Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lwakatare: Niling’angania shilingi ya Waziri bungeni hadi ruksa boda*2

63810 Pic+lwakatare Lwakatare: Niling’angania shilingi ya Waziri bungeni hadi ruksa boda*2

Mon, 15 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Spika alimkubali; zikaja sheria, kanuni Chanzo alikerwa na kilichojiri Kagera

KATI ya Jumatatu hadi Jumatano wiki hii, ilikuwa na sehemu tatu za makala hii kuhusuisafari ya kisiasa ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Wifred Lwakatare. EndeIea na sehemu yake ya mwisho ya mazungumzo hayo.

UNAJUA asili ya neno 'bodaboda'? Unajua kwamba liliwahi kusababisha shilingi ya Waziri kushikwa bungeni na kulitokea nini?

Mwanasiasa mwandamizi na Mbunge wa Bukoba Mjini anayestaafu, Wilfred Lwakatare, anasimulia chimbuko la usafiri huo wa pikipiki nchini ‘unaobeba’ ajira ya vijana wengi leo hii, ulivyosababisha mvutano mkali bungeni.

Faragha ya Nipashe na mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, anasimulia alivyoongoza hoja kuishinikiza serikali kufuta kodi ya kichwa.

Lwakatare, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), pia ana simulizi ya kinachomng'oa kutoka aliko sasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kurejea ‘nyumbani’ CUF. Fuatilia maelezo yake, kutoka maswali ya ‘Ana kwa Ana.’

SWALI: Kipi cha kihistoria unadhani kinabaki kumbukumbu kwako, bungeni na nje ya ubunge?

LWAKATARE: Ni mengi mno yanayobaki kama historia na nitajitahidi kutaja machache. Kumbuka nimekuwa mbunge vipindi viwili; kile cha 2000 hadi 2005 na 2015 hadi 2020. Kipindi cha 2000 hadi 2005 ninakiona kama kipindi nilichoacha kumbukumbu kubwa zaidi.

Kwanza, nikiwa bungeni nilijenga hoja ya kuhakikisha matumizi ya pikipiki kuruhusiwa kuanza kubeba abiria kibiashara. Ikumbukwe kwamba kabla ubebaji abiria kwa pikipiki haukuwapo kabisa, bali utaratibu huo ulikuwa zaidi nchini Uganda na mpakani mwa Kenya na Uganda.

Kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda (Mutukula), usafiri huu wa pikipiki ulikuwa zaidi ukiwavusha wafanyabiashara wa magendo ya bidhaa mbalimbali kati ya mpaka wa Tanzania na Uganda, kutoka pande zote mbili.

Hivyo, kwa kuwa usafiri huu uliwasafirisha abiria wao toka upande mmoja wa nchi na kuvuka kwenda upande wa nchi nyingine, usafiri huo wa pikipiki ukapewa jina la bodaboda.

Jina hilo limekuwa maarufu na kutumika hivyo hivyo hata kwa maeneo yasiyo na mpaka kati ya nchi na nchi. Imechukuliwa kama jina linaloakisi usafiri wa kukodi pikipiki.

Biashara hii ya usafiri wa pikipiki ilichangamkiwa sana na vijana wa upande wa Tanzania pale Mutukula na kwa kasi wakaingiza aina hiyo ya usafiri wa pikipiki kibiashara, mpaka mjini Bukoba ambako ni jimbo langu nilililokuwa nikiliwakilisha bungeni.

Biashara hiyo ilikumbwa na tatizo la kuzuiliwa na vyombo vya dola (polisi) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutokuwapo sheria ya kuruhusu pikipiki kubeba abiria kibiashara, pia malalamiko makubwa ya wafanyabiashara wa Taxi ambao waliona wameingiliwa kibiashara.

Vijana wengi waliojitosa katika biashara hiyo ya bodaboda, walipigwa na polisi barabarani, kuumizwa na kuangushwa barabarani na kuumia vibaya sana kwa kufukuzwa na 'defender' za polisi.

