Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwanini tusubiri wakubwa ili kufanya usafi?

0d5909b6201c91926443c6486f7b5efd Kwanini tusubiri wakubwa ili kufanya usafi?

Sun, 16 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba uchafuzi wa mazingira unaua watu wengi zaidi kila mwaka kuliko hata vita, maafa na baa la njaa.

Aidha, uchafuzi wa mazingira ndio chanzo kikubwa pia cha uharibifu wa uchumi. Jarida la matibabu la Lancet linasema kifo kimoja katika kila sita ya vifo milioni 9 vya mapema kote duniani katika mwaka wa 2015, vinaweza kuhusishwa na magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.

Aidha, ripoti hiyo inasema uchafuzi wa hewa ndio sababu kuu ya vifo hivyo, ukifuatiwa na uchafuzi wa maji, ambao uliua watu milioni 1.8. Ripoti hiyo pia imeonyesha gharama kubwa zinazotokana na vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, magonjwa na ustawi na kukadiria gharama hizo zinafikia dola bilioni 4.6 katika hasara za kila mwaka au sawa na asilimia 6.2 ya uchumi wa dunia.

Kutokana na ukweli huo tunaungana na Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango ya kuwataka viongozi waache kukaa ofisini na kutoka kuangalia usafi wa mazingira ili mambo yasituharibikie na kutudidimiza katika hatua zetu za kupaa kiuchumi.

Aidha, tunakubaliana na agizo lake la kuwataka wakurugenzi wa halmashauri na majiji nchini kuzingatia suala la usafi na kuhakikisha kuanzia wananchi mpaka wadau waliochukua zabuni za usafi wa mazingira wanalifanyia kazi.

Ni kweli kuwa hali aliyokutana nayo Makamu wa Rais katika ziara yake ya kuwepo kwa marundo ya uchafu katika Jiji la mfano (Dodoma) inaonesha ni kwa namna gani wananchi na wadau wengine wa usafi walivyojisahau katika kuhakikisha kwamba mazingira tunayoishi yanaakisi amani ya afya yetu na hivyo kutuwezesha kuchangia kikamilifu ukuaji wa uchumi.

Kama hali ya uchafu ikiendelea kuachwa namna hii, itakuwa ni tishio kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla kwani kama tulivyosema awali uchafuzi wa mazingira unaathiri uchumi kwa kuwa huua au kuharibu afya za watu; na katika maisha ya kawaida watu ambao ni wagonjwa au wafu hawawezi kuchangia katika uchumi, wanahitaji kutunzwa.

Ni hali ya kushangaza kuona uchafu umezagaa katika Soko Kuu la Majengo jijini Dodoma bila kuzolewa wakati ni Makao Makuu ya Taifa letu. Sasa inafaa kujiuliza kioo kama kikichafuka wengine watajionaje?

Ni vyema wananchi na watendaji wakajua na kuzingatia kwamba marundo ya uchafu si mapambo bali ni mashimo ya milipuko ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuhara mpaka magonjwa ya njia za hewa.

Hakika tunahitaji marekebisho makubwa katika suala la kuweka miji na maeneo yetu safi ili kuweka afya ya binadamu mahali pazuri kuwezesha kushiriki kikamilifu masuala ya uchumi na kuishi maisha marefu.

Shime watendaji tusisubiri viongozi wakuu kutuhimiza mipango ya usafi katika maeneo yenu ya kiutawala kwani kwa kufanya hivyo, kudhorotesha juhudi za usafi tutaleta madhara makubwa hasa kwa jamii maana huweza kusababisha vifo na hivyo nguvukazi ya taifa hupungua na kukwamisha maendeleo ya taifa hivyo kuleta changamoto kubwa kwa taifa kwa ujumla.

Columnist: www.tanzaniaweb.live