TATIZO la kutokwa harufu mbaya kwenye kinywa limekuwa likiwasumbua watu wengi, japo sehemu kubwa wanashindwa kujua chanzo chake na hata tiba sahihi.
Kuna mambo yanayochangia hali hiyo, lakini chanzo kikubwa ni uwepo wa mawe kwenye tezi ya koo ambayo kitaalamu inajulikana ‘tonsil stones’.
Inaelezwa kitaalamu, mawe hayo hayana hatari kubwa na mtu anaweza kuishi nayo kwa kipindi kirefu bila ya tiba. Hiyo ni sababu watu wengi wanaendelea kudumu na harufu mbaya kinywani kwa muda mrefu, pale wanapokosa matibabu.
Kuna wakati hali hiyo inampa muathirika harufu mbaya kinywani kiwango cha kushindwa kuficha kinachomkabili, maana harufu imetawala.
NINI CHANZO?
Tezi kwenye koo ‘tonsils’ ni sehemu ya mfumo wa ulinzi wa mwili, inayosaidia kuzuia vimelea vya kutoka nje vilivyoingia mwilini kwa njia ya mlo au kuvuta hewa.
Vitu kama vipande vidogo vya chakula, uchafu na chembe nyinginezo zinaweza kukwama na mtu akajikuta vinabaki katika mikunjo ya tezi za kooni.
Mikunjo hiyo inaweza pia kukusanya bakteria na chembe hai za mwili zilizokufa.
Wakati chembe hizo na bakteria zinapojikusanya katika tezi, askari wa mwili ‘chembe hai nyeupe’ huanza kazi ya kupambana nazo na pale kazi ya kushambulia inapokwisha hutengeneza vitu vigumu ‘mawe’ ambayo hubaki ndani ya tezi.
Hata hivyo, baadhi ya watu hujikuta wakimeza mawe pasipo kujua. Iwapo chembe hizo zinaendelea kubaki katikati ya mikunjo ya tezi inazidi kukua na hatimaye kubadilika mawe ya kwenye tezi au ‘tonsil stones’.
Hivyo, kladri mawe yanavyoshambuliwa na chembe hai nyeupe au yanapoendelea kubaki katikati ya tezi, inasababisha mtu kusikia maumivu kila mara nyingi anapomeza kitu kama chakula.
Mara nyingi, mawe katika tezi huwapata wenye umri mdogo pamoja na watu wazima wenye tezi ‘tonsils’ kubwa na wasiozingatia usafi wa kinywa.
Dalili za mawe kwenye tezi ya koo
mara nyingi huonekana kama chembe na rangi nyeupe, njano au wakati mwingine kijivu.
Hata hivyo, si mara zote mawe hayo yanaonekana mtu anapofungua kinywa, kwani kuna wakati yanajificha ndani kabisa ya mikunjo ya tezi na kusababisha yasionekane haraka.
Baadhi ya watu hawapati dalili zozote wanapokuwa na mawe kwenye tezi, licha ya viashiria mbalimbali.
Dalili kubwa ya mawe kwenye tezi, ni mtu kutokwa harufu mbaya kinywani ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na uwepo wa bakteria waliokaa kwenye mawe hayo.
Dalili nyingine za mawe ya tezi za koo ni pamoja na rangi nyekundu katika sehemu ya tezi kooni.
Pamoja na dalili hizo, kuna waathirika hupatwa na maumivu ya muda mrefu kooni na kuumwa tezi ‘tonsillitis’ linalojirudia kila mara.
Kuna wakati mtu mwenye mawe kwenye tezi hujisikia kama vile ana kitu kilichomkwama kooni, anachotaka kukimeza, lakini anashindwa.
MATIBABU YAKE
Mara nyingi mawe ya kwenye tezi, hayana madhara makubwa kwa muathirika, lakini wengi wanapenda yaondolewe kwa sababu ya harufu mbaya kinywani.
