Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAONI: Yanga, TFF wekeni kando tofauti zenu hazijengi

Mwakalebela Picha Data MAONI: Yanga, TFF wekeni kando tofauti zenu hazijengi

Sat, 10 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HATUA ya klabu ya Yanga kuamua kukimbilia serikalini kulilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa hakika haileti picha nzuri kwa mustakabali wa soka la Tanzania.

Uongozi wa Yanga umechukua uamuzi huo kwa kile kilichoelezwa kuchoshwa na uonevu ambao klabu yao imekuwa ikikumbana nao chini ya TFF ya sasa ya Rais Wallace Karia na Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidao.

Hatua hiyo ya kukimbilia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu dhidi ya uamuzi mbalimbali ambao TFF na kamati zake imekuwa ikifanya kwa klabu ya Yanga.

Yanga wamelalamikia mengi yakiwamo adhabu ya kufungiwa kwa muda wa miaka mitano na kutozwa faini ya Sh5 milioni kwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa kosa linalodaiwa la utovu wa nidhamu baada ya kuilalamikia TFF kukalia kesi na kupuuza malalamiko yao juu ya sakata la usajili wa Bernard Morrison na ishu za waamuzi.

Bahati nzuri, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuf Singo ameshafafanua namna alivyokutana na uongozi wa Yanga na wizara kuwaita mabosi wa TFF juu ya kadhia hiyo, kuwa ni wazi pande zote mbili haziaminiani ndio maana wamefikia hapo walipo.

Pia ameeleza ametoa siku nne kuanzia walipokutana ili pande hizo zikae na kuwekana mambo sawa kisha kupewa mrejesho wa walichokiamua baina yao.

Sisi kama wadau wakubwa wa michezo na hususani soka, tunaamini hii hatua iliyofikiwa sio nzuri kwa maendeleo ya soka. Hii ni kwa sababu Yanga ni moja ya klabu kubwa na yenye mashabiki wengi nchini na nje ya nchi na ni mhimili wa soka la Tanzania kama ilivyo kwa watani wao Simba.

Ieleweke mapema hatuegemii upande wowote, lakini kama wadau tuna wajibu wa kuzikumbusha taasisi hizo yaani Yanga na TFF pamoja na klabu nyingine kufanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na kuaminiana kwa masilahi ya soka la Tanzania.

Kufanya kazi kukiwa na watu wenye vinyongo ni hatari na inaweza kuharibua ule ustaarabu mzima wa mchezo huo. Hakuna anayependa kuona yale mambo yaliyokuwa yakitokea enzi za Chama cha Soka Tanzania (FAT) ya mchezo huo kuendeshwa kwa migogoro, mizengwe na kesi za mahakamani yakijirudia zama hizi na kubomoa misingi iliyojengwa na TFF ya Leodeger Tenga na wenzake.

Hatua iliyofikiwa na Yanga kukimbilia serikali ni kuonyesha ilivyochoshwa na matendo ya TFF, lakini uamuzi wa serikali kutaka pande mbili zikae na kuwekana sawa ni kielelezo kwamba hayo ni mambo madogo ambayo yanajadilika na kutatuliwa.

Hata hivyo ,hofu yetu ni kwamba Yanga ni klabu kubwa yenye mashabiki lukuki ndani na nje ya nchi, pale wanaposikia kuna mambo hayafanywi sawa juu ya klabu yao, inaweza kuleta picha mbaya kwa viongozi wa TFF na hapo ndipo Mwanaspoti haipendi hali ifikie huko!

Msisitizo wetu kwa pande zote ni kwamba viongozi wote wanapaswa kuendesha taasisi zao, hususani TFF kwa uadilifu na uaminifu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz