Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ligi ya mabasi Ligi Kuu Bara

KMC Yapokea Basi Lenye Thamani Ya Mil. 400 Ligi ya mabasi Ligi Kuu Bara

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna mambo mengi sana yanachangia maendeleo ya timu za soka duniani, timu kubwa zote zimekuwa na maendeleo baada ya kujiweka sawa kwenye miundombinu yao.

Timu nyingi za Ligi kwa sasa zimeanza kuamka kwa kufanya mambo makubwa, kuna timu kadhaa zinamiliki viwanja, nyingine zina ofisi bora na kadhalika.

Leo tunazitazama timu ambazo zinamilika mabasi yao wenyewe ambayo ni maalumu kwa ajili ya kupeleka wachezaji wao mazoezini na kusafiri umbali mrefu kwenda kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Kuna ambazo zinamiliki mabasi lakini siyo yenye hadhi kwa ajili ya kwenda umbali mrefu, lakini zinakuwa hazina jinsi kutokana na hali yao ya uchumi, inaelezwa kuwa Azam FC ndiyo timu inayomiliki gari la bei ghali zaidi na la kisasa kuliko mengine yote kwenye ligi kwa sasa:

AZAM FC

Hii ni timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye ligi ikiwa inaonekana kukua kila siku, msimu huu ilikuwa inapewa nafasi ya kuchukua ubingwa kutokana na usajili ambao wamefanya, lakini hadi sasa ikiwa imebakiza michezo sita tu ipo nyuma ya vinara kwa zaidi ya pointi 20.

Timu hii inamiliki gari la kisasa zaidi aina ya Mercedes Irizar ambalo inaelezwa lilinunuliwa kwa zaidi ya Sh 900 Milioni mwaka juzi likiwa linatajwa kuwa basi la kisasa zaidi kwa timu ya soka hapa nchini.

YANGA

Hii ni timu ambayo kwa sasa inatawala soka la Tanzania, ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita na sasa ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 62 zikiwa ni nane mbele ya Simba ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Yanga wanamiliki basi la kisasa aina ya Tata likiwa limetengenezwa na kampuni maarufu ya mabasi Marcopolo na Yanga walikabidhiwa mwaka juzi, likiwa linaelezwa kuwa ni basi la bei mbaya, pia kinachovutia zaidi ni rangi zilizopangwa kwenye basi hilo, lakini wachezaji wakisifu kuwa lina nafasi kubwa ndani ambayo inawafanya wachezaji kulaza viti na wanaweza kulitumia kwa safari ndefu bila kizuizi chochote.

SIMBA

Msimu huu hawapo kwenye kiwango bora sana wakiwa wanashika nafasi ya pili tofauti ya pointi nane na Yanga, pia wakiwa bado hawajawika sana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika walipoteza michezo yao miwili ya mwanzo.

Pamoja na kumiliki basi zuri na la kisasa ambalo walikabidhiwa mwaka juzi na kampuni ya Africaries ni basi la kisasa likiwa limetengenezwa na kampuni ya Marcopolo ambalo haliwachoshi wachezaji hata kama watakuwa kwenye safari ndefu kutokana na umbali wa kutoka kiti kimoja kwenda kingine, inaelezwa kuwa lina thamani ya zaidi ya Sh 500 milioni.

SINGIDA BS

Hii ni timu changa kwenye Ligi, huu ukiwa ni msimu wake wa kwanza, lakini tayari imeonyesha upinzani mkubwa sana ikiwa nafasi ya nne kwa sasa kwenye ligi, lakini ikiwa ni timu ambayo ilifanya usajili bora zaidi msimu huu.

Tayari Singida wameonyesha tofauti yao na timu kadhaa za ligi hiyo wakiwa wanadhaminiwa na Kampuni ya GF Trucks ambayo ndiyo iliwapa basi la kisasa lililotengenzwa na kampuni ya Dragon ambalo wanatumia sasa likiwa na vigezo vyote vya kutumiwa na mastaa wa ligi hiyo, pamoja na kwamba walikuwa wanalitumia kuanzia wakiwa Championship.