Wapo wanaofanya matibabu majumbani na hospitalini. Njia ya kwanza bora ni kuondolewa mawe kwa kutumia kijiti chenye pamba, kwa kuyachokonoa na kuyatoa kwenye tezi yalikojishikiza.
Hivyo mawe yanayoonekana kirahisi pale mtu anapopanua kinywa.
Ni njia inayotakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa, kwani tezi ni laini na kukosewa kuna madhara mengine.
Kuna wakati mawe yanajificha, hayaonekani kirahisi. Katika hali kama hiyo, mgonjwa humuona daktari na zaidi kazi humuangukia bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT), kufanya huduma ya kutoa matatizo hayo.
Iwapo njia hiyo haitafanikiwa, basi matibabu mbadala hufanyika.
Pili, kuna suala la kusukutua kinywa kwa maji ya chumvi; hiyo inasaidia kusababisha mawe kujiachia kwenye kuta za tezi na yanaweza kutoka kirahisi. Ni njia ambayo kwa wenye stadi hiyo kienyeji, hufanyika majumbani.
Tatu, kuna hatua inayotokea baada ya kutathmini tatizo la mawe kwenye tezi, daktari mhusika anaweza kumshauri mgonjwa afanyiwe upasuaji. Kitaalamu, injulikana kama ‘tonsillectomy.’
Hata hivyo, huwa ni uamuzi wa mwisho ambao daktari anatumia, iwapo hali ni mbaya na njia nyinginezo za matibabu zimeshatumika na hazifanikiwa kumaliza tatizo lililopo.
Hata hivyo, ni upasuaji unaoambatana na athari mbalimbali kama vile maumivu makali, kutokwa damu nyingi na madhara mengine ambayo ni lazima yapimwe vizuri katika uzani na daktari, kabla hajaruhusu kufanyika upasuaji.
Baada ya upasuaji wa kuondoa tezi, kasi ya kupona inategemea kiasi cha tezi kilichotolewa, japo kwa wastani mtu huchukua muda kato ya wiki moja na siku 10, kufikia hatua ya kupona kwa usahihi.
DAWA SAHIHI
Kuna Wakati dawa ya kuua bakteria (antibaiotiki) huweza kutumika kusaidia kuangamiza bakteria washiriki katika kukuza mawe hayo.
Hata hivyo matibabu ya namna hiyo si mazuri, kwa kuwa hayasaidii katika kuondoa mawe hayo au kuondoa kinachosababisha kutokea mawe.
Matibabu hayo, hayapaswi kutumika kwa muda mrefu, kwani inaweza kusababisha kujirudia tatizo hilo.
MADHARA YAKE
Ni nadra kuona mtu anapata madhara makubwa kutokana na mawe ya tezi. Hata hivyo, orodha ya madhara inajumuisha kuharibika kwa tezi la mgonjwa.
Kuharibika kwa tezi huja pale mtu anapotoa mawe yaliyopo, kwa kutumia vitu kama mswaki na nguvu zaidi inapotumika au kutokuwa umakini, inaumiza tezi husika.
Pia, katika upasuaji kuna wakati inaendana na kutokwa damu nyingi au kupata mashambulizi ya bakteria kwenye kidonda.
Hiyo inazuiwa kwa njia ya kuzingatia usafi wa kinywa. Inashauriwa, usafishaji meno na ulimi kila baada ya mlo, kabla ya kwenda kulala na mara tu baada ya kuamka ni muhimu.
Aidha, kutoa vipande vidogo vya chakula vilivyobaki katikati ya meno kila siku, hali inayosaidia kuondoa uwezekano wa kuwepo bakteria kinywani.
Kuna suala la kusukutua mdomo kila siku kwa kutumia maji maalum, kufanikisha usafi wa mdomo.
Kuna ushauri wa kitabibu kwamba, licha ya kuwapo mbinu nyingi za utaalamu wa afya, njia bora inaangukia katika hali halisi ya tatizo. Upasuaji bado inabaki njia nzuri na sahihi, suluhishi na ya uhakika.
•Mwandishi anapatikna kwa anwani ya baruapepe: [email protected]