Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kylian Mbappe na unahodha feki wa zama za kisasa

Mbappe Captain Game Kylian Mbappe

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Robert Pires anaishi katika dunia gani? Sijui. Huwa anafungua mdomo wake mara chache kuzungumzia soka na huwa namsikiliza. Majuzi alifungua mdomo wake kuzungumzia soka lakini alichozungumza sikukielewa kidogo na nikajikuta najiuliza, Pires anaishi dunia gani?

Pires alikuwa akilalamikia uamuzi wa kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps kumpa unahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe badala ya kumpa staa mwingine wa kikosi hicho, Antoine Griezmann. Pires ameshindwa kuishi katika dunia mpya ya soka na bado ameendelea kuishi katika dunia ya zamani ya soka.

Katika dunia ya zamani Pires yupo sahihi kwa asilimia zote. Alichosema ndio ukweli. Griezmann, katika umri wa miaka 32 alikuwa staa mkubwa kabla Mbappe hajakuwa staa. Hii ni katika ngazi zote. Klabuni na timu ya taifa. Baada ya kuondoka kwa Hugo Lloris kitambaa kilipaswa kwenda kwake kama ingekuwa tunaishi katika zama za zamani.

Zama za leo kitambaa kimekwenda kwa Mbappe. Jibu ni rahisi tu. Siku hizi mchezaji maarufu kuliko wote katika taifa ndio huwa anapewa kitambaa. Haijalishi kama ana sifa za kuwa nahodha au hana lakini ndiye ambaye anapewa kitambaa aongoze nchi. Mchezaji mwenye mvuto kuliko wote ndiye ambaye anapewa kitambaa.

Kwa Ufaransa mchezaji mwenye mvuto kuliko wote ni Mbappe. Ndiye mwenye ubora zaidi, pesa zaidi, anayezungumzwa zaidi, anayejulikana kwa watu wa mataifa mengine zaidi. Mtafute dada yeyote wa Kitanzania muwekee picha za Mbappe na Griezmann atakwambia anamfahamu Mbappe na sio Griezmann. Hii ndio hali halisi.

Haishangazi kuona pale Brazil nahodha ni Neymar. Zamani kitambaa angeweza kupewa Casemiro. Katika dunia anayoishi Pires nahodha angeweza kuwa hata Thiago Silva. Usishangae sana. Pele hakuwahi kuwa nahodha wa Brazil ingawa alikuwa mchezaji mwenye mvuto kuliko wote kikosini. Kitambaa kilikwenda kwa Carlos Alberto Torres.

Mwaka 1994 wakati Brazil ikitwaa Kombe la Dunia Marekani nahodha alikuwa Dunga ingawa Romario alikuwa staa zaidi. Leo kocha wa Brazil angelazimika kumteua Romario kuwa staa na sio Dunga. Leo pia Ronaldo de Lima angechaguliwa kuwa nahodha wa Brazil na sio Cafu. Maisha yamekwenda kasi na leo nahodha anakuwa na sifa nyingine.

Hapo hapo Ufaransa, nahodha wa mwaka 1998 alikuwa huyu Deschamps lakini katika dunia ya leo nahodha angekuwa Zinedine Zidane. Huyu ndiye alikuwa mchezaji mkali na mwenye mvuto zaidi katika kikosi cha Ufaransa. Deschamps angeishia kulalamika tu kama ambavyo Pires analalamika kwanini kitambaa hakikwenda kwa Griezmann.

Manahodha wa leo ni mastaa zaidi katika nchi. Lionel Messi ndiye nahodha wa Argentina. Cristiano Ronaldo ndiye staa wa Ureno. Harry Kane ndiye nahodha wa England. Mbwana Samatta ndiye nahodha wa Tanzania. Victor Wanyama ndiye nahodha wa Kenya. Kila staa mkubwa zaidi katika nchi ndiye anafanywa kuwa nahodha ingawa wapo wachezaji wenye sifa ya unahodha asilia kuliko wao.

Kwa mfano kwa zamani pale Argentina nahodha angeweza kuwa Rodrigo de Paul. Mtu wa kazi. Hata hivyo zama hizi tunahitaji mtu mwenye mvuto zaidi kikosini ambaye pia ni alama ya taifa zima katika soka. Ukiwasha televisheni yako wakati ukisubiri wachezaji wa Ufaransa waingie uwanjani kupasha misuli moto swali lako la kwanza kichwani au kwa jirani litakuwa “Mbappe yupo?” Hauwezi kujiuliza kama Griezmann yupo.