Wengi walinyang'anywa pikipiki zao na kurundikwa kwa mamia Kituo cha Polisi Bukoba. Hospitali ya Mkoa Kagera kuna wodi ilijaa vijana walioumizwa au kuvunjika au kuumizwa viungo vyao kwa kuanguka na pikipiki zao, pindi walipokuwa wakifukuzana barabarani.

Kama mbunge, niliona kuna haja kuingilia kati jambo hilo. Kwanza, pamoja na vurugu zote hizo, vijana hawakutaka kuiacha biashara hiyo, kwani ilikuwa ikiwaingizia kipato.

Hata walipokuwa wakinyang'anywa pikipiki hizo, haraka sana walikuwa wakiingiza pikipiki nyingine kutoka Uganda (zikijulikana kama bomba mbili).

Usafiri huo ulionekana kupendwa na kuwavutia watu wengi, kwa kuwa ulikuwa wa bei rahisi na uliweza kuwafikisha abiria mpaka mlangoni mwa makazi yao.

Niliwasilisha hoja bungeni nikiambatanisha na picha nyingi za majeruhi hospitalini na rundo la pikipiki kituo cha polisi. Kwa kuwa kilikuwa kipindi cha bajeti, nikaishikilia shilingi ya mshahara wa Waziri wa Mambo ya Ndani (wakati huo akiwa Omari Mapuri).

Nikaitaka serikali itoe maelezo juu ya unyanyasaji huo wa raia, pia kuitaka kuleta marekebisho ya sheria na kanuni juu ya vyombo vya kubeba abiria barabarani, pia Sheria za Usalama Barabarani.

Nimshukuru Spika (Pius) Msekwa alikuwa 'very much concerned' (aliguswa) na hoja yangu na kiti chake kikaungana nami kuibana serikali juu ya hoja hiyo.

Bila ajizi, wizara husika ikiwamo ile ya Mawasiliano na Uchukuzi iliyokuwa ikiongozwa na Profesa (Mark) Mwandosya na ya Mambo ya Ndani ya Mheshimiwa Mapuri, wakakubali kwenda kukaa na kufanya marekebisho ya sheria na kanuni.

Huo ukawa mwanzo wa mfumuko wa uingizwaji nchini maelfu ya kontena za pikipiki kutoka China na biashara ya usafiri wa pikipiki ikashamiri nchi nzima, vijijini, vitongojini na mitaani.

Hoja yangu moja tu ikatoa fursa ya kimapato kwa mamilioni ya watu; China hadi Tanzania. Ndani ya Bunge, ilifikia mahali kila nikisimama kuchangia hoja yoyote ninaitwa 'Mheshimiwa wa Bodaboda.' Ni muda wako wa kuchangia au kuuliza swali.

Ukweli ninajivunia kitu hiki hadi leo. Nikiona vijana nchi nzima wakikata mitaa barabarani wakisaka riziki wao wanasema 'kula vichwa', bila bugudha ninajisikia fahari na furaha kubwa.

Pii, nikiwa mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, nilianzisha na kuisimamia hoja iliyokuwa ikizungumzwa kwa nguvu kubwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ya ufutaji suala la kodi ya kichwa iliyokuwa ikiwadhalilisha watu wengi.

Ndani ya kamati, niliijengea hoja na kusababisha serikali kwenda kujipanga upya na matokeo yake wakakubali na kwenda kuvirekebisha vitabu vyote vilivyokuwa tayari vimechapishwa. Kwa anayebisha, aende kwenye nyaraka zinazowekwa kama kumbukumbu, atalishuhudia jambo hilo!

Tatu; nikiwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), nikiongoza vyama vitano; CUF, Chadema, TLP, UDP, NCCR- Mageuzi kwa kushirikiana na baraza langu kivuli lililokuwa likiundwa na wabunge mahiri kutoka vyama vyote (Dk. Slaa, John Cheyo, Hamad Rashid, Marehemu Philemon Ndesamburo, Freeman Mbowe), tulitengeneza kanuni na kukubaliwa na wabunge wote wa upinzani na zikanisaidia kuiongoza kambi kwa umahiri mkubwa na utulivu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live