Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAONI: Simba huu ni mwaka wa kuishangaza Afrika

Yoyote Pic 1 Data MAONI: Simba huu ni mwaka wa kuishangaza Afrika

Tue, 13 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MECHI za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilimazika jana na kutoa picha kamili ya hatua ya robo fainali itakavyokuwa.

Mabingwa wa soka mara tatu mfululizo nchini, Simba wamemaliza kileleni mwa Kundi A, hivyo hawatakutana na vinara wenzao wa makundi, bali watakabiliana na moja ya timu tatu zilizoshika nafasi ya pili kutoka kundi B, C au D.

Hii ina maana kwamba, katika droo ya robo fainali itakayopangwa Aprili 30, Simba inaweza kukutana na kati ya CR Belouizdad ya Algeria iliyomaliza katika nafasi ya pili nyuma ya nyuma ya Mamelodi Sundowns kwenye Kundi B, au dhidi ya Kaizer Chiefs iliyomaliza ya pili nyuma ya Wydad Casablanca kwenye Kundi C au dhidi ya MC Alger ya Algeria pia iliyomaliza ya pili nyuma ya Esperance ya Tunisia kwenye Kundi D.

Kwa hiyo wapinzani wa Simba tayari wameshafahamika kuwa ni kati ya timu mbili kutoka Algeria na moja ya Afrika Kusini.

Timu za Algeria zimekuwa na sifa ya kuwa ni ngumu sana katika miaka ya hivi karibuni hivyo Simba inatarajiwa kupata upinzani mkali ikipangiwa timu yoyote kati ya MC Alger na CR Belouizdad na vivyo hivyo endapo itapangiwa wakali wa Sauzi, Kaizer Chiefs.

Lakini kuna mambo mengi ya kujivunia na yanayoleta matumaini kwa Simba kwamba inaweza kufanya vyema kwenye hatua ijayo ya robo fainali na hata katika hatua zinazofuata.

Jambo la kwanza ambalo linaleta matumaini makubwa kwa Simba ni hili la kumaliza kileleni mwa Kundi A, kwani Wekundu wa Msimbazi wataanzia ugenini katika mechi yao ya kwanza ya robo fainali na kuja kumalizia nyumbani katika mechi ya marudiano.

Kitu kingine kinacholeta matumaini makubwa ni rekodi nzuri ambayo Simba wameiweka ya kutopoteza mchezo kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kwa miezi 97 iliyopita sawa na miaka 8, Simba haijapoteza mchezo kwenye Uwanja wa Taifa tangu Februari 17, 2013 ilipolala 1-0 dhidi ya Recreativo do Libolo la Angola.

Tangu wakati huo, matokeo mabaya zaidi kwa Simba Kwa Mkapa ni sare. Hii ni rekodi njema sana kwani Wekundu wa Msimbazi hucheza kwa kujiamini sana wawapo nyumbani na kauli mbiu ya “Kwa Mkapa Hawatoki” daima imekuwa ikizaa matunda.

Jambo jingine zuri ni kwamba Simba ilipangwa katika hatua ya makundi dhidi ya mabingwa mara tisa wa Afrika, Al Ahly ambao pia ndio mabingwa watetezi.

Ratiba ile licha ya awali kuonekana kuwa ingekuwa ngumu sana kwa Simba, lakini imekuja kuwa ni muhimu sana kwao kuelekea kwenye mechi hizi za hatua ya juu ya mtoano.

Simba sasa itaingia katika hatua hii ya robo fainali ikijiamini kwa sababu imeshacheza mechi mbili na mbabe wa Afrika na kumfunga katika mechi iliyokuwa muhimu zaidi kwa kila mmoja wao.

Ndio Simba ilipoteza mechi ya marudiano dhidi ya Ahly lakini mechi hiyo haikuwa na umuhimu kwa sababu kila timu ilishajihakikishia nafasi yake kundini hivyo haikuwa na maana ya mechi ya kiushindani hasa - mechi ya kiushindani baina yao Simba walishashinda 1-0 Kwa Mkapa.

Kucheza mechi mbili dhi ya Al Ahly kilikuwa ni kipimo bora zaidi ambacho Simba walihitaji katika michuano hii. Hii inamaanisha kwamba Simba itakwenda katika hatua hizi za mtoano ikiwa haimhofii yeyote.

Tunawashauri wachezaji wasibweteke, wakomae maana huu ni mwaka wao.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz