Bado tunaendelea na maombolezo ya kumuenzi nyota wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele.
Pamoja na kwamba Pele alikuwa ni raia wa Brazili, lakini Waafrika wengi walijinasibisha naye kwa kumuona kama mwenzao.
Wiki iliyopita niliandika kwamba Pele, ameshafanya kila kitu ambacho katika dunia ya leo tunaviona kama vitu vipya katika soka.
Nilisema Pele aliyerafiki dunia Desemba 29 mwaka jana na kuzikwa Januari 3, alishapiga kila aina ya chenga na alishafunga kila aina mabao ambayo leo hii yanaonekana ya ajabu katika ulimwengu wa mchezo wa soka.
Hakuna maajabu kwa yote yaliyofanywa na Johan Cruyff alikuwa na kitu kinachoitwa ‘Cruyff turn’ Pele alishafanya mapema sana.
Mambo ya Cristiano Ronaldo, Zinedine Zidane ‘zizzou style’, ‘Iniesta drible’ Pele alishafanya, Ronaldo bicycle kick, Pele alishazipiga sana. Kila aina ya utundu ‘skills’ katika mpira, Pele alishafanya.
Hata kila kile alichokifanya Lionel Messi, Pele alishafanya mapema sana.
MICHEZO YA AFRIKA NIGERIA
Katika Mashindano ya Michezo ya Afrika (All African Games), mjini Lagos, Nigeria mwaka 1973 Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ ilishiriki Katika michuano hiyo, iliyochezwa katika mtindo wa ligi, Tanzania ilifika nusu.
Mchezaji Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’ alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliounda kikosi hicho, na ilitoka sare mbili na kufungwa mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria.
Tanzania ilizitambia timu mbalimbali, ikiwamo mwenyeji Nigeria iliyoingiza timu mbili A na B.
Tanzania ilitoka sare tasa na Nigeria A, na kuifunga B yao mabao 2-1. Pia, ikazifunga Ghana na Togo kwa kuichapa kila moja bao 1-0.
Katika nusu fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Surulere, Lagos, Tanzania ilitoka suluhu na Nigeria na sare ya 1-1 na Misri.
Tanzania ilishindwa kuendelea mbele baada ya kufungwa na Algeria mabao 2-1. Fainali ikachezwa kati ya Nigeria na Algeria.
PELE WA AFRIKA
Moja kati ya chenga ambayo Kibadeni alikuwa akiitumia enzi zake katika miaka ya hivi karibuni ilitumiwa sana na mastaa kama Jay Jay Okocha na Ronaldinho Gaucho. Chenga hiyo maarufu kwa jina la ‘Karata Tatu’ hata Pele aliwahi kuitumia uwanjani enzi zake.
Kibadeni pia alikuwa na uwezo wa kuondoka na kijiji, kuwapiga chenga kundi la wachezaji wa timu pinzani kutoka katikati ya Uwanja hadi kumpiga chenga kipa na kufunga.
Ni katika michuano hiyo ya All African Games, Kibadeni akiwa amevalia jezi namba 10 (kama Pele) mgongoni alifanya mambo makubwa hadi mashabiki wa soka wa Nigeria waliokuwa uwanjani walipiga kelele na kumuimba kwa kumwita Pele wa Afrika.
Hata kilipochaguliwa kikosi cha Kombaini ya Afrika kutokana na michuano hiyo, wengi waliamini Kibadeni alistahili kuwamo kwenye kikosi hicho. Kwa kuwa haikuwa bahati yake, kura ikamwangukia Maulid Dilunga ambaye aliambatana na kipa wa Omari Mahadhi.
Uteuzi uliingiwa na utata, baada ya Chama cha Soka Tanzania (FAT), kulipeleka jina la Kibadeni.
Shirikisho la Afrika (CAF) halikutuma jina bali lilisema lilikuwa limemchagua mchezaji aliyekuwa anavaa namba 10. Enzi hizo namba 10 ilikuwa ilikuwa inavaliwa na Kibadeni na inachezwa na Dilunga.
KING ALIPAGAWISHA GHANA
Kama haitoshi, mwaka 1974 Kibadeni akiwa na kikosi cha Simba, ilienda Ghana kucheza mchezo wa robo fainali wa Klabu Bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika). Katika mchezo huo dhidi ya Accra Hearts of Oak, Simba ilipokelewa kwa kebehi kwa kutaniwa ni wanafunzi na wangefungwa mabao 12 katika mchezo huo.
Simba ilitangulia kwa bao la mapema lililofungwa na Adamu Sabu na Accra ikasawazisha.
Wakati Waghana wakiamini mchezo huo ulikuwa ukiisha kwa sare ya 1-1, Kibadeni aliuchukua mpira kutoka katikati ya uwanja na kuwapiga chenga wachezaji wa Accra mmoja baada ya mwingine na kummalizia kipa na kufunga bao la pili.
SAKHO ANA CHA KUJIFUNZA
Wakati akihojiwa baada ya usajili wa Pape Ousmane Sakho, Mtendani mkuu wa zamani wa Simba, Crescentius Magori alisema, Simba ilikuwa imemleta Kibadeni mwingine.
Magori alisema, Sakho ni mchezaji anayejua kuingia ndani ya 18 ya timu pinzani na ana uwezo mkubwa wa kukukota mpira. Alipoona watu wengi hawamweliwi alisema kwa wale waliomuona Kibadeni, huyo ndiye mfano wake.
Lakini bado Sakho anayefanana kiasi kwa kimo na Kibadeni anayevaa jezi ya nyota huyo Namba 10 ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kutoka kwa gwiji huyo ili kuweza kuitendea haki jezi hiyo uwanjani.
SIMBA ILIENDA NA JINI GHANA
Baada ya mpira kuisha beki wa kati wa Accra, Mama Akwa aligoma kuja Tanzania kwa madai Simba ilikuwa na jini langoni mwake.
Alipotakiwa kufafanua, Akwa alisema kila alipopanda na kupiga mashuti, kipa Athuman Mambosasa alikuwa imara langoni na alimkatisha tamaa kwa mashambulizi yote waliyoyafanya.
Kikosi cha Simba kilikuwa na Mambosasa, Shaaban Baraza, Mojammed Kajole, Athuman Juma, Omari Chogo/ Aloo Mwitu.
Wengine ni Khalid Abeid, Jimmy Rogers Willington Mwaijibe ‘Willy Mwaijibe’, Haidary Abeid, Adam Sabu , Kibadeni na Abbas Dilunga/ Saad Ali.