Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ligi Kuu ya Saudia utitiri wa fedha

Mane X Ronaldo.jpeg Ligi Kuu ya Saudia utitiri wa fedha

Sun, 6 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mwezi wa Novemba mwaka 2022, dunia ikisubiri Kombe la Dunia la majira ya baridi kwa mara ya kwanza na pia Kombe la Dunia likichezwa kwa mara ya kwanza katika bara la Arabia au Ghuba kama wanavyopenda kuitwa; Kombe la Dunia la Qatar 2022.

Mchezaji mkongwe wa Manchester United, Mreno Cristiano Ronaldo anawatolea uvivu waajiri wake kwa maneno makali ya shombo yasiyovumilika. Zinaanza tetesi kumhusu nyota huyo aliyerejea kwa mashetani wekundu akitokea Juventus na Real Madrid ambako akiwa na mabwana weupe wa Madrid alishinda karibu kila kitu katika Hispania, Ulaya na Dunia nzima.

Mwanzoni tetesi zilitaja Chelsea na klabu kadhaa vya Ulaya lakini baadaye ikatajwa klabu ya Al-Nasri ya Saudi Arabia, tetesi zilizoibuka kuwa kweli na kuushangaza ulimwengu wa kandanda.

Kombe la Dunia linaanza, kundi la C lilikuwa na waliokuja kuwa mabingwa Argentina, Mexico, Saudi Arabia na Colombia. Saudi Arabia inafanikiwa kuifunga Argentina na nyota wao Lionel Messi kwa mabao 2-1 katika mchezo wao wa kwanza. Ni ushindi ulioishangaza dunia na hata Saudia wenyewe kiasi cha kutangaza siku iliyokuwa inafuata kuwa siku ya mapumziko kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Saudi Arabia iliendelea kugonga vichwa vya habari katika ulimwengu wa kandanda kwa wachezaji wengi waliomfuata Cristiano Ronaldo na kisha wimbi kubwa linaloendelea katika usajili wa majira haya ya kiangazi.

Siyo kwamba ni mara ya kwanza wachezaji kutoka ligi kubwa za Ulaya kwenda kucheza sehemu nyingine kama Arabuni, Marekani na Uchina. Ni mara ya kwanza wachezaji wa Ulaya na pia wataalam wa ufundi wanaondoka kwa wingi huu na kiasi kikubwa cha pesa kikihusishwa katika uhamisho na kandarasi zao.

Ligi Kuu ya Saudia (Saudi Pro League) imekuwepo tangu mwaka 1976; ni ligi ambayo ilikuwa haisikiki sana kabla ya ujio wa Cristiano Ronaldo. Hata hivyo,hilo haliondoi ukweli kwamba ligi hiyo imekuwa na fedha kitambo japo si kwa kiwango cha sasa. Ni ligi ambayo imekuwa na matamanio ya kufika juu.Kumwajiri mtendaji Garry Cook ambaye ana uzoefu mkubwa akiwa na Kampuni ya Nike na klabu ya Manchester City ni ishara tosha kwamba ligi hiyo ina maono makubwa kimataifa.

Labda swali linalowasumbua baadhi ya watu ni je pesa zinazotumiwa na klabu za Saudia zinatoka wapi? Pesa haijawahi kuwa tatizo sana kwa nchi za ghuba zenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi asilia. Hata kabla ya wimbi hili la wachezaji kwenda Uarabuni tayari mpira umeshaonja pesa nyingi sana zinazotoka kwenye mafuta ya Uarabuni.

Manchester City ya England inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na Abu Dhabi United Group ya Sheikh Mansour Bin Zayed Bin Sultan wa Abu Dhabi-Emirati, PSG ya Ufaransa inaendeshwa na Qatar Sports Investments ya Qatar, Arsenal wanauza haki za jina la uwanja wao kwa shirika la ndege la Emirates, Madrid wana udhamini mnono wa shirika la ndege la Emirates wakati Newcastle United inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na mfuko wa taifa wa uwekezaji wa Saudi Arabia (PIF), mfuko huo uko chini ya mtawala mwana mfalme Bin Salman.

Mfuko wa PIF unaomiliki 80% ya Newcastle United unahusika sana katika manunuzi ya wachezaji kuelekea Saudi Arabia kwani mfuko huo una hisa za udhibiti katika klabu za Al Ittihad ya N’Golo Kante na Karim Benzema, Al Ahli iliyomchukua kipa Mendy wa Chelsea na Senegal na pia Firminho kutoka Liverpool, Al Nassr ya Ronaldo na Al Hilal iliyo na Ruben Neves, Kalidou Koulibaly na pia inamfukuzia Kylian Mbappe wa PSG.

Kampuni ya mafuta ya Saudia, Aramco pia ni kati ya kampuni za serikali zilizotia mzigo wa fedha katika ligi hiyo ya Saudi Pro.

Makocha na mabenchi ya ufundi pia yameimarishwa kwa kiwango ambacho hakina tofauti na ligi za Ulaya. Al Ettifaq wanaye Steven Gerrard kutoka England, Mreno Nuno Espirito Santo aliyewahi kuifundisha Wolves kwa mafanikio yuko Al Ittihad na Mkroashia Slaven Bilic aliyecheza na kufundisha West Ham FC ya London, Uingereza na pia timu ya taifa lake la Croatia sasa anafundisha Al Fateh FC.

Malengo ya klabu na utawala wa Saudi Arabia ni kuziwezesha kampuni ambazo zinabinafsishwa kwa kiasi fulani kutengeneza pesa kupitia mpira wa miguu. Saudi Arabia inapambana kuhakikisha ligi yao inakuwa moja ya timu 10 bora duniani.

Pia Saudi Arabia ina mpango wa kuomba kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2030 hivyo taswira ya ligi yake inaweza kupeleka ujumbe ambao utaupa ufalme huo kura za kutosha kuwa mwenyeji wa mashindano hayo maarufu pengine kuliko yote duniani.Ni muhimu pia kujua kuwa kwa muda mrefu Saudi Arabia imekuwa kwenye vyombo vya habari kwa kunyoshewa vidole kama nchi inayoendeshwa kiimla.

Karibuni, utawala wa Saudia ulilaaniwa kwa namna unavyoshughulika na wakosoaji. Kifo cha mwandishi na mwanaharakati Jamal Kashogi nchini Uturuki kilihusishwa moja kwa moja na mtawala mwanamfalme Bin Salman.Ligi yenye mafanikio ya Saudia sasa inaweza kuwa kwenye vyombo vya habari zaidi kuliko siasa za nchi hiyo.

Ni nini matokeo ya mafuriko haya ya wachezaji kuelekea Saudia? Hili ni swali linaloumiza vichwa vya wafuatiliaji wengi wa mpira wa miguu.Changamoto kubwa inaweza kuwa kwa klabu za Ulaya ambazo zimejikuta zimefungwa mikono linapokuja suala la matumizi ya fedha kwani sheria za Ulaya zinaweka ukomo wa matumizi kitu ambacho hakipo kwa wenzao wa Saudia.

Kuibuka kwa ligi ya Saudi Arabia kunaweza kuathiri uwekezaji mkubwa katika mpira ambao Ulaya imekuwa ikipata kutoka mataifa ya Ghuba na Asia kwa ujumla.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, utitiri wa fedha wa Saudia hauwezi kuuacha mpira wa miguu ukiwa uleule. Nani atapata na nani atapoteza ni suala la kusubiri na kuona. Litakuwa jambo zuri ikiwa mwisho wa siku mpira wa miguu utaibuka mshindi.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Columnist: Mwanaspoti