Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MASTORI YA OSCAR: Unaijua hadithi ya Messi na Guardiola?

Pep Na Messi Pep Guardiola na Messi

Mon, 15 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Leo tusizungumze mambo magumu. Maisha tayari ni magumu. Sasa kwa nini tuzidi kuyafanya magumu kwa kuzungumza vitu vigumu kila siku? Mzee wa Kaliua leo anataka tuzungumze mambo rahisi kidogo.

Wikiendi iliyopita nilikuwa natazama ‘dokumentari’ ya Manchester City inayojumuisha matukio ya msimu uliomalizika. Pep Guardiola katika ubora wa mbwembwe zake alikuwa akitoa hamasa katika mechi fulani ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Club Brudge. Ilikuwa kipindi cha kwanza City ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Joao Cancelo na Riyad Mahrez.

Guadiola alikuwa akiwaambia wachezaji wake, “mnajua kwa nini kila siku nawaambia kwamba Lionel Messi ndiye mchezaji bora kuwahi kutokea duniani? Ni kwa sababu Messi huwa haridhiki. Timu yake inapokuwa mbele na wengi wakiamini labda mechi imekufa, yeye ndiye anayekazana kutafuta mabao kadri muda unavyosonga mbele kana kwamba hajawahi kufunga kabisa. Messi huwa haridhiki.” Guardiola alimaliza kwa kuwaambia wachezaji wake wakaue mchezo. Manchester City walienda kushinda kwa mabao 5-1.

Kando ya ufundi na mbinu zake huwa nazipenda sana mbwembwe za Pep hasa akiwa katika chumba cha kubadilishia nguo. Anaongea kwa msisitizo akizunguka kama anacheza muziki huku akitupa mikono kama vile wachezaji wake hawamsikii akiongea kawaida. Ungefanikiwa kumuona Pep alivyokuwa anatoa maelekezo katika hii mechi labda ungenielewa vizuri nachozungumzia.

Wadadisi wa mambo wanadai mastaa wengi wanaopita chini ya Pep na kuitamani kazi ya ukocha hutamani zaidi kwa sababu ya mbwembwe na mikwara ya Pep. Mastaa wengi huvutiwa na maisha ya kocha huyo Mhispania katika viwanja vya mazoezi, vyumba vya kubadilishia nguo na anaposimama kando ya mstari kuongoza timu kwenye mechi. Mastaa wake huvutiwa na ile mikogo yake na jinsi anavyotawala, hivyo hutamani kutumbukia katika ukocha na kujaribu kuwa Pep.

Klabu kadhaa za England zilikuwa tayari kumsaini Vicent Kompany, alipotangaza kwamba ataondoka Manchester City miaka mitatu iliyopita. Lakini beki huyo alikataa na kuamua kurejea kwao kucheza Anderletch huko Ubelgiji. Unadhani kwanini ilitokea hivyo? Ni kwa sababu Anderletch walimhakikishia nafasi ya ukufunzi atakapowatumikia kwa mwaka mmoja. Tayari Kompany alimtamani Pep na hadi sasa yupo Burnley anazidi kukua.

Fikiria hili. Kelvin de Bruyne ana miaka 31 tu, lakini tayari anamiliki leseni A ya Uefa ya ukocha. Kwa mantiki hiyo De Bruyne anaweza kukabidhiwa klabu yoyote Ulaya kwa sasa akaisimamia. Mwili wa De Bruyne bado una nguvu za kutosha kiasi ambacho anaweza kuwa uwanjani kwa miaka sita ijayo, lakini tayari akiwa na umri alionao sasa ameshafikiria kumaliza kucheza soka na kuhamia katika ufundishaji. Alipoulizwa, alitania kwamba anatamani kucheza dhidi ya timu ya Pep ili athibitishe kama ni kweli kwamba Pep ni kocha bora duniani kama anavyotajwa.

Haya ndiyo matunda na madhara ya maisha ya mbwembwe za Pep. Pengine De Bruyne anaweza kuacha soka mapema zaidi akiwa bado na nguvu kwa sababu ya kumtamani kocha wake kama ilivyokuwa kwa Kompany.

De Bruyne naye akawaambia wachezaji kwa nini anafikiri Mbelgiji mwenzake Eden Hazard ndiye mchezaji bora kuwahi kucheza Ligi Kuu ya England kama ambavyo Pep anavyomfikiria Messi.

Lakini vipi kuhusu hili suala la Messi? Unahitaji ujasiri wa ajabu kulitaja jina lake katika chumba cha Manchester City ambacho kimesheheni mastaa ambao ni wapinzani wa karibu wa Messi. Pale wapo kina De Bruyne ambao kwa nyakati fulani wamewahi kufananishwa na Messi. Je, anajihisi vipi kocha anapomtumia mpinzani wake kama mfano?

Lakini kumbuka kuna uhasama mkubwa kati ya Messi na Ronaldo. Vipi kuhusu wale wachezaji wanaomkubali zaidi Ronaldo? Kumbuka wapo Wareno kina Ruben Dias na Bernado Silva. Pep ana uhakika hawa watu ‘hawamuumii meno’ anapomtaja Messi kuwa mchezaji bora kuwahi kutokea duniani? Ndiyo. Hawa ni wazungu na tunaamini ni watu waliostaarabika, lakini bado wanabaki kuwa binadamu. Kumbuka kuhusu ugomvi wa Thomas Tuchel na kina Thiago Silva pale PSG? Thiago na Wabrazil wenzake walikuwa hawataki kocha amuweke Mbappe juu ya Neymar. Pep huwa anajiamini nini?

Columnist: Mwanaspoti