Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MASTORY YA OSCAR: Kwanini kamati za TFF zisivunjwe zote?

Karia Wallace Rais Rais wa TFF Wallace Karia

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna muda unaweza usione tofauti kati ya Kamati za TFF na zile Kamati za Harusi. Ndiyo unaweza usione tofauti wala usishangae. Kamati za harusi mara nyingi sana humsikiliza bwana harusi. Kamati ya harusi zinaweza kukutana muda wowote wanaotaka wajumbe au aliotaka bwana harusi.

Kuna kamati inaitwa ya Saa 72. Hii ndiyo vituko vitupu! Tukio linaweza kutokea jioni ya leo, wao wakakaa kujadili wiki ijayo. Sasa hayo saa 72 yaliwekwa kwa maana gani? Vituko vitupu! Tukio linaweza kutokea leo lakini kama wadau watakaa kimya, basi kamati hii inaweza kujikausha utadhani hakuna kilichotokea.

Tunaweza kuwa na shida kubwa sana ya wachezaji wazuri. Tunaweza kuwa na shida kubwa sana ya pesa kwenye mpira wetu. Lakini shida yetu kubwa bado iko kwenye watawala. Mpira wetu kwa namna nyingi tu unaonekana unaendeshwa kwa maelekezo. Mpira wetu kwa namna nyingi tu unaonekana unaendeshwa kwa matakwa ya Viongozi wa juu.

Hata ukitazama kanuni nyingi tu za uendeshaji wa mpira zimekaa kimitego. Unawezaje kuweka Kanuni ya kuitaka kila timu mwenyeji kuwa na Ambulance au Gari ya Wagonjwa kwenye kila mechi wakati unajua hakuna timu moja inayomiliki Ambulance? Serikali yenyewe haina Ambulance kwenye kila Kituo cha Afya, timu ya mpira itaweza? Wengi tumejikita kwenye makosa ya waamuzi, kumbe huku kwenye utawala ndiyo kuna tatizo kubwa kuliko hata lile la waamuzi.

Juzi nimecheka sana baada ya kuona maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wakizifungia timu za Tanzania Prisons na Singida Big Stars kwa kosa la kusajili wachezaji ambao bado wana mikataba na klabu zao za zamani. Unajua ni kwa nini nimecheka katika hili? Ni rahisi tu. Kabla ya mchezaji yoyote kucheza mechi yoyote ya Mmashindano ni lazima awe na Leseni kutoka Bodi ya Ligi. Ili kupata leseni, ni lazima Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikutane na kujiridhisha kuwa taarifa za usajili wa kila mchezaji ziko sawa.

Hii ina maana gani? Maana yake kamati hii ilikaa na kuwajadili Musa Mbise na Metacha Mnata na baadaye kujiridhisha kuwa wachezaji hao wako sawa kuzitumikia klabu zao mpya na leseni wakapewa! Kama Musa Mbise alikuwa hajamalizana na Coastal Union, asingepewa Leseni ya kuitumikia Tanzania Prisons. Kama Metacha Mnata angekuwa hajamalizana na Polisi Tanzania, hakutakiwa kupewa leseni ya kuitumikia Singida Big Stars. Ndugu zangu tuna shida kubwa ya uongozi na Utawala kuliko ile ya waamuzi.

Kamati iliyowaidhinisha Mbise na Metacha kuzitumikia klabu zao mpya, ndio kamati iliyozifungia kusajili klabu hizo kwa kosa la kusajili wachezaji ambao bado walikuwa na mikataba na klabu nyingine. Hapo ndiyo utakapojua haujui. Ni sarakasi tupu kwenye mpira wetu. Kuna muda unatamani Kamati zote za TFF zivunjwe ili tuanze upya lakini unajiuliza, itasaidia kama watawala ni wale wale? Sipati jibu. Kama adhabu inakwenda kwa klabu, vipi kuhusu watendaji wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji waliotoa leseni kwa wachezaji hao? Wao adhabu yao ni ipi? Kamati imekaa kimya! Vipi wachezaji wenyewe kama imethibitika wamesaini na klabu mpya wakati mikataba yao ya awali na klabu zao bado ilikuwa halali? Wao wanaachwa tu? Kazi kweli kweli! Lazima tukubali kuambiana ukweli. Lazima tukubali kuwa bado tuna safari ndefu. Pale kwenye shirikisho bado kuna mapungufu mengi sana ya uendeshaji. Ukisema urudi kwenye klabu ndiyo utacheka ufe. Ni vituko vitupu. Ndiyo maana kila klabu ya nchini inaposhitakiwa FIFA aidha na Kocha au Mchezaji, huwa tunashindwa. Hatujawahi kunyooka kabisa. Wajuaji wengi. Pamoja na mapungufu ya waamuzi, binafsi naamini shida kubwa ya soka letu inaanzia kwenye aina ya wachezaji tulionao.

Ukienda kwenye Kamati ya Maadili nayo utaikuta ina changamoto za kimaadili! Wako watu wanaitwa kwenye kamati hizo kwa makosa mbalimbali, lakini husikii muendelezo. Yuko mjumbe mmoja wa Kamati ya Saa 72 aliwahi kuitwa na kamati ya maadili lakini hakuna mrejesho wa taarifa hiyo hadi leo. Kila kamati ni matatizo matupu! Ukigeukia Kamati ya Mashindano, mambo ni yale yale.

Ligi ndiyo kwanza imeanza lakini tayari kuna mechi zimeahirishwa! Ndugu zangu, kama hizi kamati zingekuwa huru na zikafanya kazi yake sawa sawa, mpira wetu ungesogea pakubwa. Mpira wetu ungeimarika sana. Kimsingi hizi kamati ndiko misingi ya mpira wetu inakosukwa. Hizi kamati uelekeo wa mpira wetu. Kamati mbovu huzalisha mpira mbovu. Lazima tufike mahali tuamue.

Kama tunahitaji kusonga mbele ni lazima tuzipe nguvu ya kufanya maamuzi huru kamati hizi. Ni lazima kamati hizi zipewe watu wenye nguvu. Hizi kamati ukizifuatilia utagundua kuwa zina mapungufu mengi kuliko waamuzi wetu. Kama wajumbe watakuwa huru na wakapewa nguvu ya kufanya maamuzi, tutasogea pakubwa. Lakini yako maeneo pia wanayofanya vizuri kwa mfano kwenye masoko, kazi nzuri pia imefanyika. Ligi yetu imetengeneza sana pesa nyingi wakati huu kuliko wakati wowote katika historia ya mpira wa nchi hii. Soka la wanawake pia kumekuwa na kuimarika kwa kiasi kikubwa pia. Tukikubali kukosolewa na kujirekebisha, kuna mahali pakubwa tutasogea.

Columnist: Mwanaspoti