Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lowassa alipendwa sana, aliumizwa, akaumiza wengi, hatasahaulika

Lowassa Deaddd).jpeg Lowassa alipendwa sana, aliumizwa, akaumiza wengi, hatasahaulika

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: mwanachidigital

Ukokotoaji umri, kuanzia Agosti 26, 1953 hadi Februari 10, 2024, ni miaka 71 kasoro miezi mitano na siku 16. Hizo ndizo namba za uhai wa mhusika anayejaza kurasa nyingi kwenye siasa za Tanzania.

Edward Ngoyai Lowassa. Wenye kumwita shujaa wa Monduli, heri yao. Wanaomtambua kama Leigwanan mashuhuri kwa Wamasai, ni utashi wao.

Utambulisho ambao haupingiki kwa yeyote ni kuwa Edward Lowassa ni binadamu. Kama ilivyo asili ya binadamu, kifo ni hatima mama. Utawasili duniani kwa kilio, wenye kukupokea watashangilia na kucheka. Utaondoka ukiwa kimya, watakaokusindikiza watahuzunika na kulia. Hiyo ni rasimu ya kila mja. Safari kutoka tumboni kwa mama, hadi umauti.

Edward, mwanasiasa aliyependwa mno na watu. Haiba yake sumaku, alivutia wengi. Ulimi wake urimbo, aliwanasa waliomsikiliza. Mtu wa mipango na mikakati, alifanikisha mengi kwenye siasa za Tanzania.

Alisimama kama kocha, akaiongoza timu kwa mafanikio hadi Rais wa nne Tanzania, Jakaya Kikwete, alipoingia Ikulu. Edward alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ushindi ya Jakaya, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Tofauti na kocha mchezoni ambaye hujielekeza kwenye ufundi, Edward alikuwa kocha tingatinga na akachonga barabara, kuhakikisha Jakaya anapita salama na anafika palipokusudiwa bila madhara.

Tingatinga linapochonga barabarani huumiza vingi. Edward aliumiza wengi. Walioutamani urais dhidi ya Jakaya, hawakusalimika. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na 2005, kuna wanasiasa walijeruhiwa kwa propaganda. Edward ni mbeba lawama!

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (mwaka 1990 – 1994), John Malecela, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, ilivumishwa alibadili dini kuwa Muislamu, akapewa fedha na Waarabu ili awe Rais.

Nilipata kumuuliza Malecela kuhusu uvumi huo wa kubadili dini, akajibu: “Ni Edward huyo.” Malecela alimtaja mwandishi wa habari veterani nchini Tanzania kuwa ndiye alitumiwa na Edward kueneza hizo propaganda.

Waziri Mkuu wa Tanzania (mwaka 1995 – 2005), Fredrick Sumaye, aliunguzwa na moto mkali wa propaganda za kisiasa, alipoujaribu urais mwaka 2005. Alibebeshwa mizigo mingi ya kashfa na majina yenye kumuumiza yeye na familia. Sumaye aliitwa mla rushwa aliyejitajirisha kwa uwaziri mkuu.

Ulifika wakati Sumaye aling’aka, akaushambulia mtandao wa Jakaya, ulioongozwa na Edward kuwa waliusaka urais kwa kuchafua na kuumiza wengine. Zingatia, tingatinga likichonga barabara, vingi huumia. Edward alikuwa tingatinga.

Sumaye tena, mwaka 2012, alijitokeza kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (Nec) CCM. Kutoka Hanang, Manyara, sauti ya Sumaye ikasikika akilalamika kuchezewa rafu na Edward, hadi akakosa ujumbe wa Nec. Hii ilikuwa vita ya urais 2015.

Waziri Mkuu wa Tanzania (mwaka 1984 – 1985), Dk Salim Ahmed Salim, baada ya utumishi wake uliotukuka kimataifa, akitokea kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), alifanya majaribio ya kushinda urais mwaka 2005.

