Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MASTORY YA OSCAR: Nimemuwaza huyu Ninja mara tatu

Nabi Ninja Kocha Nabi na Ninja

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Sajili zote za Yanga zikatikisa. Wakasimamisha nchi mpaka kwa kufanya utambulisho usiku wa manane.

Kabla ya hapo walijivunia kuwaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wao muhimu. Shomari Kibwana, Zawadi Mauya na Bakari Mwamnyeto ni kati ya wachezaji waliolamba mikataba mipya Yanga na kufurahiwa na mashabiki wao.

Kisha ikafika zamu ya Abdallah Shaibu ‘Ninja’ naye akalamba mkataba wa mwaka mmoja.

Ninja kama jina lake ni kati ya wale mabeki wachache wagumu wa kizamani waliopo mbioni kutokomea. Hawatokomei kwa sababu wana uwezo mkubwa, bali kutokana na mabadiliko ya soka la kisasa haliwahitaji tena.

Ninja ni kati ya wale mabeki wa kizamani wagumu wanaojua kulihami lango lao vyema. Ni beki halisi. Anajua kupora mipira na kumdhibiti mpinzani asimfikie kipa. Anajua kuondoa mpira katika hatari na kuliweka lango lake salama. Na hayo ndiyo majukumu ya msingi ya beki.

Tatizo ni kwamba soka la kisasa la kina Pep Guardiola limekuja na vitu vingi vipya vya kutaka kila mchezaji hadi kipa ajue kuuchezea mpira.

Soka la kisasa limekuja na mambo mapya ya kutaka washambuliaji wasipimwe kwa mabao pekee, bali hadi jinsi wanavyoshiriki katika uzuiaji wakati hawana mpira.

Ni sababu kama hizi zinazomfanya beki kama Ninja akose nafasi ya kucheza katika timu kama ya Yanga mara kwa mara. Kitu kama hiki pia kinamtokea Gadiel Michael wa Simba. Mpira wa kisasa unahitaji mambo mengi sana kwa mchezaji.

Majuzi tu hapa tulikuwa na mjadala juu ya kimo cha Dickson Job, lakini hapohapo Yanga ambapo Job anacheza katika benchi alikuwepo Ninja aliyemzidi urefu maradufu. Kule timu ya taifa ambapo mjadala ulianzia katika benchi alikuwepo Kennedy Juma ambaye ni mrefu kuliko Job. Ni kwa sababu soka la kisasa linahitaji mambo mengi zaidi ya majukumu ya msingi. Job anajua kuuchezea mpira kuliko Ninja na Kennedy.

Kila ninapomtazama Ninja katika benchi la Yanga huwa najiuliza ni kwa jinsi gani tumepoteza wachezaji wenye miili aina yake.

Umbo la Ninja linaendana na nafasi anayocheza. Mabeki wa katikati huwa ‘wanacheza mijitu iliyoshiba na kwenda hewani.’

Tazama hata Ulaya ambao tunapenda kuwatumia kama mifano, wapo mabeki wangapi wafupi? Kama taifa tumepoteza mabeki wengi wenye miili ya Ninja.

Hati ya kusafiria ya Ninja inaonyesha mwaka huu anatimiza miaka 23. Ni umri ambao mchezaji anapaswa kuwa uwanjani. Lakini Ninja ametumia miaka yake miwili ya Yanga tangu arejee kutoka Marekani kukaa benchi au jukwaani kuliko kuwepo uwanjani.

Ni kitu kibaya kwa mchezaji anayetaka kukua na kufika mbali. Unakaa chini na kuutazama mwaka mmoja alioongezewa Yanga unatamani kumlaumu kwa uamuzi wake, lakini unajiuliza Ninja angefanya nini zaidi?

Zipo timu ngapi Ligi Kuu ambazo zinaweza kumpa kile anachopatiwa na Yanga? Kumbuka majuzi tu alipelekwa nje ya nchi na Yanga kutibiwa baada ya kupata majeraha makubwa. Ni timu ngapi Tanzania zinaweza kumpatia huduma hiyo?

Ninja kama walivyo wachezaji wote anatamani kuwepo uwanjani kucheza, lakini inabidi afumbe macho na kukaa benchi kinyonge kisha pesa ziingie katika akaunti yake ya benki. Nimekuwa nikirudia mara nyingi kwamba tukazane kutengeneza ligi tajiri ili kuokoa vipaji vya baadhi ya wachezaji.

Hapo unageuka na kuwafikiria Yanga, wameona nini cha ziada kwa Ninja hadi wakamuongezea mkataba mpya? Kama misimu miwili ametumia akiwa nje ya uwanja kipi kitaongezeka zaidi ndani ya huu mwaka mmoja? Ukweli ni kwamba Yanga wamegundua hawawezi kupata beki mzawa wa daraja la juu kumzidi Ninja. Hakuna sababu za kuingia gharama kumuongeza beki mpya wakati yupo ambaye atakupa utakachopata kwa huyo mpya.

Ukweli mwingine ni kwamba Ninja angecheza zaidi kama angekuwa katika timu nyingi za Ligi Kuu Bara, lakini alikuwa Yanga ambapo nafasi ni finyu. Yanga wameamua kujilinda kwa kumpa mwaka mmoja ili litakapofika dirisha lingine watazame kama wanaweza kumpata beki wa juu zaidi ya Ninja.

Columnist: Mwanaspoti