Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Lionel Messi amevipiga vita vilivyo vizuri, imani ameilinda

Lionel Messi Psg C961s9vxza14z255h31atpkd Lionel Messi

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nimesoma mahali PSG wamegawanyika katika suala la Lionel Messi. Mkataba wake na PSG unatamatika mwisho wa msimu huu na bodi imegawanyika kuhusu kumwongezea mkataba mpya. Lipo kundi linalohitaji aondoke na wapo wanaotaka asalie.

Mwezi Juni mwaka huu Messi anatimiza miaka 36. Mshale wa saa unakimbia sana. Leo Messi siyo mtoto tuliyemwona akifanya miujiza Catalunya na jezi ya Barcelona. Uzee umemfika na sasa eti kuna watu hawamhitaji katika timu yao.

Mwandishi mmoja wa gazeti hili hupenda kuuliza, zama zimekwenda wapi? Yule Messi aliyewapa ubatizo wa moto mabeki wa timu pinzani na kuwatesa makipa eti leo kuna timu haimtaki? Mambo hufika mwisho.

Ukweli ni, Messi sio yule tena. Miguu yake imechoka na akili yake haifanyi kazi kwa haraka mara mbili zaidi ya wachezaji wengine kama ilivokuwa zamani. Sambamba na akili hata moyo wake wa soka nao umechoka na umekinai mafanikio.

Nilikuwa namtazama katika pambano la pili la UEFA dhidi ya Bayern Munich, moyo wa Messi hauna kiu tena ya mafanikio. Ukimtazama usoni na namna alivyokuwa anacheza unaona kabisa hana hofu hata kama wataondoshwa. Ni tofauti na alivyokuwa Barcelona. Moyo wake wa mapambano aliuacha Catalunya. Ni kama vile PSG alienda kula pensheni.

Inawezekana bado miguuni kwa Messi kuna vitu kadhaa lakini tatizo huyu ni Messi na watu wakimtazama wanataka kumuona yule hatari wanaliyemkariri kichwani. Inawezekana Messi akafunga mabao idadi sawa na Karim Benzema- watu wakaridhika na alichokifanya Benzema na wakasikitishwa na Messi.

Hiki ndicho kinachosababisha baadhi ya watu ndani PSG wasimtake. Klabu ambayo haijatwaa hata taji moja la Ulaya huku yeye akiwa amelitwaa mara nne. Ni kwa sababu vichwani mwao wana ile sura ya Messi aliyewafunga Manchester United katika fainali ya Ulaya.

Lakini hapo kuna tatizo lingine la uchumi. Messi ni kati ya wachezaji wanaovuta pesa nyingi zaidi pale PSG. Yeye na swahiba wake Neymar sambamba na Kylian Mbappe. PSG wanatamani kumpunguza ili kuweka sawa vitabu vyao vya fedha. Hakuna sababu ya kumlipa pesa nyingi kama hawezi kuwasaidia kushinda klabu bingwa Ulaya.

Kwa inavyoonekana itakuwa ngumu sana kwa PSG kumbakiza Messi. Swali ni wapi ataak baada ya Paris? Nasikia Barcelona wanataka kumrudisha Catalunya. Mashabiki wengi wa Barcelona bado wanampenda Messi na rais Joan Laporta anataka Messi arejee kuivaa jezi ya Barca walau kwa mara ya mwisho.

Barcelona wanaitamani nafasi ya mwisho ya kumuaga Messi vizuri zaidi. Kumbuka Messi alifanya kila alichoweza kuhakikisha anabaki Barcelona lakini wakati ule kulikuwa na mvutano mkubwa katika uongozi. Tatizo kubwa la kumrejesha Messi kwa sasa Barcelona litakuwa kwa kocha. Inawezekana mashabiki na viongozi bado wanampenda lakini sidhani kama yupo kocha Ulaya anayetamani kufanya kazi na Messi.

Kama nilivozungumza hapo awali, Messi si mshindani tena uwanjani. Xavi anaweza kuwa rafiki mkubwa wa Lionel Messi lakini sidhani kama atapenda kuwa kocha wake nyakati hizi ambazo jua linaelekea utosini.

Binafsi naamini sehemu sahihi zaidi kwa Lionel Messi kwenda miaka hii ni kule kwa Waarabu au Marekani. Ligi za kule siyo ngumu kama Ulaya. Bado atawezana na mikiki ya huko na ataendelea kutazamwa kama staa wa ligi tofauti na Ulaya ambayo inatawalia na vijana wenye damu changa.

Kule kwa waarabu atavuna pesa nyingi ambazo hakuna sehemu yoyote ya dunia itaweza kumpatia. Ni kweli Messi amechuma noti za kutosha Ulaya na ni tajiri mkubwa. Lakini waarabu wanaweza kumlipa pesa ambayo hajawahi kulipwa katika maisha yake yote ya soka. Ni vema akaenda kupumzika huku akifurahia kitita kikubwa cha pesa kinachoingia katika akaunti yake kila wiki.

Hakuna kitu kipya anachokihitaji katika maisha yake ya soka tena akizingatia ukweli kwamba ameshinda kila kitu hadi Kombe la Dunia ambalo mpinzani wake Ronaldo hajafanikiwa kulitwaa. Aende kupumzika sasa.

Columnist: Mwanaspoti