidizi, Selemani Matola kuhusu mabeki aliocheza nao kabla ya kuwavunjia heshima wakongwe hawa.

Manula alipaswa kuwaheshimu na sio kumpa sifa Tshabalala bila ya kutazama waliomtangulia. Na ikitokea siku Tshabalala akitaka kumsifu Manula kwanza afanye utafiti kuhusu uwezo wa makipa wa zamani kina Athuman Mambosasa, Omary Mahadhi Bin Jabir na Mohammed Mwameja. Wengine ni kina Elias Michael na Juma Pondamali, Ally Yusuf ‘Iddy Msakaa’ na Iddy Pazi ‘Father’.

Columnist: Mwanaspoti