Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MJUAJI: Duh! ushabiki wa timu kwa mastaa wa Simba na Yanga

Mjuaji Pic MJUAJI: Duh! ushabiki wa timu kwa mastaa wa Simba na Yanga

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa leo buana, nawazungumzia wachezaji mbalimbali nyota waliokuwa na mapenzi ya Simba lakini wakajikuta wakiitumikia Yanga na wale wenye mapenzi na vijana wa Jangwani, lakini wakaishia kuwatumikia Wekundu wa Msimbazi. Je unawajua? Endelea nayo...!

ABDALLAH ‘KING’ KIBADENI

Huyu ndiye mwamba anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye dabi ya Kariakoo hadi sasa.

Mwaka 1977, wakati Yanga ikifungwa 6-0 na Simba, mabao matatu yalifungwa na Kibadeni. Lakini hata Kibadeni mwenyewe anakiri awali mapenzi yake yalikuwa ni rangi ya kijani kutokana na rangi hiyo kutumiwa na Chama cha TANU.

Baba yake Abdallah Seif alikuwa kiongozi wa chama hicho cha siasa ambacho mwaka 1977 kilibadili jina na kuitwa CCM baada ya TANU kuungana na Afro Shiraz.

Kama haitoshi, Kibadeni alishawahi kwenda Jangwani kutaka kuichezea timu hiyo, lakini hakupata nafasi inadaiwa ni kutokana na kikosi hicho kuwa imara katika miaka ya 70‚ akakosa nafasi katika kikosi kilichoitwa The Sky is the limit.

Ndipo King Mputa alipoangukia upande wa pili na kuwa staa mkubwa sana.

Mbali na kuwa staa mkubwa alikuwa pia kocha aliyeipa mafanikio timu hiyo mwaka 1993 kwa kuifikisha kwenye fainali ya Kombe la Caf.

EDWARD CHUMILA

Huyu kwa sasa ni marehemu, lakini naye alidaiwa aliwahi kwenda Jangwani akitokea Temeke Squad jijini Dar es Salaam, ila kwa bahati mbaya alikataliwa. Tena aliwambiwa maneno fulani ya kashfa ambayo siyo mazuri kuandikwa katika safu hii.

Maneno hayo yalimkera sana. Bahati nzuri kwa upande wake alipoenda upande wa pili, Simba akachukuliwa na akaapa kila atakapokuwa akikutana na Yanga ni lazima awafunge. Kweli alifanikiwa kutimiza dhamira yake kwa kuifunga Yanga mara kadhaa. Waulize mashabiki wa Jangwani ni mshambuliaji gani aliyekuwa akiwanyima raha kutoka Msimbazi, hawataliacha jina la Chumila kwa namna alivyojua kuitesa.

MADARAKA SULEIMAN

Mzee wa Kiminyio, akihojiwa katika kipindi cha AM cha UTV, hivi karibuni Madaraka alishindwa kuthibisha mapenzi yake kwa timu aliyoitumikia kwa muda mrefu Simba Sports.

Mtangazaji Mahmoud Zubery alimbana na kumwambia alikuwa na taarifa zake alizopewa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Athuman Abdallah ‘China’ waliokuwa wakiishi naye katika Kitongoji cha Manzese.

Inadaiwa Madaraka miaka ya nyuma alishangilia upande wa pili wa shilingi katika mechi ya dabi ya kihostoria ya mwaka 1974 kule Nyamagana Mwanza, Simba ilifungwa 2-1 na Yanga.

METHOD MOGELLA

Kiongozi mmoja shabiki kindakindanki wa Simba, Meja Rashid Makame alimuona akiwa na timu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Oljoro), akavutiwa na kiwango chake akamsogeza hadi JKT Ruvu na kumtangenezea mazingira ya kujiunga na Simba. Kitu ambacho Meja Makame hakuwa anakijua ni kwamba, Method ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa Yanga wa kulia.

Mwaka 1991 hatimaye Method’ Fundi’ akaitosa Simba na kwenda kujiunga na timu ya mapenzi ya moyo wake, Yanga.

EZEKIEL GRAYSON

Kipaji hiki kilionwa na Mwenyekiti wa FAT (enzi hizo) wa Mkoa wa Pwani, Subira Mambo ‘Mr Handsome’.

