Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Eti Kibadeni alikuwa Yanga?

Kibaden Abdallah Kibadeni

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mmoja kati ya wachezaji waliopata umaarufu mkubwa nchini ni Abdallah Athumani Seif maarufu kama Kibadeni.

Huyu bwana alikuwa fundi wa mpira na ameisaidia sana Simba katika mambo mengi na kuweka rekodi kibao.

RANGI YA JEZI ZA YANGA

Pamoja na kuitumikia Simba kwa kwa mafanikio makubwa, Kibadeni inadaiwa alikuwa na mapenzi na Klabu ya Yanga.

Inadaiwa dhamira yake ya kwanza katika kucheza soka ilikuwa ni kuitumikia klabu hiyo yenye masikani yake Mitaa ya Jangwani. Kabla ya kutua Simba kwa mara ya kwanza mwaka 1970 alianzia kufanya mazoezi katika Uwanja wa Kaunda uliokuwa unamilikiwa na Yanga.

Hata hivyo, jitihada zake hazikuzaa matunda kwani hakuna aliyekiona kipaji chake kwa wakati huo na kushindwa kumfungulia mlango. Kibadeni alitarajia angeweza kuvaa jezi za Yanga ili aitumikie timu hiyo, lakini mipango yake ilikwamishwa.

Jambo hili, hata Kibadeni mwenyewe amekuwa akilitolea ufafanuzi wa kutosha mara kwa mara.

Kibadeni amefichua kitu kilichomfanya kwenda kufanya mazoezi na Yanga mwaka 1969 kuwa ni kuvutiwa sana na rangi za jezi zao kwa kuwa zimefanana na zile za Chama Cha TANU ambapo ndani ya familia yao walikuwa ni wapenzi wakubwa wa chama hicho.

Baba yake mzazi Athuman Seifu, miaka ya 1960 alikuwa mwenyekiti wa TANU akaja kuwa diwani wa CCM Wilaya ya Ilala, hivyo rangi za njano na kijani zilitawala nyumbani kwao na hilo likamfanya avutike mpaka Jangwani ambako wanatumia jezi zinazoendana na rangi hiyo.

Staa huyo aliwahi kufafanua kuwa vitambaa vya makochi nyumbani kwao vilikuwa na rangi ya kijani.

KWA NINI KIBADENI

Jina la hilo halipo katika majina ya ukoo wao. Ni jina la utani alilopewa na watoto wenzake wakati akisoma katika Shule ya Msingi ya Habib Punja iliyoko Mtaa wa Mwanza, Ilala jijini Dar es Salaam.

Jina la Kibadeni maana yake ni kitu cha baadaye. Na hii ilikuwa ni mwaka 1959 (wakati alipokuwa na umri wa miaka 10 tu).

Kibadeni alizaliwa Oktoba 11, 1949 katika Mtaa wa Kiburugwa, Mbagala jijini Dar es Salaam. Kibadeni alipokuwa na umri wa miaka 20 tu, alijiunga na Simba SC iliyokuwa ikiitwa Sunderland.

AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI

Mwaka 1974, Kibadeni alikuwa mmoja kati ya wachezaji walioshiriki kuipeleka Simba katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mabingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa).

Miamba hiyo ilianza kucheza raundi ya kwanza dhidi ya Linare ya Lesotho na nyumbani kushinda kwa mabao 3-1 na walipoenda ugenini walishinda kwa mabao 1-5.

Katika raundi ya pili, Simba ilicheza na Green Buffaloes ambayo zamani ilikuwa timu ya Jeshi la Zambia. Katika mchezo wa nyumbani ilitoka sare tasa lakini ugenini Simba ilishinda 0-9 na kutinga robo fainali.

Hapo ilicheza na Hearts of Oak ya Ghana na nyumbani mchezo uliisha kwa sare tasa na Simba kushinda ugenini 1-2 kwa mabao ya Kibadeni na Adamu Sabu.

Katika nusu fainali Simba ilitolewa kwa penalti 3-0 na Ghazl El Mahalla Sporting Club maarufu kama Mahalla El Kubra.

Inadaiwa baada ya kufanyiwa visa vingi, wachezaji wa Simba waliamua kujikosesha penalti hizo. Kikosi cha Simba kiliundwa na Athuman Mambosasa, Shaban Balaza, Hamis Askari, Athuman Juma na Aloo Mwitu.Pia, Khalid Abeid, Willy Mwaijibe (Gumbo), Haidari Abeid (kapteni), Adamu Sabu, Kibadeni na Abas Dilunga.

HISTORIA MIAKA 45

Julai 19, 1977 Kibadeni aliandika historia katika dabi ya Kariakoo kwa kufunga mabao matatu ‘hat trick’.

Mpaka leo Kibadeni anashikilia rekodi hiyo ambayo haijavunjwa kwa takribani miaka 45.

Mwaka huo Simba ikiwa chini ya Mwenyekiti, Joachim Kimwaga na Katibu Jimmy David Ngonya, iliundwa na kikosi hiki Mahadhi, Daud Salum, Mohammed Kajole, Athuman Jumam na Mohamed Bakary ‘Tall’.

Wengine ni Aluu Ali, Mwaijibe, Jumanne Hassan Masmenti, Kibadeni, Martin Kikwa/ Dilunga.

KWA NINI PELE, KING?

Kutokana na umahiri wake wa kusakata kabumbu, Kibaden aliitwa Pele au King kwa maana ya Mfalme. Wakati alipokuwa akicheza, Brazil ndiyo iliyokuwa juu kisoka, mchezaji ambaye alikuwa anamuiga staili yake ya uchezaji ni Edson Nascrimento ‘Pele’. Pia, Kibadeni alikuwa akivaa jezi namba 10 kama Pele. Mashabiki walipoona kiwango chake ni cha kustajabisha walimuita King. Mashabiki wa Simba ndio waliompachika jina hilo wakimfananisha na mfalme wa soka duniani Pele, kwa hiyo akajikuta akiitwa Abdallah Kibaden King.

Columnist: Mwanaspoti