Dk Salim, Rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa katika miaka tofauti, alipochukua fomu CCM, kuomba kuwa mgombea urais, alinyukwa kwa kashfa za kutisha. Aliitwa Hizbu na akapigwa kashfa nzito kuwa ndiye alimuua Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Maumivu ya Dk Salim hayaelezeki. Kutoka binadamu aliyeimbwa na wasifu wake kuwa somo la kufundishia shuleni, hadi kuitwa majina mabaya kisa kujitokeza kuwania urais. Dk Salim alisema: “Nimegundua kugombea urais Tanzania ni aina nyingine ya kujivunjia heshima.”

Nyuma ya maumivu ya Dk Salim, jina la Edward lilitajwa kwa sababu timu aliyoiongoza kumpeleka Jakaya Ikulu, ilitajwa kuwa mpishi wa kila kashfa na tuhuma zilizoelekezwa kwa Dk Salim. Edward aliumiza wengi.

Anne Kilango Malecela, aliposhindwa ubunge, Same Mashariki, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, lawama zote zilielekezwa kwa Edward, kwamba alitumia gia kubwa kumwondoa bungeni. Vivyo hivyo kwa mumewe, Malecela, aliposhindwa kura za maoni, jimboni kwake Mtera mwaka 2010.

Christopher Ole Sendeka, alipopoteza ubunge jimbo la Simanjiro, mwaka 2015, Edward alitajwa kuwa sababu. Samuel Sitta, alipokwama kutetea kiti cha Spika wa Bunge mwaka 2010, alilalamika kuwa alidhibitiwa na mafisadi. Alimaanisha Edward na timu yake.

Bernard Membe, alipotoka wa mwisho, katika tano bora iliyopenya Nec, kuelekea kumpata mgombea urais CCM mwaka 2015, Edward alitajwa kumchezea rafu. Vivyo hivyo, kwa January Makamba, aliyetoka wa nne na kushindwa kupenya kwenda Mkutano Mkuu CCM, kwa hatua ya mwisho kumpata mgombea urais.

Pius Msekwa, alijitokeza kuwania uspika wa Bunge mwaka 2005 akiwa na matumaini makubwa. Aliondoka ukumbini akiwa na maumivu baada ya kushindwa na Sitta. Nyuma ya ushindi ya matokeo hayo, alikuwepo Edward, ambaye alihamasisha “wanamtandao” kumchagua Sitta.

Aliumizwa sana

Edward ni muundaji wa taswira ya siasa zilizopo Tanzania, zilizochipua mwaka 1995 na kupata uga mpana mwaka 2005. Siasa za kuunda mtandao na kuunganisha nguvu. Edward alianza kwa kushirikiana na Jakaya.

Ni Edward aliyemshawishi Jakaya kuunda timu ya pamoja na alipofanikiwa, wakawa wanasiasa mapacha. Edward alipokatwa jina kwenye mbio za kuwania tiketi ya CCM ya kuwa mgombea urais mwaka 1995, hakulalamika, alielekeza nguvu zake zote kwa Jakaya. Na hatua ya mwanzo, walishinda.

Jakaya aliongoza kwa kura lakini hakufikisha asilimia 50, hivyo mchuano wa wawili ukarejewa dhidi ya Benjamin Mkapa, ambaye alishinda na kutangazwa kuwa mgombea wa kiti cha urais.

Inatoa majibu kuwa Edward alikuwa mwaminifu kwenye makubaliano. Mwingine angepata kinyongo baada ya jina lake kukatwa, mwenzake akafanikiwa kupenya. Edward alisimamia malengo mpaka mwisho. Alikuwa askari wa kutumainiwa na yeyote waliyeunda jeshi la pamoja.