Mzee Mambo alikuwa ni Mwananchi wa kutupwa, hivyo akamtoa Ezekiel Grayson ‘Jujuman’ (baba yake Aunty Ezekiel) kutoka Kisarawe hadi Jangwani.

Watu walioishi na Ezekiel wilayani Kisarawe walishangaa kumuona akienda Jangwani kwa kuwa walimjua ni Mnyama. alikuwamo kwenye kikosi cha Yanga kilichofungwa 6-0 na Simba. marehemu Ezekiel hatimaye mwaka 1977, alijiunga na timu ya mapenzi yake, Simba Sports.

ATHUMANI JUMA ‘CHAMA’

Huyu akiwa Mwanza, alichezea timu ambayo ni tawi la Simba ya Nyamaume.

Chama naye ni marehemu alikuwa Mnyama haswa lakini viongozi wa Simba ndio waliomfanya aende Yanga.

Akiwa amechaguliwa Timu ya Taifa ya Tanzania iliyokuwa inacheza na Nigeria kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 1980, Chama aliachwa Dar es Salaam na timu hiyo katika safari ya kwenda Nigeria. Viongozi wa Simba wakataka kusamjili lakini wakamtelekeza katika Hoteli ya Sky Way, Posta jijini Dar es Salaam. Chama alirudi Mwanza na aliyekuwa kiongozi wa Yanga, Issa Makongoro wa Yanga akaenda kumsajili kwa ulaini kabisa.

HUYU HATAKI KUTAJWA

Staa huyu alikuwa akipandisha bendera ya Simba juu ya nyumba yao katika mkoa mmojawapo wa Kanda ya Ziwa.

Hata mfadhili wa zamani wa Yanga, Abbas Gulamali alipoenda kumsajili, mlezi wa mchezaji huyo alimwonyesha bendera ya Simba iliyokuwa imepandishwa juu ya nyumba yao na kumwambia ameipandisha huyo aliyemfuata ili kumpeleka Yanga.

Hata hivyo, Gulamali alisema hajali kuhusu hilo, akamsajili. Staa huyo alikuja kupata mafanikio makubwa Jangwani na hadi leo humwambii kitu kuhusu Yanga anabishana na mashabiki nje ya Uwanja wa Benjamini Mkapa ingawaje soka lake amemalizia akiwa mitaa ya Msimbazi.

ATHUMANI ‘CHINA’

Huyu ni kiungo aliyeibukia mitaa ya Manzese akiichezea National Three Stars

Mwaka 1982, Simba Kids ilicheza na timu hiyo na kuifunga mabao 3-0. Kesho yake China alifika viwanja vya Jangwani kuomba kujiunga na Simba Kids katika uwanja wa Simba ambao leo hii kumejengwa makao makuu ya mabasi yaendayo kasi. Lakini China moyoni mwake alikuwa na timu aliyokuwa akiipenda, ambayo ni Yanga.

Mara kadhaa wachezaji wa Simba Kids walipopewa tiketi za bure kuingia uwanjani, China alikwepa kukaa jukwaa la Simba ‘Main Stand’, alikuwa akikimbilia upande wa pili wa Yanga.

Mwaka 1987, China alisajiliwa na Timu ya Tumaini iliyokuwa daraja la nne Wilaya ya Kinondoni kisha Yanga ikamsajili kibabe.

Mechi yake ya kwanza alicheza dhidi ya Majimaji ya Songea ambayo ilikata rufaa baada ya kupoteza mchezo huo ikidai China ni mchezaji halali wa Tumaini na sio Yanga.

FAT chini ya Mwenyekiti, Mohammed Mussa ilitupilia mbali rufaa ya Majimaji kwa kuiambia ilichelewa kukata rufaa.

China akabaki Yanga akicheza mazoezi na kusafiri na timu hiyo msimu mzima na msimu uliofuata 1988 ikampandishwa kama mchezaji kutoka kikosi cha pili.

Msimu huo China akachaguliwa kuwa mchezaji mdogo kuliko wote wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) akitajwa kuwa na umri wa miaka 18, miaka ambayo alishaipita tangu akiwa Simba Kids. Mwaka 1994, China alijiunga na Simba kwa maslahi kutokana na ushawishi wa Azim Dewji baada ya kurudi nchini akitokea Uarabuni. Kabla ya hapo China alikwenda Uingereza kuitumikia timu ya Ligi Daraja la Nne ya Walsall FC.

Columnist: Mwanaspoti