MBEYA CITY

Hii ni timu inayomilikiwa na Halmshauri ya Mbeya, ikiwa ni moja ya timu yenye mashabiki wengi na miaka mitatu nyuma ilitikisa sana kwenye ligi pamoja na kwamba sasa haina matokeo mazuri sana, wanashika nafasi ya 10 na pointi 27.

Mbeya City wanamiliki basi lililotengenezwa na Kampuni ya Marcopolo, walipewa mwaka 2015 na mdhamini wao Nassor Bin Slum ambaye anaendelea kuwadhamini hadi sasa, linatajwa ni basi la kisasa maalum kwa ajili ya safari ndefu na gharama yake ni zaidi ya Sh 400 milioni.

IHEFU

Hii pia ni timu changa kwenye Ligi Kuu Bara lakini imeonekana kukua kwa kasi zaidi kwa siku za hivi karibuni baada ya kuanza msimu huu vibaya.

Ihefu pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wengi mastaa ambao wameshatumika kwenye timu za Simba na Yanga, lakini ni kati ya timu ya mkoani ambayo inamiliki basi la kisasa.

Timu hiyo ipo nafasi ya nane na kwa mujibu wa taarifa basi lao lilinuliwa kwa kitita cha milioni 330 ni moja ya magari ya kisasa ambayo ni sahihi kwa safari za mbali na karibu kwa wachezaji wakiwa wamelitumia kabla hata hawajapanda daraja.

NAMUNGO

Hii ni kati ya timu ambayo inamiliki uwanja wake mwenyewe wa kisasa ambao wanaweza kuutumia hata michezo ya usiku, ikiwa kwa sasa inapambana kwenye Ligi baada ya kujikusanyia pointi 32 katika nafasi ya saba.

Timu hiyo hivi karibuni ilikabidhiwa basi jipya lilitengenezwa na kampuni ya Dragon ambalo ilielezwa kuwa lilitolewa na wadau wa soka wa mkoa wa Lindi, hata hivyo hii inakuwa timu ya kwanza ya mkoani kumiliki mabasi mawili ya kisasa kwa ajili ya wachezaji wao kwa kuwa mwanzoni walikuwa na basi lingine la kisasa.

Hii inatajwa kuwa kati ya timu yenye wadhamini wengi kwenye Ligi msimu huu.

KMC

Hii ni timu nyingine ambayo inamilikiwa na Halmashauri, wakiwa chini ya Wilaya ya Kinondoni na ikiwa ni timu ambayo imekuwa ikipewa matarajio makubwa sana kila msimu wa ligi lakini msimu huu hali yao siyo nzuri.

KMC ipo nafasi ya 13 na pointi 23 ikiwa haipo nafasi nzuri ya kubaki ligi na hivi karibuni ilikabidhiwa basi safi la kisasa ambalo wakati linazinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amosi Makala alisema ni la mkopo kutoka benki ya NBC. Inadaiwa kuwa na thamani ya Sh 450 milioni.

GEITA GOLD

Baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika, Geita waliuza wachezaji wengi sana wa kikosi cha kwanza na hali ya mashaka ilitua kwenye timu hiyo, lakini wameendelea kuwa bora kila siku na sasa timu hiyo inashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 34 wakiwa na uhakika mkubwa wa kubaki kwenye ligi.

Basi hilo la Kampuni ya Marcopolo walikabidhiwa mzunguko huu wa pili na wadhamini wao na siku ya kwanza tu walikwenda nalo Lindi kucheza na Nanungo, na wachezaji kulisifia kutokana na ubora wake.

Timu nyingine zenye magari ya kisasa ni Dodoma Jiji na Kagera Sugar.

Daktari wa Polisi Tanzania, Richard Yomba anasema kwa timu za Ligi Kuu zinashauriwa kuwa na mabasi ya kisasa kwa kuwa nyingi zina safiri umbali mrefu na wachezaji hawatakiwi kujikunja muda mwingi.

“Ukisafiri kwa Coaster timu inatakiwa kufika mapema na kupata muda wa kupumzika muda mrefu kwa kuwa wachezaji wanakuwa wamekunja miguu muda mrefu, magari ya kisasa ni muhimu ili wachezaji wapate na muda wa kulaza siti ili wapumzike ndiyo maana ukiona basi la Polisi Tanzania mambo yote hayo yamezingatiwa.”

Columnist: Mwanaspoti