Ni sababu, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Edward aliamua kujiweka kando kwenye uchukuaji fomu CCM. Alijitoa kwa ajili ya Jakaya. Lawama nyingi kuwa alicheza sana rafu kumpeleka Jakaya Ikulu inadhihirisha Edward ni aina ya mchezaji aliye tayari kupewa kadi nyekundu kwa ajili ya kufanikisha ushindi wa timu yake.

Baada ya mambo mengi waliyofanya pamoja, Jakaya alishinda urais. Edward akawa Waziri Mkuu. Ilipoibuka kashfa ya Richmond, Jakaya hakumkingia kifua, alimwacha wimbi limzoe hadi kumtupa nje ya uwaziri mkuu. Edward aliumizwa na kujiona amesalitiwa.

Martin Luther King Jr alipata kusema: “In the end, we will remember not the words of our enemies, but the silence of our friends.” – “Mwishoni, hatutakumbuka maneno ya maadui zetu, bali ukimya wa marafiki zetu.”

Siku ilikuwa Alhamisi, Februari 7, 2008, Edward alitangaza kumwandikia barua Rais (Jakaya) ya kujiuzulu uwaziri mkuu. Alitangulia kusema: “Kuna matamanio ambayo nitayatimiza. Ni uwaziri mkuu. Tatizo ni uwaziri mkuu.” Edward aliumizwa kuwa kuna watu waliuonea kijicho uwaziri mkuu wake wakati aliuvujia jasho. Hakuna aliyemtetea. Jakaya alikaa kimya.

Edward aliumizwa sana na Sitta. Fikiria walikuwa kwenye mtandao mmoja. Wamefanikiwa. Baada ya safu kujipanga, inaibuka hali ya kutoelewana kati ya waziri mkuu na spika. Kisha, Sitta aliunda kamati iliyochunguza kashfa ya Richmond. Kamati hiyo ikamning’iniza Edward.

Aliposema “tatizo ni uwaziri mkuu”, tafsiri ilikuwa moja tu; Sitta. Kwamba mwanamtandao mwenzake huyo hakutosheka na uspika, akawa anahitaji uwaziri mkuu wa Edward. Matamanio hayo ya uwaziri mkuu ndiyo yalisababisha mzozo mkubwa wa kisiasa bungeni.

Edward alikuwa binadamu. Bila shaka aliumizwa pale mtu aliyempigania kuingia Ikulu (Jakaya), aliyeongoza kikao cha kumkata jina. Tena, Jakaya akapambana juu chini kuhakikisha Dk John Magufuli, ambaye alikuwa mpinzani wa Edward, ashinde urais.

Makada vijana wa CCM, Nape Nnauye na Paul Makonda, kwa nyakati tofauti, walikuwa mwiba kwa Edward. Walimshambulia majukwaani na hata kwenye mikutano na waandishi wa habari. Vijana hao, Jakaya aliwapa vyeo serikalini na kwenye chama. Haikuhitaji afungue kinywa ndipo ifahamike kuwa Edward aliumizwa.

Alipokuwa anaweka sawa mipango yake ya urais mwaka 2015, Edward alikuwa na timu pana. Baada ya kukatwa CCM na kuamua kujiunga na Chadema, watu wake wengi wa karibu walibaki CCM na walisimama jukwaani kumnadi Magufuli.

Alipendwa sana

Haiba ya Edward ilimfanya awe na nguvu kubwa ya ushawishi. Kishindo chake alipokuwa anafanya ziara mkoa kwa mkoa kutafuta wadhamini, vilevile mafuriko ya watu katika mikutano yake ya kampeni, ni kipimo sahihi kuthibitisha kuwa alipendwa sana.

Edward hatasahaulika. Uhusika wake kwenye siasa za nchi, umemfanya akose mfanowe. Kwa ujenzi wa shule za kata za sekondari nchi nzima, kutoa maji Ziwa Victoria hadi mikoa ya Shinyanga na Tabora, iliyokuwa na uhaba mkubwa. Edward anasahaulikaje?

Columnist: mwanachidigital