Kwa nchi zetu kama Tanzania mchezaji kama Samatta inakuwa muhimu zaidi kuwa nahodha pengine ilivyo Messi kwa Argentina au Mbappe kwa Ufaransa. Amewazidi wachezaji wote kikosini kwa umaarufu lakini pia utambuzi wa mambo (exposure) huku pia akiwazidi kwa kipato.

Haiwezi Samatta akaongozwa na Bakari Mwamnyeto kama nahodha wake. Samatta ameona mengi katika soka, amesikia mengi, amefanya mengi. Yeye ni mtu wa kutazamwa zaidi na wachezaji wenzake kuliko yeye kuwatazama zaidi wachezaji wengine. Yeye ndiye anayepaswa kuwaongoza wachezaji wenzake na sio kuongozwa na wao.

Mwamuzi yeyote anapomuona yeye inakuwa rahisi kumuheshimu kwa sababu anakuwa anaijua sura yake au amewahi kumuona mahali akicheza soka la juu. Kama sio kumuona itakuwa amewahi kumsikia. Ni tofauti na kundi la wachezaji wengine.

Hata hivyo, unahodha huu wa Mbappe umeanza kushika kasi zaidi katika timu za taifa lakini haupo katika klabu. Katika klabu nahodha anaweza kuchaguliwa kwa tamaduni zile zile za zamani. Anaweza kuwa mchezaji aliyecheza klabuni kwa muda mrefu kuliko wenzake. Anaweza kuchaguliwa kwa kuwa kijana wa mjini zaidi katika klabu anayochezea.

Kwa mfano, Manchester United nahodha ni Harry Maguire. Hakukuwa na ulazima wa kumpa Cristiano Ronaldo. Na hata sasa hakuna ulazima wa kumpatia Marcus Rashford. Arsenal nahodha ni Martin Odegaard ingawa staa wa timu anaelekea kuwa Bukayo Saka. Katika klabu tamaduni hazijabadilika sana na sioni kama zitabadilika.

Binafasi naamini nahodha wa klabu huwa anakuwa nahodha halisi kuliko nahodha wa timu ya taifa. Kwa mfano, sioni kama Mbappe ana sifa za unahodha. Anajisikia na ni kiburi. Sioni kama ana busara za kiongozi. Tayari ameshakorofishana na wachezaji wenzake kama Olivier Giroud kutokana na kiburi chake kinachotokana na ustaa wake au pesa alizonazo tukijumlisha na utoto wake.

Mtazame Ronaldo. Sioni kama anaweza kuwa nahodha halisi. Anasusa, ana majivuno, anajiweka yeye mbele kuliko timu. Lakini katika dunia ya leo ndiye anapaswa kuwa nahodha kwa sababu ni staa mkubwa zaidi katika nchi. Ni dunia ambayo tumejichagulia kuishi.

Messi naye sioni kama anastahili kuwa nahodha asilia. Ni mpole mno. Muda mwingi wachezaji wa Argentina hutumia kumlinda Messsi pengine kuliko ambavyo Messi anawalinda wenzake. Unakuwaje na nahodha ambaye anaonewa na wapinzani kuliko wachezaji wake? Hata hivyo, huyu ndiye alama ya soka Argentina na duniani.

Wakati mwingine naamini unahodha huu wa timu ya taifa katika miaka ya karibuni ni ule wa kumpa mchawi mwanao akushikie. Kwamba mchezaji staa zaidi kikosini ajihisi kuwajibika zaidi uwanjani kwa ajili ya kutetea taswira yake na ya timu kwa ujumla.

Sababu nyingine nadhani ni ile ya kumridhisha na kuunganisha timu. Ni rahisi kwa mchezaji staa kikosini kukiunganisha kikosi na kusiwepo makundi ndani ya timu kuliko anapokuwa nje kama mchezaji wa kawaida. Anapokuwa sio nahodha anaweza kuanzisha kundi ambalo litamsumbua nahodha na timu kwa ujumla.

Columnist: Mwanaspoti