Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Liwalo na liwe! Simba, Yanga

Chama Aziz Liwalo na liwe! Simba, Yanga

Sat, 25 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Liwalo na liwe lazima kieleweke. Unaweza kusema ni vita ya kufa au kupona kwa Simba na Yanga ambazo leo na kesho zinakabiliwa na mechi ngumu za raundi ya tatu ya hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

Simba iliyopo katika kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika, leo kuanzia saa 1:00 usiku, inakabiliwa na mchezo mgumu na muhimu kwenye Uwanja wa St. Mary’s, Uganda dhidi ya wenyeji wao, Vipers ambao inalazimika kuibuka na ushindi ili kuweka hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali.

Baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Horoya na Raja Casablanca, ushindi wa leo dhidi ya Vipers yenye pointi moja, ndio unaweza kuibakisha Simba na matumaini ya kusonga mbele, vinginevyo shughuli yao inaweza kuishia hapo. Baada ya mechi hiyo, kesho kuanzia saa 1:00 usiku, watani wao Yanga watakuwa na shughuli mbele ya wenyeji wao, Real Bamako ya Mali, mechi ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa 26 Mars.

Ushindi katika mchezo huo wa ugenini, unaweza kuifanya Yanga iongoze kundi D la mashindano hayo kutegemeana na matokeo ya mchezo baina ya TP Mazembe na Monastir lakini kubwa zaidi utaiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali.

MAREFA HAPO JIRANI TU

Refa kutoka Msumbiji, Celso Alvacao (33) ndiye amepewa jukumu la kushika filimbi katika mchezo baina ya Vipers na Simba akisaidiwa na Wamakonde wenzake, Arsenio Marengula, Teofilo Mungoi na Simoes Guambe.

Mwamuzi Alvacao hana historia nzuri na Simba kwani ndiye alichezesha mechi ambayo walilala mabao 2-1 ugenini dhidi ya Red Arrows ambayo ilikuwa ya marudiano ya hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita. Katika mechi 11 za mashindano ya klabu Afrika ambazo refa huyo amechezesha, ametoa kadi 43 ambazo njano ni 42 na moja nyekundu.

Kwa upande wa Yanga, mechi yake ya ugenini dhidi ya Real Bamako itachezeshwa na marefa kutoka Botswana wakiongozwa na mwamuzi wa kati, Joshua Bondo (44) atakayesaidiwa na Mogomotsi Morakile, Kitso Sibanda na Tshepo Gobagoba.

Bondo ni refa mwenye kumbukumbu nzuri na klabu za Tanzania ingawa amekuwa anapenda kumwaga kadi. Mechi mbili ambazo amewahi kuchezesha klabu za Tanzania, zilipata ushindi na katika mechi 10 zilizopita, ametoa kadi 45 ikiwa ni wastani wa kadi 4.5 kwa kila mechi ambapo kati ya hizo, kadi za njano ni 43 na mbili zikiwa nyekundu.

VIWANJA VYEPESI KINOMA

Uwanja wa St. Mary’s utakaotumiwa kwa mechi baina ya Vipers na Simba na ule wa 26 Mars ambao utachezwa mechi baina ya Real Bamako na Yanga, havina takwimu za kutisha kwa timu ngeni jambo ambalo linapaswa kuwafanya wawakilishi hao wa Tanzania kutoingia na hofu katika mechi zao hizo.

Vipers imecheza mechi 10 za mashindano ya Klabu Afrika kwenye Uwanja wake wa St. Mary’s ambapo imeshinda mechi nne tu, ikitoka sare nne na kupoteza mbili huku ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.

Kwa upande wa Uwanja wa 26 Mars, wenyeji Real Bamako katika mechi 16 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika wamepata ushindi mara tano tu, wakitoka sare katika mechi nane na kupoteza michezo mitatu huku ikifumania nyavu mara 18 na wenyewe wamefungwa mabao 12.

NAMBA ZIHESHIMIWE

Matokeo ya mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Simba na Yanga zilicheza ugenini yanapaswa kuzilazimisha timu hizo kucheza kwa nidhamu kubwa na kujituma vilivyo katika mechi za leo na kesho ili ziweze kupata matokeo mazuri dhidi ya Vipers na Real Bamako.

Simba katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo ilikuwa ugenini, imepata ushindi mara tatu, sare moja na imepoteza michezo sita huku ikifunga mabao tisa na nyavu zake zimetikiswa mara 15.

Yanga yenyewe ugenini imeshinda mechi tatu na imepoteza saba na imefunga mabao saba huku yenyewe ikiruhusu kufungwa mabao 14.

MAYELE, PHIRI WABEBA JAHAZI

Nyota wawili wanategemewa zaidi na Simba na Yanga kuzibeba katika mechi zao za raundi hii kutokana na takwimu bora za ufungaji ambazo wamekuwa nazo katika mashindano ya klabu Afrika.

Moses Phiri amebeba matumaini ya Simba katika mchezo wa leo dhidi ya Vipers kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu ambapo katika mabao manane ya Simba iliyopachika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, yeye amefunga mabao matano peke yake.

Kwa upande wa Yanga, matumaini yao ni Fiston Mayele ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga na kupiga pasi za mwisho ambapo katika mabao 14 ya Yanga katika mashindano ya Klabu Afrika msimu huu, amehusika na mabao tisa, akifunga saba na kupiga pasi mbili zilizozaa mabao.

VIKOSI HIVI HAPA

Kikosi cha Simba katika mechi ya leo kinaweza kupangwa hivi: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin, Moses Phiri, Jean Baleke na Clatous Chama.

Yanga kinaweza kuwa na Djigui Diara, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Mudathir Yahya na Kennedy Musonda.

Hata hivyo, vikosi hivyo vinaweza kubadilika kutegemeana na mitazamao ya makocha wa timu hizo mbili.

MATUMAINI KIBAO

Yanga na Simba kwa nyakati tofauti zimeonyesha kujiamini kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini.

Beki wa Simba, Mkenya Joash Onyango alisema kama wachezaji wameongea na kuweka mipango yao ambayo yote inalenga ushindi huku wakikumbuka mechi mbili za mwanzo walizopoteza.

“Tumepoteza mechi mbili mfululizo jambo ambalo sio la kawaida kwetu, wachezaji wote tumezungumza na kukubaliana kutopoteza tena na kampeni hiyo tutaianza kwenye mechi ya Vipers kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele. Tumehimizana kujitoa kwa kadri ya uwezo ili kufikia lengo,” alisema Onyango.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema: “Kundi bado liko wazi na timu yoyote inaweza kufuzu robo fainali. Ushindi katika mchezo huu ni muhimu kwani utatuweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo yetu hivyo tumejiandaa kikamilifu.”

Columnist: Mwanaspoti